Tuesday, April 24, 2012

Hakimu ambembeleza Lulu mahakamani


Msanii wa filamu, Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akibubujikwa machozi kiasi cha kumfanya Hakimu Ritha Tarimo ambembeleze ili kumnyamazisha.
Lulu anashtakiwa mahakamani hapo kwa kutuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba na alifikishwa jana kwa mara ya pili akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.
Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 3:06 asubuhi akiwa katika basi dogo la Magereza pamoja na mahabusu wengine wanawake ambalo lilikuwa likisindikizwa na magari mengine mawili na alikuwa chini ya ulinzi wa askari sita wa kike wa Magereza na askari mmoja wa kike wa Polisi wakishirikiana na askari wa kiume wa Magereza zaidi ya sita.
Mara baada kuingia katika chumba cha Mahakama, Lulu ambaye alikuwa amevalia dira jekundu alianza kulia kwa uchungu hali ambayo ilimlazimu Hakimu Tarimo pamoja na baadhi ya askari kumnyamazisha.
Ulinzi ulikuwa wa kufa mtu



Ilikuwa ni kazi kupata picha yake, hata JK halindwi namna hii!




Kutokana na kujaa kwa watu mahakamani hapo, askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza walilazimika kuufunga mlango wa Mahakama hiyo ili kesi hiyo isikilizwe.
Baada ya kesi hiyo kutajwa, Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda aliiomba Mahakama iamuru watu wote watoke nje kwa sababu walikuwa wamefunga njia ili mtuhumiwa huyo aweze kupitishwa.
Hakimu Tarimo alikubaliana na ombi hilo na kuwaamuru askari kusafisha njia ili waweze kumpitisha msanii huyo kwa kile alichosema kuwa Lulu bado ni mtuhumiwa na anaweza kuumizwa.
“Askari safisheni njia ili mtuhumiwa aweze kupita kwa sababu yeye bado ni mtuhumiwa anaweza kuumizwa,"alisema Hakimu Tarimo.
Baada ya kutolewa kwa amri hiyo, askari walitimiza wajibu wao na muda mfupi njia ilipatikana na msanii huyo kutolewa mahakamani hapo.







Jopo la mawakili
Katika kesi hiyo, Lulu anatetewa na jopo hilo la mawakili akiwemo Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Joaquine De- Melo, Kenedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe. 
De- Melo  pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King.
Fungamtama ambaye ndiye kiongozi wa jopo la mawakili hao wanaomtetea Lulu, anakumbukwa kwa kuitetea kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, katika kesi dhidi ya Tanesco, ambayo alishinda na shirika hilo kuamriwa kuilipa kampuni hiyo  zaidi ya Sh94 bilioni kwa kuvunja mkataba.
Kibatala ambaye pia anamtetea kada wa Chadema, Fred Mpendazoe katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Segerea, pia ni Makamu wa Rais wa TLS, wakati Massawe anatoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Mawakili hao walijitokeza jana mbele ya Hakimu Tarimo tayari kumtetea Lulu na baada ya mawakili hao kujitambulisha, Wakili Kaganda alisema upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama iipangie tarehe nyingine.
Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mara ya kwanza Lulu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando  akikabiliwa na la shtaka hilo la mauaji. 
Wakili Kaganda alimsomea hati ya mashtaka alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu katika maeneo ya Sinza Vatican, Wilaya ya Kinondoni, mtuhumiwa alimuua  Kanumba. Kanumba alifariki dunia siku hiyo saa 9:00 usiku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya ugomvi baina yake na Lulu.














 Hisia zikampanda
Akaanza kulia