Monday, June 25, 2012

Lulu bado njia panda


                                              
SERIKALI imezidi kumweka katika wakati mgumu msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, anayekabiliwa na kesi ya tuhuma za mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Hatua hiyo inatokana na hatua ya upande wa mashitaka kukwamisha usikilizwaji wa kesi hiyo kwa kuwasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya kupitiwa upya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kukubali kufanya uchunguzi wa umri sahihi wa mshitakiwa huyo.
Umri wa Lulu umeibua utata wa kisheria baada ya upande wa utetezi kusema mteja wao ana miaka 17 na si 18 kama Hati ya Mashitaka inavyoonyesha, hivyo unadai kisheria anapaswa kushitakiwa katika Mahakama ya Watoto huku ule wa mashitaka ukipinga hoja hiyo.
Kufutia hali hiyo, mshitakiwa huyo aliyefika Mahakama Kuu jana Jumatatu kusikiliza shauri la utata huo wa umri wake, alishindwa kujizuia na kumwaga machozi baada ya mahakama hiyo kusimamisha shauri hilo.
                                          
Katika kesi yake ya msingi iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lulu anatuhumiwa kumuua Kanumba usiku wa Aprili 7, 2012 nyumbani kwa marehemu, Sinza, jijini Dar es Salaam.
Utata wa umri wa Lulu ulitarajiwa kusikilizwa hiyo jana Jumatatu na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Juni 11, 2012 Mahakama Kuu iliamua kufanya uchunguzi wa usahihi wa umri wa msanii huyo kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanaomtetea.
Lakini jana Jumatatu, Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, asema mahakamani hapo kuwa upande wa Jamhuri tayari imewasilisha maombi Mahakama ya Rufani kuomba uamuzi huo wa Mahakama Kuu uliotolewana Jaji Dk. Fauz Twaib ufanyiwe marejeo.
Jaji Dk. Twaib alikubaliana na maombi haya Jamhuri na kusimamishwa usikilizwaji huo hadi Julai 9, 2012, ikiwa Mahakama ya Rufani itakuwa imemaliza kushughulikia maombi hayo ya Serikali.
Kabla ya mahakama kufikia uamuzi huo, mawakili wa Lulu, Kennedy Fungamtama na Peter Kibatala, walipinga maombi ya serikali wakidai ni mbinu ya kuchelewesha shauri hilo.
                               
                                

Fungamtama alidai kuwa hadi wakati huo mahakama ilipoanza hapa kuwa na amri yoyote ya Mahakama ya Rufani ya kusimamishwa usikilizwaji wa suala la utata wa umri wa mteja wao.
“Hata kwenye maombi haya hakuna maombi yanayoelekeza kusimamishwa kwa usikilizwaji wa maombi haya,” alisema Fungamtama.
“Kinachofanywa hapa ni matumizi mabaya ya mamlaka ya Ofisi ya DDP (Mkurugenzi wa Mashtaka).”
Kwa upande wake, Wakili Kibatala, alidai kuwa maombi hayo ya Jamhuri kwa Mahakama ya Rufani hayaoneshi mazingira ya kusimamishwa kwa usikilizwaji wa maombi hayo na kwamba hiyo inabaki kwa mamlaka ya Mahakama Kuu yenyewe.
“Lakini kwa maslahi ya mshtakiwa ambaye anaendelea kuteseka mahabusu, tunaiomba mahakama hii iamuru usikilizwaji wa maombi haya (utata wa umri ) uendelee,” alisisitiza Kibatala.
Lakini akijibu hoja hizo, Wakili Kaganda, alidai ofisi ya DPP inatambua matakwa ya haki na kwamba inatenda kwa matakwa ya haki haitumii vibaya mamlaka yake.


Lulu anaendelea kushikiliwa rumande kwa vile aina ya shitaka linalomkabili halina dhamana kisheria.