Thursday, August 23, 2012

Hatimaye makarani wa Sensa walipwa


SIKU moja baada ya makarani wa Sensa ya Watu na Makazi kugoma kula kiapo cha utii na kutunza siri, Serikali imewalipa posho zao ili kuendelea na kazi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema makarani ambao hawakuwa wamelipwa posho zao, Serikali imeshawalipa na hakuna karani anayedai posho katika wilaya hiyo.
Rugimbana aliyasema hayo jana Dar es Salaam baada ya makarani zaidi ya 800 juzi kutishia kugoma kula kiapo cha utii na kutunza siri kabla ya kulipwa posho zao.
Alisema jana (juzi), kulikuwa na matatizo ya kifedha katika Manispaa ya Kinondoni na ndiyo maana kulikuwa na ucheleweshwaji wa kuwalipa makarani hao posho zao za mafunzo.

                                  


“Jana (juzi) kulikuwa na matatizo ya kifedha ambapo Manispaa ilichelewa kupata fedha kutoka hazina, lakini hadi jana asubuhi tulipata fedha hizo na kuwalipa makarani hao posho zao,” alisema Rugimbana na kuongeza:

“Makarani wote ambao jana (juzi) waligoma kula kiapo tuliwalipa fedha zao na kwamba kinachosubiriwa ni kuanza kwa kazi hiyo,” alisema.

Sunday, August 12, 2012

Bolt ashinda dhahabu ya tatu


LONDON, England
MWANARIADHA Usain Bolt ametwaa medali ya tatu ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki baada ya kuiongoza timu yake ya Jamaica kushinda mbio za 4x100m za kupokezana vijiti.
Timu ya Jamaica katika mbio hizo za 4x100m ilitumia muda wa sekunde 36.84 huku wanariadha wake Nesta Carter, Michael Frater, Yohan Blake na Bolt wakishirikiana vizuri kupata ushindi huo.
Bolt ndiye alimaliza mbio hizo kwa upande wa Jamaica akipokea kijiti kutoka kwa Blake na kumaliza mbio hizo kwa ushindi na kuufanya umati wa watu uliokuwa uwanjani kushangilia kwa nguvu.
"Nimefurahi sana kumaliza mashindano yangu kwa ushindi mkubwa, yalikuwa ni mashindano mazuri, nina furaha pia kwa timu yangu kupata ushindi kwa sababu wenzangu walijituma kweli na tulijotoa kwa dhati,"alisema Bolt.
                          
                                    

Alipoulizwa kama anatarajia kufanya hivyo katika michezo ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Rio de Janeiro, Bolt alisema,"itakuwa michezo migumu sana, hivi sasa Yohan Blake anakimbia vizuri sana, natumai pia kutakuwa na wanariadha wengi vijana katika michezo ijayo ya Olimpiki kwa hiyo itakuwa michezo migumu sana."
Wakati huohuo mwanariadha Mo Farah wa Uingereza ameshinda mbio za mita 10,000 katika michezo hiyo ya Olimpiki na kutwaa medali ya dhahabu.
Farah, 29, ambaye wiki iliyopita alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 alimaliza mbio za mita 10,000 na kuwashinda Dejen Gebremeskel wa Ethiopia na Thomas Longosiwa wa Kenya.

                                   


Farah ambaye mke wake ana mimba na anatarajia kujifungua watoto mapacha alisema,"siwezi kuamini kama nimeshinda, nilikuwa najisikia nimechoka, lakini nilipokimbia na kukaa mbele ya wenzangu nilisema natakiwa kupambana mpaka nishinde na kweli nilifanya hivyo."
Alisema,"medali zote mbili nilizozipata nazielekeza kwa watoto wangu wawili watakaozaliwa, nashukuru sana kupata medali katika michezo ya Olimpiki kwa sababu kupata medali mbili katika michezo ya Olimpiki siyo jambo dogo."
Uingereza ilikuwa haijawahi kutwaa medali ya dhahabu katika michezo ya riadha upande wa mbio ndefu katika michezo ya Olimpiki hivyo ushindi wa Farah ni faraja kubwa kwa Waingereza.

Anaconda auawa Bahari ya Shamu


Bahari ya shamu, MISRI
NYOKA wa ajabu (Anaconda) ambaye anadaiwa kuua zaidi ya watalii 320 na madereva 125 wa nchini Misri ameuawa juzi na wanasayansi pamoja na mabaharia wataalamu waliobobea katika fani hiyo wakishirikiana na madereva wa nchini Misri.
Mashujaa hao wa dunia ni pamoja na wanasayansi walioshiriki katika mchakato huo wa kumkimbiza nyoka huyo mpaka kuuawa ni pamoja na d. Karim Mohammed, d. Mohammed Sharif, d.  Mr Sea, d. Mahmoud students na d. Mazen Al-Rashidi
Majina ya madereva walioshiriki zoezi la kumuangamiza nyoka huyo mkubwa ni  Ahmed leader, Abdullah Karim, fisherman Knight, Wael Mohammed, Mohammed Haridi, spears Alvajuma, Mahmoud Shafik na a full-Sharif.


Mwili wa nyoka huyo umekuwa kivutio kwa watu wa nchi hiyo waliokusanyika kuuona mwili huo na sasa umekwishahamishiwa katika hifadhi ya Morgue katika kituo cha wanyama cha kimataifa kiitwacho Sharm El Sheikh.

Watu 250 wafariki dunia


AZARBAIJAN ,Iran
JUMLA ya  watu wasiopungua 250 wamefariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi ambalo limetokea kwenye mkoa wa Azarbaijan Mashariki nchini Iran. 
Mkurugenzi wa Kamati ya Migogoro ya mkoa wa Azarbaijan Mashariki ulioko magharibi mwa Iran Khalil Saei alisema watu hao wamefariki dunia baada ya  tetemeko hilo la  ardhi kuyakumba maeneo ya Ahar, Varzaqan na Haris.
Raia wa Iran wakijaribu kuwaokoa wenzao walionasa katika nyumba iliyobomolewa na tetemeko la ardhi juzi, zaidi ya watu 250 walifariki dunia. Picha na AFP

Aliongeza kuwa zaidi ya watu wengine 2000 wamejeruhiwa katika tukio hilo. 
Alisema kwamba  zaidi ya Vijiji 60 vya mkoa wa Azarbaijan vimeharibiwa kwa baina ya asilimia 50 hadi 80 kutokana  tetemeko hilo na timu za uokoaji zinaendelea kutoa misaada kwa walioathirika licha ya njia na barabara nyingi kuharibiwa. 
Tetemeko hilo ambalo lilikuwa na  ukubwa wa 6.2 kwa kipimo cha Rishta ulitokea juzi jioni, kituo chake kikuu kikiwa katika eneo la Ahar. 
Tetemeko jingine kama hilo lilikuwa na  daraja 6 kwa kipimo cha Rishta lilitokea saa 12 na dakika 4 jioni katika eneo la Varzaqan

Uchungu wa kuibiwa

Msanii Mohamed Nice 'Mtunisi' akilia baada ya kukamata CD feki walizozikamata kwa kushirikiana na Kampuni ya Steps Entataiment jana, Dar es Salaam.

Tuesday, July 31, 2012

Tanesco waendeleza libeneke na wezi wa umeme

Mtuhumiwa wa wizi wa umeme Jeilan Mohamed, akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi huku akiangalia mafundi wanavyong’oa mita ya umeme kwenye nyumba yake Buguruni Malapa Jijini Dar es Salaam jana kwenye zoezi linaloendelea la kukamata wezi.

Fundi Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tenesco)  Didas Lwinga, akiwaonyesha waandishi wa habari mita iliyofunguliwa na kubandikwa gundi (Super Glue) mara baada ya kuing’oa.


Mtuhumiwa wa wizi wa umeme Jeilan Mohamed, akiongozwa na jeshi la polisi kupanda gari baada ya kutuhumiwakuliibia umeme kwa njia ya kuunganisha kabla haujafika kwenye mita  maeneo ya Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam.





Sunday, July 1, 2012

Hivi mnapata wapi leseni?!..

Dereva wa lori akivunja sheria za usalama barabarani kwa kugeuza gari katika Barabara ya Mandera eneo la TOT jijini Dar es Salaam jana huku kukiwa na alama inayokataza tendo hilo. Kutoheshimu seria za usalama barabarani ni mojawapo cha vyanzo vya ajali nchini. Picha na Jube Tranquilino

Thursday, June 28, 2012

Huu ni UNYAMA



Mkurugenzi wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Hellen Kijo-Bisimba akiwa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka jana mara baada ya kumpata akiwa amepewa kipigo na watu wasiojulikana kabla ya kumpeleka hospitali kwa. Picha ndogo ni Daktari huyo kabla ya kipigo.
                                        
NI unyama. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka ametekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji Dar es Salaam.
Daktari huyo ambaye amekuwa akiratibu mgomo wa madaktari unaoendelea, aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono na miguu akiwa katika hali mbaya.
Baada ya kuokotwa na wasamaria wema na kufikishwa katika Kituo cha Polisi, Dk Ulimboka aliwahishwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) kwa matibabu, na ilielezwa kuwa hali yake haikuwa nzuri.
Taarifa za kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka zilisambaa kwa kasi katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu.
 Gari la wagonjwa lililokuwa limembeba Dk Steven Ulimboka likiingia katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana huku likiwa limezongwa na Madaktari.
                              

Kutokana na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu wameituhumu Serikali kuhusika na tukio hilo, huku Serikali ikikana tuhuma hizo, na papohapo ikiagiza Jeshi la Polisi kuwasaka waliohusika.
Akisimulia mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika klabu ya Leaders jijini Dar es Salaam, alikokuwa na wenzake wawili.
Alisema baada ya kukaa kwenye baa hiyo kwa muda, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku zingine.
"Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk. Ulimboka)," alieleza na kuongeza,
"Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini ilikuwa haina namba."
Madaktari wakiwa wamebeba Dk Steven Ulimboka kumwamisha kutoka katika Chumba wagonjwa mahututi baada ya kupata huduma ya kwanza kutokana kupigwa na watu wasiojulikana.
                                 
Taarifa zaidi kutoka Moi alikolazwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu, zilieleza kuwa baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa daktari huyo aliteswa vibaya, ikiwamo kuumizwa sehemu za siri, kuvunjwa meno kadhaa, mbavu na miguu.
Habari zaidi zilisema kuwa, baada ya kufikishwa katika Msitu wa Pande na kupata kipigo, alizimia kwa muda na alipozinduka aliwachomoka watekaji hao na kujaribu kukimbia. 
Msitu wa Pande ulioko wilayani Kinondoni, ndiko wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam waliuawa na polisi mwaka 2006.
Chanzo chetu cha habari kilisema, baada ya Dk Ulimboka kujaribu kuwatoroka watekaji, walipiga risasi mbili hewani, aliposimama wakamshika na kumpa kipigo na mateso zaidi, hivyo kusababisha avunjike maeneo mbalimbali ya mwili.
Polisi waunda tume
Jeshi la Polisi limeunda jopo kuchunguza tukio la utekaji nyara na shambulio la kudhuru mwili wa Dk Ulimboka.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa tukio hilo ni la aina yake na kwamba halijawahi kutokea hapa nchini.
Alisema jopo hilo ambalo linaongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ahmed Msangi linahusisha wapelelezi wa fani mbalimbali.
“Ni issue (jambo) ambayo imetokea bila kutegemea katika namna ambayo ina utata, hivyo kazi yetu ni kutegua utata huo,” alisema Kova na kuongeza:
“Hatutaki katika nchi yetu matukio kama haya yawe ya kawaida, tunataka liwe la mwanzo na la mwisho.” 
Kamanda huyo alisema yeye alipata taarifa za kutekwa Dk Ulimboka usiku wa kuamkia jana saa 7 usiku.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, Dk Ulimboka aliokotwa na raia mwema katika eneo la Msitu wa Pande jana saa 2:30 asubuhi karibu na barabara huku akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili, ikiwamo kichwani na mikononi. 
Alisema raia huyo (jina limehifadhiwa) alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Bunju, na askari walikwenda kwenye gari la raia huyo na kumkuta Dk Ulimboka wakamchukua na kwenda naye ndani.
  Kova alisema: “Aliyemuokota alisema alimkuta amefungwa mikono na miguu, na inaonekana kama watu hao walikuwa wanalipiza kisasi.”
Kwa mujibu wa kamanda huyo, akiwa kituoni hapo, Dk Ulimboka alijieleza kwamba juzi saa 5:30 usiku akiwa katika klabu ya Leaders na wenzake wanapata vinywaji pamoja na wateja wengine, walikuja watu watano na kuwatishia.
Alisema watu hao waliwataka walale chini na kwamba walitii, kisha watu hao walimchukua Ulimboka na kuwaambia wengine waendelee na vinywaji.
“Ulimboka alisema watu hao walikuwa na gari aina ya Escudo lenye rangi nyeusi na hili gari halikuwa na namba na walichukua ufunguo wake wa gari, nyaraka kadhaa na hela alizokuwa nazo,” alisema Kova.
Alisema akiwa katika gari hilo na watu wengine watano, ghafla walianza kumpiga huku wakiwa hawasemi chochote na kwamba baadaye walimfunika kichwani na fulana nyeusi hadi Msitu wa Pande.
Kova alisema baada ya maelezo hayo, Dk Ulimboka alitoa namba za simu za rafiki yake Dk Deogratius, na baada ya hapo alipewa fomu ya matibabu (PF3) na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi na mtu yeyote mwenye taarifa kamili kuhusu tukio hilo atoe taarifa, kwani lisipojulikana vizuri linaweza kuzua minong’ono mingi.

Askari ajeruhiwa MNH
Katika hatua nyingine, Kova alisema watu wasiojulikana wamemjeruhi Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi cha Selander Bridge ambaye alikwenda MNH kufanya upelelezi wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa Kova, Mkuu huyo wa upelelezi alijeruhiwa wakati akiwa anaongea na simu, na kwamba watu hao pia walimpora vitu alivyokuwa navyo ikiwemo simu.

Mkurugenzi Moi
Mkurugenzi wa Tiba katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Cuthbert Mchalo alisema majeruhi huyo alifikishwa hospitalini hapo saa 4:25  asubuhi, kwa msaada wa gari la wagonjwa la Kampuni AAR, kutoka Kituo Kidogo cha Polisi Bunju.
“Tumempokea, anaendelea vizuri na amepata maumivu katika maeneo ya kifuani, kichwani na tumboni,” alisema na kuongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Alifafanua kwamba kwa sasa wanajitahidi kumpatia matibabu, ingawa alipelekwa hospitalini hapo akiwa katika hali ambayo siyo nzuri, na uchunguzi zaidi unaendelea.

Wanaharakati walaumu Serikali
Miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika Kituo cha Polisi Bunju kumuona Dk Ulimboka ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba ambaye alisema kilichotokea kinaonyesha jinsi gani Serikali ilivyo na woga katika kushughulikia  matatizo ya wananchi.
Dk Bisimba alisema wao wanaamini kuwa tukio hilo lina mkono wa Serikali na kama ni kinyume cha hapo, basi inapaswa kuwaridhisha wananchi kuwa hawana mkono wao katika sakata hilo.
“Kama wao hawana mkono wao basi wanapaswa kuwaridhisha wananchi kuwa hawahusiki kwa kuwatia mbaroni wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria,” alisema Bisimba.
                               


Mkurugenzi huyo alisema matamshi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni jana kuwa wanashughulikia suala la madaktari na watalimaliza liwalo na liwe inaleta tafsiri kuwa kilichotokea kina mkono wao.
“Alivyosema liwalo na liwe na kinachotokea sasa kinabainisha kuwa mengi zaidi yatafuata,” alisema Bisimba na kuongeza kuwa hali hiyo inasikitisha na haikuwahi kufikiriwa.
Bisimba alisema baada ya wasamaria kumkuta mnamo saa 12:00 asubuhi, walimpeleka katika kituo kidogo cha Polisi cha Bunju ambako polisi walifungua mashtaka ya wizi wa maungoni na kupatiwa RB yenye namba BJ/RB/1870/2012.
“Mimi nilipata taarifa za kutekwa kwake kutoka kwa mwenzie aliyekuwa naye mnamo saa nane usiku, na baada ya kupata taarifa hizo niliwaeleza wanaharakati wenzangu juu ya hatua za kuchukua,” alisema Bisimba.

Bisimba alisema aliwasili katika Kituo cha Polisi cha Bunju, jana mapema asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka akiwa amejeruhiwa vibaya, lakini hakuwa amepatiwa huduma yoyote.
“Tulikwenda kumchukua na kukuta hali yake ni mbaya, lakini cha ajabu pamoja na majeraha yote hakupatiwa msaada wowote wa huduma, jambo ambalo lilitusikitisha sana,” alisema. 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sikika, Irenea Kiria alisema kilichotokea ni kitu kibaya na kinaonyesha jinsi gani Serikali inavyoshughulika na watu, badala ya kujali hoja za msingi ambazo zinawasilishwa.
Kiria alisema hoja za madaktari zilipaswa kusikilizwa kwani licha ya madai ya masilahi yao lakini pia wanapigania mazingira bora yenye utu kwa ajili ya wagonjwa.
Madai mengine ni upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wananchi pamoja na upatikanaji wa dawa, mambo ambayo alisema hayahitaji mjadala.

“Suala la masilahi ya madaktari linazungumzika lakini siyo suala la dawa, mazingira bora ya kuwahudumia wagonjwa na upatikanaji wa vifaa tiba na vipimo vingine,” alisema Kiria.

Nchimbi: Tutawasaka
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alisema Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika na utekaji huo.
  Dk Nchimbi alisema mjini Dodoma kuwa Serikali haihusiki kwa namna yoyote ile na utekaji nyara huo, na kwamba kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa kwani hakikubaliki katika jamii hasa kwa zama hizi.
 
                                 

“Kwanza, madaktari ni watu muhimu ambao wao ndio wanaotuwezesha sisi kuishi, kwa hiyo wapo kwa ajili ya maisha yetu, hata kama asingekuwa daktari, kwa mtu yeyote yule, jambo hili halikubaliki katika nchi yetu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:
  “Tumewaagiza polisi wafanye uchunguzi ili kuwabaini wahusika na wakipatikana wafikishwe katika vyombo vya sheria, maana hatuwezi kwa namna yoyote kuvumilia vitendo vya aina hii.”
  Alisema Serikali imestushwa sana na tukio hilo na haitavumilia kwa namna yoyote vitendo hivyo pamoja na vile vya unyanyasaji kwani ni kinyume cha sheria.
  Kuhusu kupigwa kwa Mkuu wa Upelelezi (OC- CID), ASP Mukiri, Dk Nchimbi alisema lilikuwa ni tukio la bahati mbaya kwamba madaktari waliokuwapo Muhimbili walishindwa kuwa na uvumilivu kwani askari aliyepigwa alikuwa ameagizwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela kwenda kufuatilia matibabu ya Dk Ulimboka.
  “Hapa ndipo ninapotofautiana na watu wengi, mnampigaje polisi, maana yule anapaswa kuwa rafiki wa raia, sasa unampigaje mtu ambaye ni mlinzi na umemwajiri, analipwa kwa kodi yako?” alihoji Dk Nchimbi.

                                


Yaliyojiri bungeni
Tukio hilo lililosambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, liliibuka bungeni, ambako Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alilaani vikali kitendo cha watu wanaodaiwa ni maofisa wa vyombo vya usalama kumpiga Dk Ulimboka.
Alisema kitendo hicho ni unyama unaostahili kukemewa na kila mpenda amani hapa nchini.
“Tumestushwa na tukio hilo na tunalaani vikali kitendo hicho na kumwombea Dk Ulimboka ili apone haraka,” alisema Mdee.

Katika hatua nyingine,  hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana, kujionea hali ilivyokuwa baada ya kusambaa kwa taarifa za kupigwa kwa Dk Ulimboka.
Katika hospitali ya Mwananyamala, wengi walioonekana walikuwa ni wauguzi huku madaktari wakidaiwa kwenda katika hospitali ya Muhimbili kumuona mwenzao aliyejeruhiwa.
Dk Ulimboka aliwahi kufanya kazi katika hospitali hiyo ya Mwananyamala katika miaka ya nyuma.
Hata hivyo, juhudi za waandishi kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo, hazikufanikiwa baada ya wafanyakazi wa Ofisi ya Mganga Mkuu kusema kuwa mganga huyo amekataa kuzungumza, akiwataka waandishi wafike ofisini kwake leo.
Wagonjwa wakiwa wodini katika hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi jana huku mgomo wa madaktari ukiwa umepamba moto na kusababisha kliniki zote hospitali hiyo kufungwa na wagonjwa wanaohudumiwa ni wale tu waliokutwa na mgomo wakiwa wodini na wa matibabu ya dharura.
“Ameniambia niwapeleke kwa katibu wake, lakini na yeye nimemkosa, sasa nimerudi kwake ameniambia niwaambie mrudi kesho,” alisema katibu muhtasi wake.
Katika hospitali za Temeke na Amana, hali pia ilikuwa hivyo, baadhi ya wahudumu waliokutwa katika hospitali hizo wakikataa kuzungumza kwa madai kuwa wanaotakiwa kuzungumza hawapo.

Madaktari jeshini waitwa kazini

 Taarifa zilizotufikia wakati tukienda mitamboni, ambazo hazijathibitishwa, zilieleza kwamba madaktari wote wanaofanya kazi kwenye hospitali za jeshi ikiwamo Lugalo ambao hawakuwa zamu jana jioni, waliitwa kazini, tukio ambalo linahusishwa na tamko la Serikali linalotarajiwa kutolewa leo.

Monday, June 25, 2012

Lulu bado njia panda


                                              
SERIKALI imezidi kumweka katika wakati mgumu msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, anayekabiliwa na kesi ya tuhuma za mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Hatua hiyo inatokana na hatua ya upande wa mashitaka kukwamisha usikilizwaji wa kesi hiyo kwa kuwasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya kupitiwa upya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kukubali kufanya uchunguzi wa umri sahihi wa mshitakiwa huyo.
Umri wa Lulu umeibua utata wa kisheria baada ya upande wa utetezi kusema mteja wao ana miaka 17 na si 18 kama Hati ya Mashitaka inavyoonyesha, hivyo unadai kisheria anapaswa kushitakiwa katika Mahakama ya Watoto huku ule wa mashitaka ukipinga hoja hiyo.
Kufutia hali hiyo, mshitakiwa huyo aliyefika Mahakama Kuu jana Jumatatu kusikiliza shauri la utata huo wa umri wake, alishindwa kujizuia na kumwaga machozi baada ya mahakama hiyo kusimamisha shauri hilo.
                                          
Katika kesi yake ya msingi iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lulu anatuhumiwa kumuua Kanumba usiku wa Aprili 7, 2012 nyumbani kwa marehemu, Sinza, jijini Dar es Salaam.
Utata wa umri wa Lulu ulitarajiwa kusikilizwa hiyo jana Jumatatu na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Juni 11, 2012 Mahakama Kuu iliamua kufanya uchunguzi wa usahihi wa umri wa msanii huyo kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanaomtetea.
Lakini jana Jumatatu, Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, asema mahakamani hapo kuwa upande wa Jamhuri tayari imewasilisha maombi Mahakama ya Rufani kuomba uamuzi huo wa Mahakama Kuu uliotolewana Jaji Dk. Fauz Twaib ufanyiwe marejeo.
Jaji Dk. Twaib alikubaliana na maombi haya Jamhuri na kusimamishwa usikilizwaji huo hadi Julai 9, 2012, ikiwa Mahakama ya Rufani itakuwa imemaliza kushughulikia maombi hayo ya Serikali.
Kabla ya mahakama kufikia uamuzi huo, mawakili wa Lulu, Kennedy Fungamtama na Peter Kibatala, walipinga maombi ya serikali wakidai ni mbinu ya kuchelewesha shauri hilo.
                               
                                

Fungamtama alidai kuwa hadi wakati huo mahakama ilipoanza hapa kuwa na amri yoyote ya Mahakama ya Rufani ya kusimamishwa usikilizwaji wa suala la utata wa umri wa mteja wao.
“Hata kwenye maombi haya hakuna maombi yanayoelekeza kusimamishwa kwa usikilizwaji wa maombi haya,” alisema Fungamtama.
“Kinachofanywa hapa ni matumizi mabaya ya mamlaka ya Ofisi ya DDP (Mkurugenzi wa Mashtaka).”
Kwa upande wake, Wakili Kibatala, alidai kuwa maombi hayo ya Jamhuri kwa Mahakama ya Rufani hayaoneshi mazingira ya kusimamishwa kwa usikilizwaji wa maombi hayo na kwamba hiyo inabaki kwa mamlaka ya Mahakama Kuu yenyewe.
“Lakini kwa maslahi ya mshtakiwa ambaye anaendelea kuteseka mahabusu, tunaiomba mahakama hii iamuru usikilizwaji wa maombi haya (utata wa umri ) uendelee,” alisisitiza Kibatala.
Lakini akijibu hoja hizo, Wakili Kaganda, alidai ofisi ya DPP inatambua matakwa ya haki na kwamba inatenda kwa matakwa ya haki haitumii vibaya mamlaka yake.


Lulu anaendelea kushikiliwa rumande kwa vile aina ya shitaka linalomkabili halina dhamana kisheria.