HALI ya usalama katika Jimbo la Igunga inazidi kuwa tete baada ya milio ya risasi kurindima usiku wa kuamkia jana katika tukio lenye utata mkubwa, huku vyama vya Chadema na CCM vikiendelea kushutumiana.
Wakati CCM) ikidai risasi hizo zilifyatuliwa na Mratibu wa Kampeni wa Chadema, Mwita Waitara, Chadema wanadai risasi hizo zilifyatuliwa na Mbunge wa Sumbawanga mjini, Aishi Hilal wa CCM.
Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku wa kuamkia jana nje ya nyumba ya kulala wageni ya Misana Lodge ambapo magari mawili aina ya Toyota Landruicer na Toyota Prado yalivunjwa vioo.
Gari hiyo ya Toyota Landcuiser linaelezwa kumilikiwa na Mbunge Hilal na Prado inadaiwa kuwa ni ya Mbunge wa Viti Maalumu CCM, Ester Bulaya, ambaye CCM kinadai kuwa wafuasi wa Chadema walitaka kumteka.
Eneo lilipotokea tukio hilo ndiko ambako wafuasi wa Chadema wanalala ikiwamo kulaza magari yao yakiwamo yanayotumika katika kampeni na magari ya wabunge hao yapo katika Kituo cha Polisi Igunga kwa uchunguzi.
Naibu Kamishina wa Polisi Isaya Mngulu, ambaye ndiye Msemaji wa Polisi katika Uchaguzi Mdogo Jimbo la Igunga alithibitisha jana kuwapo kwa tukio hilo na kueleza kuwa silaha iliyotumika ni bastola yenye kipenyo cha milimita tisa.
“Hatujafanikiwa kuipata bastola hiyo lakini kutokana na maganda mawili ya risasi tuliyoyaokota eneo la tukio, inawezekana silaha iliyotumika ni bastola ya milimita 9,”alisema Mngulu.
Naibu Kamishina huyo alisema tayari watu zaidi ya 10 wamekwishahojiwa na polisi na kuandikisha maelezo yao wakiwamo Wabunge hao wawili, Waitara na walinzi watatu walioshuhudia tukio hilo lenye utata.
“Mpaka sasa hatuwezi kusema vioo vya magari yale vilivunjwa kwa kutumia risasi au mawe na hili ni moja kati ya mambo tunayoyachunguza, ikiwamo ni nani hasa aliyefyatua risasi zile,” alisema Mngulu.
Katika tukio hilo, kada mmoja wa CCM aliyekuwamo katika gari la Mbunge Bulaya aliyetajwa kwa jina la Ramadhan Twaha, alidai kuwa amejeruhiwa kwa risasi katika mkono wake wa kushoto na kutibiwa kisha kuruhusiwa.
Lakini Kamishina huyo wa polisi alisema kuwa, asingependa kuingia kwa undani kuhusu tukio hilo, ila polisi wameshaanza uchunguzi.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo, polisi walipekua chumba anachoishi Waitara pamoja na cha dereva wa moja ya magari ya Chadema, lakini hawakukuta bastola yeyote ndani ya vyumba vyao.
Eneo kulipotokea tukio hilo ni umbali wa meta 20 hivi kutoka Hoteli ya Peak ambayo wamefikia viongozi wa kitaifa wa CCM.
Maelezo ya Bulaya
Akizungumza na Waandishi wa habari jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya alidai kuwa usiku huo alikuwa ametokea Baa ya Silent Inn akiwa na wabunge wenzake wawili akiwamo Aishi.
Mbunge alidai wakati anatokea katika baa hiyo kuelekea katika Hoteli ya Peak walikofikia viongozi wa CCM, waliona gari ya Chadema ikija mbele yao katika barabara ya lami kuelekea Peak na kuwamulika kwa taa kali.
“Wakawa wanakuja kwa speed (mwendo kasi), ikabidi tuwakwepe. Wakati tunakweoa tuligonga kibao. Baada ya tukio hilo ikabidi dereva wetu ageuze gari tukaanza kukimbilia barabara ya kuelekea Singida,” alidai Bulaya.
Alidai kuwa baada ya kuwakwepa, Waitara alitoa bastola na kufyatua risasi hewani kulishambulia gari lao huku vijana wengine wa Chadema waliokuwa wamepakiwa nyuma ya gari hilo, wakirusha mawe.
“Ikabidi mimi nimpigie simu Mbunge Aeshi kumweleza kuwa hawa watu wanataka kuniteka naye akawasiliana na polisi ambao walikuja kusaidia. Baada ya Waitara kuona kuna gari linawafuata wakakimbilia porini,” alidai.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, baada ya kuona Waitara na kundi lake wanafuatwa ndipo walipogeuza gari na kurudi hoteli waliyofikia na kuingiza gari lao ndani ya geti na wakati huohuo, polisi wakafika.
Mbunge huyo alidai kuwa Mwita alianza kumwinda yeye na Aeshi muda mrefu. Wengine aliodai kuwa walikuwa wanawindwa ni Mratibu wa Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigella.
Alifafanua kuwa juzi kabla ya tukio hilo, aliwakamata vijana wa Chadema wakiwa na fomu walizoziandaa kwa lengo la kuorodhesha wapiga kura na kununua shahada jimboni humo, kitendo kilichomuudhi Waitara.
Mbunge Aeshi anena
Mbunge huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa muda mfupi baada ya kuachana na Bulaya, alipokea simu kutoka kwake (Bulaya) akimwarifu kuwa amevamiwa na alikuwa akielekea Singida hivyo aende kumwokoa.
“Kwa hiyo nilimwambia dereva ageuze gari tukaanza kuwafuata nyuma kuelekea Singida na nilipowakaribia nikampigia Esther nikamwambia niko nyuma yake na nimeshalifahamu hilo gari linalomfukuza,” alisema.
Alisema baada ya kulibana sana gari hilo liliingia porini naye akalifuata huko na ndipo likageuza kurudi mjini na yeye akaendelea kulifukuza na kwamba, akiwa njiani alikutana na polisi wa doria akawaarifu.
“Polisi nao wakatufuata hadi pale wanapokaa, lakini wanaonekana ni wajanja sana maana tulikuta gati (lango) likiwa wazi gari lao likaingia moja kwa moja hadi ndani na wakati huo polisi wakafika,” alidai.
Alidai kuwa wakiwa katika taharuki hiyo, ghafla gari yake ilipigwa kwa risasi kioo cha pembeni ambayo ilipita na kuvunja pia kioo cha upande wa pili na kwamba, tukio hilo lilishuhudiwa na polisi waliokuwa eneo hilo.
Tundu Lissu awageuzia kibao CCM
Mkurugenzi wa Sheria na Katiba wa Chadema, Tundu Lissu, alisema jana kuwa vijana wao ndio waliovamiwa na kundi la Vijana wa CCM wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga mjini, Aeshi.
“Lengo lao lilikuwa ni kuchoma magari yetu moto, baada ya kugundulika kuwa wameingia katika eneo la hoteli tulipokaa, vijana wetu walianza kupiga kelele na kuizunguka ile gari ya Mbunge wa Aeshi,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa baada ya mbunge huyo kuona amezungukwa alichomoa bastola na kufyatua risasi hewani watu wakalala chini akatoroka, lakini ile gari yake ilidhibitiwa hadi polisi walipokuja.
Alifafanua kuwa polisi walilichukua gari lile na kumtafuta Mbunge huyo na kumpeleka kituoni.
Lisu alisema anashangaa badala ya polisi kumkamata mbunge huyo kwa matumizi mabaya ya silaha, walimwachia huru.
“Badala ya kumweka ndani kama walivyowaweka ndani Wabunge wetu waliotuhumiwa kumvua yule Mkuu wa Wilaya kilemba cha kichwani wakawaachilia na badala yake wanakuja kumpekua Waitara,” alisema.
Alidai kuwa mtu aliyetoa taarifa polisi kuwa Waitara ana silaha ni Mbunge Esther Bulaya aliyekuwepo pia kwenye tukio hilo la saa 8:00 usiku na kumtuhumu kwa kuwatukana polisi alipofika kituo cha polisi Igunga.
“Yule mbunge aliyefyatua risasi yupo huru bunduki yake anayo… na Rage (Ismail) aliyekuwa na bunduki juzi kwenye mkutano wa hadhara yupo huru licha ya makatazo ya tume ya uchaguzi…,”alilalamika.
Alisema jeshi la polisi linatumika kama chombo cha mabavu badala ya kutumika kama chombo cha kulinda amani na kwamba, wakiambiwa wakamate watu wa Chadema wanawakamata bila kuuliza.
Waitara azungumza
Kwa upande wake, Mwita Waitara alisema anashangazwa na hatua ya Mbunge Bulaya kumsingizia tukio kubwa kama hilo.
Aliwaambia Waandishi wa habari kuwa wakati wa tafrani hiyo yeye alikuwa amelala chumbani kwake na alishtuka usingizini kutokana na kelele alizozisikia nje.
Waitara alisema pamoja na yeye kutokuwapo kwenye gari usiku huo, anashanagzwa na hatua ya polisi kumkamata na kumshikilia kwa saa kadhaa.
Chadema wataka mgombea
CCM aenguliwe
Lissu alisema tayari Chadema kimemwandikia barua Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Uchaguzi kulalamikia kitendo cha Mbunge wa Tabora mjini, Ismail Aden Rage, kutembea na bastola waziwazi hadharani.
Kutokana na kitendo hicho, Chadema kimemwomba mwenyekiti wa kamati hiyo ya maadili kukiomba mgombea wa CCM, Dalaly Kafumu, aondolewe kwenye kampeni kutokana na ukiukwaji huo wa maadili.
Lissu alisema Ibara ya 2(2) ya Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ilivyofanyiwa marekebisho Septemba 20, mwaka huu inakataza kubeba silaha yoyote inayoweza kudhuru mtu yeyote katika mikutano ya kampeni.
Alilitaka Jeshi la polisi kumkamata Rage na wabunge waliofyatua risasi na kuwaweka rumande akisema kama hilo litafanyika ataamini jeshi hilo linatenda haki kwa usawa na bila upendeleo.
Polisi kumhoji Rage
Naibu Kamishina wa polisi, Mngulu alisema polisi watamhoji Mbunge wa Tabora Mjini Aden Rage kwa kitendo chake cha kutembea na bastola hadharani.
“Tutaanza kwa kumhoji Mheshimiwa Rage kwa nini alitembeza na bastola na uchunguzi utakapokamilika tutatuma kwa wataalamu wa sheria ili wafanye ufafanuzi kwamba katika hali ile inakuwaje,” alisema.
CCM nao watoa tamko
Katibu wa NEC Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba alisema jaribio la kutaka kutekwa kwa wabunge wao wawili usiku wa kuamkia jana ni mwendelezo wa matukio ya vurugu dhidi ya wana-CCM na viongozi wake.
Nchemba alisema yeye na wabunge hao wamekuwa wakiwindwa kwa muda mrefu na Chadema baada ya wao kubadilisha upepo na kuwafanya vijana wabadilike na kuamua kukiunga mkono CCM.
Katibu huyo ambaye pia ni mratibu wa kampeni za CCM jimbo la Igunga amelaani tukio hilo na matukio mengine, akiwataka polisi kuwakamata wote waliotajwa kuhusika kuwashambulia wabunge hao.
Zitto Kabwe atua Igunga
Katika hatua nyingine Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe, jana aliingia katika Jimbo la Igunga kuongeza nguvu ya kampeni kwa chama chake cha Chadema na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa wanachama na wapenzi wa chama hicho.