Thursday, January 19, 2012

Tanzania yawakilisha dai la nyongeza eneo la bahari


Jahhuri ya Muungano wa Tanzania, imewasilisha katika Umoja wa Mataifa, Andiko la kudai eneo la nyongeza lenye ukubwa wa maili 16,000 nje ya eneo la sasa la maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Anna Tibaijuka (Mb) ndiye aliyewasilisha Andiko hilo, kwa niaba ya serikali, katika hafla fupi na ya kihistoria iliyofanyika siku ya Jumatano katika Ofisi za Idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari.

Andiko hilo lilipokelewa na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Sergei Tarassenko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye aliipongeza Tanzania kwa hatua hiyo muhimu na kuahidi kwamba Idara yake kupitia, Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mipaka ya bahari italifanyia kazi andiko hili.

Mkurugenzi huyo alielezea Tanzania, kama moja kati ya nchi inayoheshimu na yenye historia nzuri katika Umoja wa Mataifa.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha Andiko hilo, Waziri Anna Tibaijuka, alisema kwa kuwasilisha Andiko hilo, Tanzania si tu kwamba imefanya kazi ya uhakika ya maandalizi na hatimaye uwasilishaji lakini ni hatua kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi , Anna Tibaijuka akimkabidhi Mkurugenzi wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari, Sergei Tarassenko kwa Niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, andiko la kudai nyongeza ya maili 61,000 nje ya eneo la maili 200 la Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari , jijini New York, Marekani.

Akabanisha kwamba mchakato wa maandalizi ya Andiko hilo ambao umechukua miaka mitano, umewashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwamo wa ndani na nje , ikiwa ni pamoja na kuzihusisha nchi ambazo zinapakana kibahari na Tanzania.

Akizungumza manufaa ya kudai nyongeza ya eneo hilo, Waziri Tibaijuka alisema. “ Tanzania itanufaika kwa kuongeza ukubwa wa eneo la mipaka ya nchi lakini la msingi zaidi ni unufaikaji wa rasilimali zikiwamo za mafuta na gesi na madini ambazo zitakuwamo katika eneo hilo jipya, rasilimali ambazo kwa sasa zinaelekea kutoweka katika eneo la maili 200”.

Eneo ambalo Tanzania inadai liongezwe la maili 61, 000 ukubwa wake ni sawa na eneo la mikoa mitatu ikiunganishwa kwa pamoja.

Aidha kuongezwa kwa eneo hilo kutaisaidia pia serikali katika masuala ya ulinzi na usalama hasa katika kipindi hiki ambacho vitendo vya kiharamia wa baharini vikiwa vimeongeza katika eneo la bahari ya Hindi.