Thursday, October 27, 2011

Mume wa Kim Kardashian apigwa chini


NI takribani wiki nane zimepita tangu staa wa televisheni, Kim Kardashian afunge ndoa na mcheza kikapu, Kris Humphries lakini ndani ya muda huo matukio mengi yamewakumba wanandoa hao.
Habari zinasema kuwa baada ya Hamphries kufunga ndoa na Kim, walikubaliana kuwa na yeye angekuwa sehemu ya kipindi cha televisheni cha Keeping Up With The Kardashian.
Lakini kampuni inayotengeneza kipindi hicho imekataa kumuingiza mwanamume huyo kama mmoja wa washiriki huku akielezwa kuwa kama atataka kutokea hata lipwa hata senti.
Kampuni inayoandaa kipindi hicho, William Morris Endeavor Entertainment imemkataa Humphries ikisema kuwa haitakuwa na mkataba wowote na mcheza kikapu huyo linapokuja suala la malipo.
Wakati Humpries akipigwa chini kwenye kipindi hicho, habari zimezagaa kuwa wawili hao wako mbioni kutalikiana. Inaelezwa kuwa Kim yuko mbioni kueleza sababu za kuoana na kuachana katika kipindi kifupi.

Miranda Kerr aonyesha sidiria ya almasi


KUNA usemi kuwa almasi ndiye rafiki wa kweli wa mwanamke, lakini kwa Miranda Kerr kwake imekuwa zaidi anapofikia kuvaa sidiria iliyonakshiwa kwa vito vya madini hayo.
Miranda ambaye asili yake ni Australia amenunua sidiria hiyo kwa dola za Marekani 2.5mil. Anatarajia kuionyesha inavyokaa pale anapoivaa katika fasheni shoo itakayofanyika Novemba 29 mwaka huu.
Watengenezaji wa sidiria hiyo, wamemuomba Miranda ashiriki katika onyesho la mavazi maalumu kwaajili ya kuonyesha sidiria hizo ambazo unapoivaa unapaswa kuwa na ulinzi wa kutosha.
Onyesho hilo litarushwa moja kwa moja katika kituo cha televisheni cha CBS.
Sidiria moja imewagharimu watengenezaji masaa mia tano ambayo ni wastani wa siku 20. Vipande 3400 vya almasi vimetumika kunakshi sidiria hiyo.

Cher Lloyd umaarufu haujanizidi


LONDON, Uingereza
CHER Lloyd ambaye ni staa wa shindano la uimbaji nchini Uingereza, X Factor amesema umaarufu alioupata haujabadili maisha yake.
Lloyd amesema tangu aingie kwenye shindano hilo maisha yake yamebadilika kwa kutazamwa tofauti na watu lakini si katika maisha yake binafsi.
Binti huyo mwenye umri wa miaka 18 amesema bado ananunua nguo katika maduka yaleyale aliyokuwa akinunua zamani.
"Watu wakishapata umaarufu huwa wanabadili kila kitu wakati mwingine hata marafiki, lakini mimi bado nanunua nguo katika maduka yaleyale ya watu wa kaiwada na pia marafiki zangu ni walewale," alisema Llyoid.
Mwanamuziki huyo chipukizi anasema jamii inataka kumbadilisha lakini hakubaliani na hali hiyo kwani anataka kuendelea na maisha yake ambayo ni mazuri sana.
"Kuna siku niliingia kwenye duka moja ambalo linasifika kwa kuwauzia nguo mastaa, bei zake zilinishtua sana na niliondoka bila kununua chochote,
Lakini pia kuna siku nilikutana na mashabiki wangu katika maduka ya kawaida wakaniuliza kwanini ninafanya manunuzi katika maduka yale,niliwajibu ndiyo maisha yangu ya kila siku na hayawezi kubadilika," alisema Lloyd.

Mama Yeyoo aendelea kulia vichwa Ubungo

Mwanamke wa Kimasai akimnyoa mteja wake kandokando ya barabara ya Morogoro eneo la Stendi ya mabasi ya ubungo jijini Dar es Salaam jana.

Zitto hali mbaya, ahamishiwa Muhimbili

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akiwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam kutokana na kusumbuliwa na homa. Kulia ni rafiki wa Mbunge huyo, Alex Kitumo.


Hali ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye alilazwa katika Hospitali ya Aga Khan, ilibadilika ghafla jana jioni kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Zitto alilazwa Aga Khan juzi jioni baada ya kusumbuliwa na maumivu ya kichwa kabla ya kuruhusiwa na kisha kurudishwa baada ya maumivu hayo kuendelea.

Kaka wa mbunge huyo, Salum Mohamed alisema jana jioni kwamba hali ya mdogo wake ilikuwa ikiendelea vyema lakini ilibadilika ghafla na kuanza kutetemeka.

“Hali yake ya Zitto imegeuka kuwa mbaya, anatetemeka mwili mzima na sasa tunampeleka Muhimbili kwa uangalizi zaidi,” alisema Mohamed.

Jana jioni, mwandishi wa gazeti hili alimtembelea Zitto Aga Khan jana majira ya saa kumi jioni na kumkuta akiwa anaendelea vyema. Zitto, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alisema maeneo mengine katika mwili wake yalikuwa yamepona isipokuwa maumivu ya kichwa.

Awali, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, Erasto Tumbo alisema Zitto anasumbuliwa na ugonjwa wa kipanda uso.