LONDON, England
MWANARIADHA Usain Bolt ametwaa medali ya tatu ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki baada ya kuiongoza timu yake ya Jamaica kushinda mbio za 4x100m za kupokezana vijiti.
Timu ya Jamaica katika mbio hizo za 4x100m ilitumia muda wa sekunde 36.84 huku wanariadha wake Nesta Carter, Michael Frater, Yohan Blake na Bolt wakishirikiana vizuri kupata ushindi huo.
Bolt ndiye alimaliza mbio hizo kwa upande wa Jamaica akipokea kijiti kutoka kwa Blake na kumaliza mbio hizo kwa ushindi na kuufanya umati wa watu uliokuwa uwanjani kushangilia kwa nguvu.
"Nimefurahi sana kumaliza mashindano yangu kwa ushindi mkubwa, yalikuwa ni mashindano mazuri, nina furaha pia kwa timu yangu kupata ushindi kwa sababu wenzangu walijituma kweli na tulijotoa kwa dhati,"alisema Bolt.
Alipoulizwa kama anatarajia kufanya hivyo katika michezo ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Rio de Janeiro, Bolt alisema,"itakuwa michezo migumu sana, hivi sasa Yohan Blake anakimbia vizuri sana, natumai pia kutakuwa na wanariadha wengi vijana katika michezo ijayo ya Olimpiki kwa hiyo itakuwa michezo migumu sana."
Wakati huohuo mwanariadha Mo Farah wa Uingereza ameshinda mbio za mita 10,000 katika michezo hiyo ya Olimpiki na kutwaa medali ya dhahabu.
Farah, 29, ambaye wiki iliyopita alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 alimaliza mbio za mita 10,000 na kuwashinda Dejen Gebremeskel wa Ethiopia na Thomas Longosiwa wa Kenya.
Farah ambaye mke wake ana mimba na anatarajia kujifungua watoto mapacha alisema,"siwezi kuamini kama nimeshinda, nilikuwa najisikia nimechoka, lakini nilipokimbia na kukaa mbele ya wenzangu nilisema natakiwa kupambana mpaka nishinde na kweli nilifanya hivyo."
Alisema,"medali zote mbili nilizozipata nazielekeza kwa watoto wangu wawili watakaozaliwa, nashukuru sana kupata medali katika michezo ya Olimpiki kwa sababu kupata medali mbili katika michezo ya Olimpiki siyo jambo dogo."
Uingereza ilikuwa haijawahi kutwaa medali ya dhahabu katika michezo ya riadha upande wa mbio ndefu katika michezo ya Olimpiki hivyo ushindi wa Farah ni faraja kubwa kwa Waingereza.