SIKU moja baada ya makarani wa Sensa ya Watu na Makazi kugoma kula kiapo cha utii na kutunza siri, Serikali imewalipa posho zao ili kuendelea na kazi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema makarani ambao hawakuwa wamelipwa posho zao, Serikali imeshawalipa na hakuna karani anayedai posho katika wilaya hiyo.
Rugimbana aliyasema hayo jana Dar es Salaam baada ya makarani zaidi ya 800 juzi kutishia kugoma kula kiapo cha utii na kutunza siri kabla ya kulipwa posho zao.
Alisema jana (juzi), kulikuwa na matatizo ya kifedha katika Manispaa ya Kinondoni na ndiyo maana kulikuwa na ucheleweshwaji wa kuwalipa makarani hao posho zao za mafunzo.
“Jana (juzi) kulikuwa na matatizo ya kifedha ambapo Manispaa ilichelewa kupata fedha kutoka hazina, lakini hadi jana asubuhi tulipata fedha hizo na kuwalipa makarani hao posho zao,” alisema Rugimbana na kuongeza:
“Makarani wote ambao jana (juzi) waligoma kula kiapo tuliwalipa fedha zao na kwamba kinachosubiriwa ni kuanza kwa kazi hiyo,” alisema.