Monday, April 9, 2012

Ratiba ya mazishi ya Steven Kanumba


Msanii wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012, atazikwa kesho Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Mazishi ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu, mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.

Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo katika tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye maisha ya milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye shughuli nzima.


Ratiba

Mwili wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga.

Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi, wakijipanga kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.

Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.

Saa 6:00 mchana, ratiba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya Kinondoni, msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea makaburini.

Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya marehemu.

Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili kumuaga kwa heshima.

Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe.


K.N.Y GABRIEL MTITU

MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

Hatima ya Lulu iko mikononi mwa DPP



Hatma ya msanii maarufu wa kike Elizabeth Michael maarufu kama ‘Lulu’ anayeshikiliwa polisi kufuatia kifo cha msanii Steven Kanumba iko mikononi mwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema suala la msanii huyo kusema ana kesi ya kujibu au la, liko mikononi mwa DDP ambaye ndiye atakayepitia jalada baada ya polisi kukamilisha upelelezi wao.

Kamanda Kenyela alisema Lulu kupelekwa mahakamani ni uamuzi wa DPP ambaye atatakiwa kulipitia faili lake na kujiridhisha kama ana kesi ya kujibu au la.

“Kumpeleka mahakamani ni mpaka DPP tutakapomwasilishia jalada la tuliyoyakusanya na ndiye atakayeamua kama kuna kesi ya kujibu au hakuna,”alisema Kamanda Kenyela.

Alisema hadi hivi sasa bado wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa daktari ambao hata hivyo hawatautoa kwa vyombo vya habari kwa kuwa huwa ni siri.

“Bado tunasubiria ripoti ya daktari na upelelezi unaendelea ila ripoti hiyo ni siri, si lazima apelekwe mahakamani kesho (leo) kwa kuwa bado upelelezi unaendelea,”alisema Kenyela.

Kanumba alifariki usiku wa kuamkia Jumamosi nyumbani kwake, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kenyela, zilieleza kuwa kifo cha msanii huyo kilitokana na ugomvi uliotokea kati yake na mpenzi wake ndani ya nyumba yake.


Taarifa za kifo cha Kanumba zilianza kusambaa kuanzia saa 10.00 alfajiri na kuenea kwa kasi ambapo hadi kufikia saa moja asubuhi, mamia ya watu walikuwa wamejazana nyumbani kwa Kanumba kutaka kuthibitisha habari hizo.

Kadri muda ulivyozidi kusogea ndivyo idadi ya watu ilizidi kuongezeka nyumbani kwa msanii huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kutoka na filamu zake kuuzwa na kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa watu waliomiminika kwa haraka nyumbani kwa Kanumba ni wasanii wa fani mbalimbali nchini, wanasiasa na viongozi mbalimbali wa Serikali


Chanzo cha kifo chake

Kwa mujibu wa maelezo ya mdogo wake aitwaye Seth ambaye alikuwapo eneo la tukio, alisema kaka yake alishinda nyumbani na baada ya kula chakula cha jioni, alimwambia wajiandae kutoka.

Hapa mwili wake ukiwekwa vizuri kabla haujaingizwa monchwari ya Muhimbili


Seth alisema kuwa wakati Kanumba akiwa tayari amejiandaa, walisikia mlio wa gari likifunga breki nje ya nyumba.

Alisema gari hilo lilikuwa limemleta mpenzi wa kaka yake msanii wa filamu, Lulu ambaye aliingia ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwa Kanumba.

Baada ya kuingia ndani, muda mfupi alisikia sauti zilizoashiria kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya wapenzi hao.

“Ghafla ulizuka mzozo ndani na dakika chache baadaye, Lulu alitoka na kuja kuniambia kuwa Kanumba amedondoka baada ya kujigonga ukutani na kwamba yupo taabani hajitambui,” alisema Seth.

Alisema alipoingia chumbani, alimkuta kaka yake akiwa katika hali mbaya hivyo akaamua kumpigia simu daktari wake, ambaye alipofika na kuwashauri wampeleke haraka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu.

Seth alisema kabla ya kufika Muhimbili walipitia Kituo cha Polisi cha Oysterbay kupatiwa Fomu ya matibabu (PF3).

Hata hivyo, baada ya polisi kupata maelezo ya awali ya ugomvi huo, walimshikilia Lulu kituoni hapo na kumwacha Seth akimpeleka Kanumba hospitali.

Alisema walipofikia Hospitali ya Muhimbili, madakati waligundua kuwa tayari Kanumba alishaaga dunia.

Awali Kamanda Kenyela akithibitisha kutokea kwa tukio hilo alisema Kanumba alikufariki kutokana na ugomvi uliotokea kati yake na rafiki yake wa kike Lulu.