Monday, January 30, 2012

Dk Mwakyembe ajitokeza hadharani, arusha kombora


Hatimaye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe jana alijitokeza hadharani na kusema amepona huku akiapa kuendeleza vita dhidi ya mafisadi hadi kifo chake.

Dk Mwakyembe aliondoka nchini Desemba 9, mwaka jana kwenda katika Hospitali ya Appolo, India kwa matibabu baada ya kuugua maradhi yaliyosababisha ngozi yake kuharibika na tangu arejee alikuwa hajawahi kuonekana katika hadhara ya watu.

Jana, waziri huyo alionekana mwenye afya njema huku akiwa amevalia suti, glovu nyeusi na kofia aina ya pana.

Akiwa na kundi la makada wenzake wa CCM wanaojipambanua kupambana na ufisadi, akiwemo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, Dk Mwekyembe alisema awali, alikuwa na hali mbaya kiafya lakini sasa anamshukuru Mungu kwa kuwa anaendelea vizuri.

Mwakyembe na kundi hilo walikuwa katika uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima na kuongozwa na Mchungaji Josephat Gwajima, Dk Mwakyembe.

Wengine waliohudhuria ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Mbunge wa Viti Maalumu Mbeya, Hilda Ngoye, aliyekuwa Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro na Mjumbe wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkoa wa Kilimanjaro , Paul Makonda.


Mbali ya kuapa kuendeleza mapambano dhidi ya mafisadi, Dk Mwakyembe pia alitoboa siri ya afya yake akisema: “Nilifika hospitalini Oktoba 10 (mwaka jana), na tangu wakati huo sikuweza kuvaa viatu lakini leo hii naweza kuvaa viatu, kwa hiyo shetani ameshindwa.”

Alisema atatumia siku za Jumapili kuzunguka katika makanisa mbalimbali kwa lengo kumkemea shetani.

Sitta atoa tuhuma

Kwa upande wake, Sitta ambaye ni mshirika wa karibu kisiasa wa Dk Mwakyembe alirejea kauli yake ya awali kuwa Naibu Waziri huyo alilishwa sumu.

“Nasema Dk Mwakyembe kapewa sumu. Kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo basi watueleze ukweli, tena haraka” alisema Sitta na kushangiliwa na maelfu ya waumini wa kanisa hilo.

“Vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia lakini baada ya saa moja unarudi tena, kitu hicho siyo cha kawaida. Wamejaribu, wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote. Kwa hiyo nuksi, kurogwa kuwekewa sumu ni kama maji katika mgongo wa bata, yanatiririka tu na kwenda zake,” alisema Sitta.

Alisema mafisadi wapo kwa ajili ya kuangamiza taifa na kuwaangamiza viongozi wanaotetea maslahi ya wananchi na kutokana na hali hiyo, siku zao zina hesabika.

“Mungu yupo kwa ajili ya kutetea wanyonge na si kuwalinda mafisadi hao... ndiyo maana Dk Mwakyembe amepona. Kwa sababu alikuwa miongoni mwa watu wanaotetea maslahi ya wananchi,” alisema.

Tumejipanga

Kwa upande wake, Kilango alisema kundi lao la wapiganaji na wapambanaji wa ufisadi lipo makini kutetea maslahi ya taifa na si watu wachache akisema wamejitoa muhanga kwa ajili ya kuwashughulikia.

“Kundi letu limeundwa kwa ajili ya kutetea maslahi ya Watanzania, ndiyo maana tulikuwa na nguvu kwenye Bunge la Tisa la kasi na viwango ambalo lilikuwa linafanya uamuzi wa haki bila ya kumuonea mtu, kutokana na hali hiyo tumejipanga upya, tutawashughulikia,” alisema.

Alisema Bunge hilo lililoongozwa na Sitta lilikuwa makini kwenye uamuzi na kwamba hawataogopa kulishwa sumu wala kutishiwa maisha akisema wako tayari kwa lolote kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi na wana imani kwamba watashinda.

Naye Lembeli alisema Mungu amemponya Dk Mwakyembe na sasa yuko tayari kufa kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi huku Ngoye akisema amezaliwa ili kutetea maslahi ya wananchi na kupambana na walafi, wala rushwa na mafisadi wanaodhulumu haki za wananchi.

“Tumerudi kwa kishindo, kwa ajili ya kutetea haki zenu, tunaomba mzidi kutuombea ili tuweze kuwashughulikia, hatuwezi kuona wananchi wananyonywa na wachache wakati wenyewe wananeemeka,” alisema Ngowe.

Kwa upande wake, Kimaro alidai kwamba mafisadi walitumia zaidi ya Sh120 milioni kwa ajili ya kumng’oa jimboni kwa sababu alionekana ni miongoni mwa watu wanaojifanya wana kimbelembele katika kutetea maslahi ya taifa.

Alisema licha ya kutoka bungeni, msimamo wake utabaki palepale, kutetea maslahi ya wa wananchi na Watanzania kwa ujumla... “Haiwezekani rasilimali za Watanzania ziliwe na wachache. Tutapambana iwe kwa jua au mvua,” alisema Kimaro.


Madaktari waendeleza libeneke

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Haji Mponda, Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa busy na simu zao Muhimbili jana, wakiwa katika harakati za kunusuru mgogoro ili madaktari warejee kazini.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Haji Mponda, Naibu wake Dk. Lucy Nkya (kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia (kulia) wakijadili jambo kabla ya kutambulisha katika mkutano wa madaktari katika hoteli ya Starlight kabla ya kutimuliwa kikaoni hapo.