Tuesday, September 20, 2011

Mourinho kumbadili Fergie


Kocha wa Manchester United, Alex Ferguson anataka kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho achukue nafasi yake pindi atakapoacha kazi katika klabu hiyo.
Kocha huyo anaamini Mourinho ndiye atakayelinda heshima ya Old Trafford kwa kunyakua vikombe vingi iwezekanavyo.

Ferguson, ambaye amekuwa karibu na kocha huyo wa Ureno tangu mwaka 2007 aliongeza kuwa Mourinho ana uzoefu wa kutosha na anafahamu misingi ya kazi.
Mtu mmoja ambaye anawafahamu watu hao alisema; "Alex na Jose ni watu wa karibu sana. Alex atafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kocha huyo anatua katika klabu hiyo." Jose alikuwa na matatizo akiwa Real Madrid kutokana na kukwaruzana na watu mara kwa mara lakini Alex anafahamu namna ya kuwashawishi viongozi wa juu ili wamkubali. "Kocha huyo alijiimarisha vya kutosha alipokuwa katika Ligi Kuu England na alipoondoka alishitua watu wengi."

Rita Dominic aanza kupotea


Rita Dominic amesema kwamba si kwamba amegoma kushirikishwa kwenye filamu za wasanii wengine bali amewapa vigezo na ndio maana hatokei katika kazi nyingi siku hizi.

Msanii huyo mwenye mvuto amedai kuwa si yeye tu hata mastaa wenzake wameanza kupotea makusudi ili kuongeza ubora kwenye filamu za Nollywood.
"Siyo mimi tu hata na wengine wameanza kufanya kazi kwa masharti, si kushiriki kila filamu kwavile umepewa fedha. Ubora wa filamu umeanza kuporomoka sana Nollywood, kama mtu hataki kufanya kazi yenye ubora hatanipata wala siwezi kushiriki.
"Hakuna sababu ya kuendelea kufanya mambo ndivyo sivyo, tunataka kuhamasisha watu wafanye na kuandaa kazi nzuri."

Jamani..kha! Msinifuatefuate


Uche jombo amesisitiza kuwa amefunga mjadala unaomhusisha na mwanasoka wa Nigeria, Ikechukwu Uche na wala hataki kusikia magazeti yakiendelea kumuuliza.
Imekuwa ikiripotiwa kuwa wawili hao wana uhusiano wa kimapenzi na wana mipango ya kufunga ndoa siku zijazo. Lakini ameruka vikali na kusisitiza; "Msinifuatefuate."

"Ngoja nikusaidie kwa kuwa najua kila mtu anataka kujua nini kinaendelea kwa ubaya na uzuri. Nataka uelewe kwamba sitaki kusikia wala kuzungumzia tena hilo suala, nashangaa kila mtu anafukuafukua tu kutaka kujua nini kinaendelea,"alisema.
"Siwezi kuzungumzia chochote kuhusiana na Uche na nimefunga mjadala, sipendi muendelee kuzungumzia mambo ambayo hayapo, mnapotezea watu muda waache wasome mambo ya maana."

Kama unamtaka Shilole soma hapa


Inaezekana nafasi iko wazi, ebu jaribu! Binti anayekuja juu katika tasnia ya filamu Bongo, Zuwena Mohamed 'Shilole' amesema anapenda kuolewa na mwanaume anayejishughulisha na si kijana mvivu anayetegemea mwanamke.
Msanii huyo mwenye haiba, ambaye ameshiriki katika filamu nyingi zinazofanya vema mtaani amesema; "Sipendi mwanaume anayekaa tu bila ya kufanya kazi zaidi ya kushinda maskani tu, bali nataka mwanaume mchakarikaji, anayefanya kazi kwa nguvu kwa ajili ya kuendeleza familia yetu na kujiongezea kipato zaidi, haiwezekani kuwa na mwanaume tegemezi asiye na msaada kwa familia yake."

"Maana siku hizi kuna wanaume nao wakiona mwanamke mjasiriamali tu, hawataki kazi wakitegemea wanawake zao, wanaume wa namna hiyo kwangu marufuku siwahitaji kabisa hawana nafasi," anasema Shilole.
Msanii huyu ambaye ameshiriki katika filamu ya Mafisadi wa Mapenzi, anamiliki Duka la Nguo pamoja na duka la vinywaji linaloitwa Shilole Pub maeneo ya Mwananyamala, Dar es Salaam.

Arsenal ubingwa bye bye! Tafuteni nafasi ya nne


Ni mambo ya ajabu kuona kikosi chenye nguvu cha Arsenal kikihangaika kutaka kupanda bila mafanikio! Timu hiyo imekuwa ikijaribu kunyanyuka lakini mara kadhaa imeendelea kuzama kuelekea chini ya msimamo wa Ligi Kuu England.
Timu hiyo tayari umecheza mechi tano za Ligi Kuu England lakini imedumaa katika msimamo wa Ligi. Ilianza vibaya lakini wiki iliyopita ilizinduka baada ya kupata ushindi dhidi ya Swansea, lakini ghafla wikiendi iliyopita ilipata kibano cha mabao 4-3 kutoka kwa Blackburn Rovers. Aibu si kufungwa pekee, aibu inakuja kwa kuwa wamefungwa na klabu ambayo imekuwa ikijitahidi kutokushuka daraja.
Jambo hilo linamfanya Wenger ajikute katika maswali mengi ambayo majibu yake huenda yasipatikane katika siku za karibuni. Na huu ndio ukweli wa Arsenal kwa sasa.

Mabeki wabovu
Kuruhusu mabao manne maana yake ni kwamba kuna mashaka makubwa katika nafasi ya beki. Sasa mabeki hao tayari wameruhusu mabao 14 katika mechi tano tu, hali itakuwaje siku za usoni?
Sasa washambuliaji wapya na wa zamani wanaweza kucheza kwa makini na kusaka mabao mengi iwezekanavyo lakini kama upande wa beki umepwaya, timu haiwezi kufanya mambo ya maana, watakuwa wakibahatisha kila kukicha. Mchezaji wa zamani wa Bundesliga, Per Mertesacker ndio alionekana uchochoro kabisa.

Mertesacker vilevile alihakikisha ushindi wa Blackburn baada ya kushindwa kufunga bao kwa njia ya kichwa umbali wa mita tatu tu kutoka kwa kipa.
Ni kweli matatizo hayawezi kumwelemea mtu mmoja lakini kwa kawaida roho huuma wakati unapofahamu kwamba ulikuwa na nafasi ya kuisaidia timu yako lakini hukufanya hivyo.
Na katika matukio kadhaa beki mwingine wa kati Laurent Koscielny naye amekuwa hatoi mchango mkubwa wa kuisaidia timu yake na kuna wakati huonekana kama vile anawasidia wapinzani.
Kitendo cha kujifunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Blackburn kinaonyesha kuwa mabeki wa kocha Wenger bado wana safari ndefu kuelekea kwenye mafanikio.

Wenger mtegoni
Ni kweli kocha Arsene Wenger ni mtu anayeheshimiwa katika klabu baada ya kutoa matunda katika siku za nyuma lakini kila kiti kina mwanzo na mwisho. Kama kocha huyo hatatafuta mbinu kubwa ya kufanya timu ianze kushinda itakuwa ni kazi kubwa kuendelea kutesa katika klabu hiyo.

Mashabiki walianza kumzomea Wenger baada ya kufungwa mabao 8-2 na Manchester United na huenda kichapo kutoka kwa Blackburn kikaongeza hasira si tu kwa mashabiki bali pia kwa viongozi wa ngazi ya juu.

Washambuliaji wazuri
Arsenal ilipoanza mechi dhidi ya Blackburn Rovers ilionekana kuwa ngumu na washambuliaji walionekana kuwa imara.
Gervinho na Mikel Arteta walifunga mabao yao ya kwanza katika klabu hiyo na Marouane Chamakh naye alizifumania nyavu.
Washambuliaji walionekana kuwa makini na walionana vizuri kabla ya mabeki kusambaratika. Sasa ni wakati wa washambuliaji kujidhatiti zaidi katika kutafuta mabao mengi iwezekanavyo ili mabeki wanapofanya uzembe waweze kuwabeba.

Arsenal ifikirie nafasi ya nne
Huenda Arsenal imeanza kujitoa taratibu katika kusaka ubingwa na badala yake inabidi itoke jasho kuhakikisha inashika nafasi ya nne mwishoni mwa msimu. Itakuwa ni ndoto kwa wao kuwania ubingwa kwa kuwa katika mechi tano za awali wameshinda mara moja, wametoka sare mara mbili na kufungwa mara mbili, hizo ni mechi za awali, je mechi zijazo zitakuwaje?
Huwezi kusema kuwa timu hiyo inaweza kushuka daraja kwa kuwa ni mapema sana lakini ubingwa umeanza kuyeyuka.

Walilie bahati
Vile vile wanatakiwa kuombea bahati la sivyo kila mara wataishia kupata majonzi. Ni vigumu kuelewa waliruhusu vipi mabao manne dhidi ya Blackburn lakini unaweza kusema kuwa bahati iliwatupa mkono.