Friday, January 6, 2012

Twende tukaone maajabu Rubondo


Ninashawishika kuwaalika watanzania wenzangu kwamba twendeni tukaone maajabu katika hifadhi inayoundwa na visiwa 11. Hii ni nyingine bali ni hifadhi ya Rubondo iliyopo wilaya ya Geita Mkoani Mwanza, ikiundwa na visiwa ambavyo ni

makazi ya ndege na wanyama wa aina mbalimbali.

Kwa namna vinavyoonekana, Rubondo ambayo iliyoanzishwa Januari 1977, inafananishwa na lulu ya kijani ndani ya ziwa Viktoria.

Inafikika kwa boti kupitia kituo cha Nkome wilayani Geita au Muganza upande wa wilaya ya Chato mkoani Kagera.

Awali kisiwa kilikaliwa na jamii ya Wazinza na kumbukumbu ipo eneo la 'Maji Matakatifu' yaliyotumika kwa tambiko la kupata baraka za miungu na samaki walipendelea eneo hili kuliko sehemu nyingine.


Wapo wanyama wa asili na baadhi hawapatikani katika hifadhi nyingine kama aina ya nzohe'statunga' huku hifadhi ikiwa na historia ya kuwa na uoto wa asili mithili ya misitu ya Kongo.


Moja ya matukio ya kushangaza ni ufundi wa baadhi ya wanyama ambao huogelea mpaka visiwa vingine vya hifadhi na baadhi hugeuka chakula cha wanyama wengine waishio majini.

Mkuu wa hifadhi Herman Batiho anasema mbali na kujivunia hazina ya wanyama kama tembo, twiga, viboko na mbega pia ni sehemu pekee unapoweza kuwaona kasuku wa kijivu kutoka Afrika Magharibi.

Ni eneo pekee ndani ya ziwa Viktoria linalotunzwa kwa ajili ya mazalia ya samaki.

Changamoto za kimazingira zinaongeza umuhimu wa sehemu hii kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi yanayotegemea rasilimali za ziwa.


Kubadilika kwa ubora wa maji ni dalili ya kubadilika kwa ikolojia ya ziwa ambapo matokeo ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tafiri) mwaka 2009 sangara walipungua kutoka tani 750,000 mwaka 2006 hadi 227,365 mwaka 2010.


Ujangili mkubwa sio wa vipusa vya faru na tembo kama hifadhi ya Serengeti bali uvuvi wa sangara na watoto wao.

Mkuu wa hifadhi hiyo anasema ulinzi umeimarishwa kwa ajili ya usalama wa viumbe waliopo.


Kuelekea Kisiwa cha ndege

Safari ya kukifikia kisiwa cha ndege inapitia visiwa kadhaa ambavyo vina kila aina ya vivutio ukiwemo mwamba mkubwa ambacho ni kituo maalumu kwa ajili ya malezi ya watoto wa mamba.

Mayai huanguliwa kisiwa jirani na watoto husafirishwa kinywani hadi kwenye mwamba kuwakinga na maadui.


Baadhi hufa wakati wa safari na wachache hulindwa dhidi ya ndege hadi hatua ya kujitegemea.

Kisiwa cha Chambuzi kinapambwa na maelfu ya ndege kutoka Mashariki ya mbali, Afrika na Ulaya ambao hukimbia usumbufu utokanao na shughuli za binadamu na msimu wa baridi kali.


Kwa mujibu wa Christina Kibwe, mtaalamu wa ikolojia katika hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo ni eneo pekee unapoweza kuona aina zaidi ya 200 za ndege na maelfu ya viota vyao vilivyochimbwa ardhini.


Hata hivyo ni vigumu kumuona ndege aina ya domo kiatu ambaye yuko katika kundi la vivutio vinavyotoweka na hupendelea maeneo ya ardhi oevu, kando ya mito na mabwawa.


Domo ni aina ya ndege wanaojulikana kitaalamu kama ‘balaeniceps rex’ na yuko hatarini kutoweka baada ya makazi yake kuharibiwa. Chakula chake kikuu ni samaki aina ya kambale na kamongo ambao huwasubiri waibuke.

Mtafiti katika Idara ya Zuolojia na uhifadhi wa viumbepori Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jasson John anakiri ndege huyo atapotea katika uso wa dunia kama hatua za kumnusuru hazitachuliwa sasa.

Anasema ni kivutio kikubwa na hapa nchini wanakadiriwa kubaki ndege 200 ambao inabidi walindwe kwa mujibu wa sheria za wanyamapori na kuwa wapo ndege kati ya 5,000 na 8,000 waliobaki duniani.


Utafiti wa Mradi wa Mazingira wa Rufiji wa mwaka 2003 unatetea maarifa ya kimila na kisayansi kulinda viumbe hai. Mathalani wakazi wa maeneo hayo waliamini nyama ya kiboko hailiwi kwani hurutubisha maziwa kwa kinyesi.

Maarifa ya kimila mbali na kuokoa vizazi vya wanyama wa asili kama ilivyo katika hifadhi ya Rubondo, pia yamesaidia kuhifadhi maelfu ya hekta za misitu iliyoaminika kuwa makazi ya mizimu wakiogopa kuikasirisha kwa kuchoma moto.


Uhusiano na vijiji jirani

Utulivu wa ziwa uliniwezesha kusafiri bila shida katika boti ndogo hadi kijiji cha Nyabugela baada ya siku tatu za kutembelea visiwa vilivyozunguka hifadhi ya taifa Rubondo.

Vijiji jirani mbali na kufaidika na utalii pia vinaweza kusaidia utekelezaji wa sheria namba 5 ya mwaka 2009 inayozuia usafirishaji wa wanyama hai na kufanikisha mipango ya kudhibiti wizi wa rasilimali ambapo sekta ya utalii inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa.