Friday, April 13, 2012

Kanumba alijitabiria kifo filamu yake ya mwisho


Mpiga picha na mhariri wa filamu za Steven Kanumba, Zakayo Magulu amesema kifo cha msanii huyo kinafafana na hadithi ya filamu yake ya mwisho aliyoigiza, inayoitwa Price of Love ambayo bado haijatolewa.

Mugulu alisema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican, Dar es Salaam.

Alisema filamu hiyo ambayo Kanumba aliibadilisha jina na kuiita Power and Love inaeleza jinsi msanii huyo alivyotoa figo na baadaye kufa baada ya kusukumwa na mpenzi wake katika filamu hiyo ambaye alikuwa ni Irene Paul.

Akiielezea filamu hiyo ambayo bado haijatoka licha ya kuwa imeshakamilika, alisema Kanumba aliigiza kama mtu maskini aliyempenda msichana ambaye alikuwa na uhusiano na mwanamume tajiri.

“Katika filamu ile Kanumba alitoa figo yake moja baada ya huyo msichana (mpenzi wake) kuugua na kutakiwa kuwekewa figo nyingine. Alipotoa Figo uliibuka ugomvi baina yake na mpenzi wake ambaye alimsukuma na Kanumba alianguka na kuumia. Baada ya tukio hilo, alikimbizwa hospitali na baada ya muda mfupi alifariki dunia.”


Alisema msanii, Idrisa Makupa maarufu kama Kupa ndiye aliyeona kifo cha Kanumba katika filamu hiyo na pia hata baada ya kifo chake, ndiye mtu wa mwisho kuuona mwili wa Kanumba ukiingizwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuufunika…. “Ni mambo ya ajabu.”

Alisema hata daktari aliyemfanyia operesheni Kanumba katika filamu hiyo ndiye huyo huyo aliyefika nyumbani kwa Kanumba kumpatia huduma baada ya kuanguka.

Alisema tukio la kifo cha Kanumba katika filamu hiyo iliyoandikwa na Ali Yakuti halikuwepo ila liliongezwa na msanii huyo mwenyewe… “Filamu hiyo ilikuwa na matukio (scene) 84 lakini, yalibadilishwa matukio 40 likiwemo la kifo chake.”

Mchaguaji wa maeneo ya kupigia picha za filamu za Kanumba, Rahim Khatib maarufu kama Kiuno alisema katika filamu hiyo ya mwisho ya msanii huyo alipendekeza picha zipigwe katika maeneo yenye giza na mwanga halisi (usio wa taa).



Mtoto wa Kanumba

Katika hatua nyingine imebainika kuwa Kanumba (28), ameacha mtoto mmoja wa kiume.

Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu, mama mzazi wa msanii huyo, Flora Mtegoa alisema: “Kama kuna aliyezaa na mwanangu ajitokeze na familia itamsikiliza.”

Taarifa za Kanumba kuacha mtoto zilikuwa gumzo jana nyumbani kwa marehemu ambako baadhi ya ndugu walioonekana kufurahia na wengine kupinga wakidai kuwa mtoto huyo na marehemu.

“Leteni hilo gazeti…, hao wanaojitokeza waje tu mimi ndiyo nafurahi waache wawalete wajukuu zangu,”alisema Mtegoa baada ya kuelezwa kuwa taarifa hizo ziliwahi pia kuripotiwa na moja ya magazeti nchini (siyo Mwananchi).

Hata hivyo, baada ya mama huyo kutoa kauli hiyo dada yake marehemu Kanumba, Abella Kajumulo alisema mtoto huyo si wa mdogo wake kwa sababu katika uhai wake Kanumba hakuwahi kuieleza familia yake kama ana mtoto wala mke.

“Mbona huyo mwanamke hakujitokeza wakati wa msiba wa Kanumba aje kujitokeza hivi sasa? Niliwahi kumwuliza (Kanumba) juu ya ndoa yake na kama ana mtoto alikataa kabisa akasema hana mtoto wala mke,” alisema Kajumulo.

Wakati ndugu hao wakibishana kuhusu habari hizo, aliibuka kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Patrick Kamwele na kuwaeleza kuwa mtoto huyo ni wa Kanumba na kwamba anamfahamu vizuri msichana huyo.

Kamwele ambaye ni raia wa Kenya aliingia mkataba na kampuni ya Kanumba The Great tangu mwaka 2009 na katika mazungumzo yake na ndugu hao aliwaeleza kuwa atakuwa shahidi iwapo atahitajika kufanya hivyo.

Alisema mara ya kwanza kumwona msichana huyo ilikuwa Septemba 2009, baada ya kufika nyumba kwa Kanumba kwa ajili ya kufanya mazungumzo kabla ya kuingia naye mkataba.

“Baada ya kukaa nyumbani kwa Kanumba kwa muda wa wiki mbili huyo msichana, alianza kuumwa na Kanumba alimpeleka hospitali na alibainika kuwa ni mjamzito,” alisema Kamwele.



Alifafanua kwamba baada ya msichana huyo kusema kuwa mimba hiyo ni ya Kanumba, yeye pamoja na baadhi ya wasanii wa bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia, waliitwa katika kikao na msanii huyo.

“Katika kikao kile tulimhoji msichana huyo na alisema mimba ni ya Kanumba, ila baadaye msichana huyo aliondoka ingawa mimi sijui kama alifukuzwa au aliondoka mwenyewe,” alisema.

Alisema kilichoendelea baada ya hapo hakukijua mpaka alipokuja kuiona habari hiyo katika gazeti jana.

Mmoja wa wasanii wa filamu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema anamfahamu msichana huyo na kwamba alikuwa mfanyakazi wa ndani wa Kanumba.

Msanii huyo alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na Kamwele mbele ya ndugu zake Kanumba, huku akitizama picha ya msichana huyo katika gazeti na alisema: “Namfahamu huyu msichana alikuwa msichana wa kazi wa Kanumba.”

Kamwele aliwataka ndugu wa marehemu Kanumba kulichukulia suala hilo kwa umakini kwa kuwa hawawafahamu watu wote waliokuwa wa karibu wa msanii huyo.

“Mimi nimekaa na marehemu Kanumba kwa muda mrefu na ninawajua waliokuwa watu wake wa karibu akiwemo huyo msichana, nawashauri kulipa uzito suala hili,” alisisitiza Kamwele.


Familia yatoa utaratibu

Katika hatua nyingine, mama wa marehemu Kanumba amewaomba radhi wananchi wote kwa kitendo cha kukatisha ratiba za kuuaga mwili wa msanii huyo juzi katika Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Mutegoa alisema ratiba hiyo ilikatishwa kutokana na watu kuwa wengi na kusababisha kuibuka kwa vurugu… “Sikutegemea kama watu wangekuwa wengi kiasi kile mpaka wengine kufikia hatua ya kupoteza fahamu… nawaomba radhi wote waliofika, pamoja na hayo wingi ule wa watu ulinipa faraja kubwa. Wameonyesha upendo wa hali ya juu.”
Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Sinza Vatican huku taarifa za awali zikieleza kuwa kifo chake kilitokana na ugomvi na aliyekuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.

Ali Kiba ahojiwa polisi kwa kumpa lifti Lulu

Ali Kiba

Msanii wa muziki wa Bongo Flava, Ali Kiba, anadaiwa kuhojiwa na polisi kwa maelezo ndiye aliyempa Elizabeth Michael ëLuluí msaada wa usafiri (lifti) baada ya kutoka kwa Steven Kanumba.
Lulu ndiye anayetuhumiwa kuhusika na kifo cha Kanumba kilichotokea usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
Kachelo aliyemhoji Lulu Jumatatu wiki hii, amedai kuwa msanii huyo alihojiwa katika kituo cha Polisi cha Oysterbay kutokana na kutajwa na mtuhumiwa kuwa ndiye aliyempatia lifti baada ya kutoka kwa Kanumba.
Mwanaspoti lilimtafuta Ali Kiba ili azungumzie taarifa hizo, alipopatikana kwa njia ya simu, msanii huyo alisema: ìSamahani kaka siwezi kuzungumzia chochote kuhusu mambo hayo.î Kisha akakata simu.
Lulu alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jumatano wiki hii na kutotakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji.
Lulu alitoa maelezo yake polisi Jumatatu ikiwa ni saa 65 tangu kutokea kwa kifo cha Kanumba., ambapo alizungumza na kachero wa Makao Makuu ya Polisi ambaye pia ana taaluma ya saikolojia.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kachero huyo (jina tunalo) aliyetoka makao makuu alifanikiwa kufanya mahojiano na binti huyo ambaye awali aligoma.
Imeelezwa kuwa, alitumia takribani sasa tatu kumlainisha Lulu azungumze.
Katika mahojiano , kachero huyo ambaye alitoka katika Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai alisema tayari amemhoji mtuhumiwa namba moja Lulu pamoja na msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya kufuatia kifo cha Kanumba, aliyefariki usiku wa kuamkia Jumamosi.
Akimnukuu Lulu katika mazungumzo yake, kachero huyo alisema Lulu aliitwa na marehemu Kanumba ili waweze kutoka (out) kwenda kwenye bendi ya Mashujaa ambayo ilikuwa inapiga kwenye kiwanja chao cha nyumbani, Vingunguti.
Lulu

Mtuhumiwa alionekana kutokuwa tayari, lakini marehemu ëakamlazimishaí.
Kachero huyo alisema: "Lulu anadai alifika nyumbani kwa marehemu saa tano usiku, lakini akiwa ameweka msimamo wa kutokwenda sehemu yoyote usiku ule, lakini Kanumba alikuwa akilazimisha ndipo yakatokea mabishano na marehemu akafunga mlango kwa funguo.
"Hata hivyo, baada ya ugomvi wa kama nusu saa hivi, Lulu alifanikiwa kuondoka chumbani humo na alifungua mlango kwa taharuki na kuondoka bila kujua kilichotokea nyuma, huku akimweleza ndugu wa marehemu kwamba Kanumba ameanguka."
Mpashaji habari wetu huyo alisema, kumekuwa na jumbe fupi za maneno kutoka kwa wanasiasa ambazo zimekuwa zinaingia kwenye simu ya kiganjani ya Lulu, zikiahidi kumsaidia.
Alionya kuwa kama wanasiasa wataanza kuingilia uchunguzi wa Polisi katika kesi hiyo ambayo imevuta hisia za watu wengi, wanaweza kuharibu mambo. Lakini yeye mwenyewe akionyesha kwamba yuko imara na anafahamu anachokifanya.
Kuhusu msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ali Kiba, kachero huyo alisema kwamba alihojiwa kutokana na kutajwa na mtuhumiwa kama mtu aliyempatia msaada wa usafiri (lifti) baada ya kutoka kwa Kanumba.
Kachero huyo alisema kutokana na taarifa ambazo wanaendelea kuzipata, kuna uwezekano watu wengi zaidi wakahojiwa ili kujiridhisha kabla ya ëwatuhumiwaí kuanza kupandishwa kizimbani baada ya upelelezi kukamilika.

MCT yawaonya wanahabari kuhusu ‘Lulu’


Baraza la Habari Tanzania (MCT), limewaasa waandishi wa habari kuzingatia maadili ya kazi yao hasa wakati huu wa kuripoti kesi inayomhusu Elizabeth Michael ‘Lulu’.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili wa MCT, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alisema kuwa wadau wa tasnia ya habari wamekuwa wakimuhukumu moja kwa moja Lulu kuwa ndiye aliyemuua Steven Kanumba.

“Kwa mjibu wa sheria na maadili ya uandishi wa habari mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ile ni mtuhumiwa mpaka atiwe hatiani na mahakama,” alisema Jaji Mihayo na kuongea:

“MCT inasikitishwa na baadhi ya vyombo vya habari kwa ukiukwaji wa maadili uliojitokeza wakati vikiripoti kuhusu kifo cha Kanumba, vimemuhukumu Lulu kuwa ameua kinyume na maadili ya kazi yao.”

Jaji Mihayo alisema kuwa MCT kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa matamko yanayowakumbusha wanahabari kujiepusha na uandishi wa habari au vichwa vya habari vinavyohukumu.

“MCT inatambua fika kesi zilizoko mahakamani ni kivutio kwa umma kutaka kujua kinachopendelea ili kuona haki ikitendeka na pia wanahabari wana haki ya kujua na kuripoti yanayojiri huko na katika vyombo vingine vya sharia,” alisema Jaji Mihayo na kuongeza:

“Wanahabari ni lazima watambue kuwa kuna taratibu na makubalianao ya kijamii juu ya namna taarifa zinavyopaswa kuripotiwa ili kutowadhuru watu wengine.”



Naye Katibu Mkuu wa (MCT), Kajubi Mukajanga alisema kuwa mwandishi wa habari ana uwezo wa kuifanya jamii ikaamini na kumfikiria Lulu moja kwa moja kuwa ndiye aliyemuua Kanumba jambo ambalo si kweli mpaka lithibitishwe mahakamani.

Kuhusu taarifa ambazo zimekuwa zikienezwa na mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Kanumba kuwa zimesabishwa na Lulu alisema Mukajanga alisema kuwa MCT hawahusiki na mitandao hiyo.

Mukajanga alisema atafuatilia kujua nini kilisababiaha kuwepo kwa usiri kwa polisi kutotoa taarifa ya wapi Lulu alitakiwa kufikishwa mahakamani ili waandishi wa habari wapate nafasi ya kufanya kazi yao.