Tuesday, August 23, 2011


Mtoto wa Gaddafi asema hajakamatwa, aapa atapambana hadi kieleweke!

Mtoto wa kiume wa kiongozi wa Libya, kanali Muammar Gaddafi, Seif Al Islam, amejitokeza hadharani katika hoteli moja mjini Tripoli na kukanusha madai kuwa amekamatwa.

Habari zinasema kuwa, Al Islam aliibuka katika hoteli hiyo jana asubuhi ambayo waandishi wa habari wa kigeni wamekuwa wakiishi mjini hapo na kuwaeleza waandishi hao, wananchi wa Libya na dunia kwa ujumla yupo salama na ataendeleza mapambano mpaka kieleweke.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), Luis Moreno-Ocampo, na waasi wa Libya walisema juzi kuwa mtoto huyo wa Gaddafi wamemkamata.

Seif amesema utawala wa Gaddafi bado unaudhibiti mji mkuu Tripoli na kwamba baba yake yuko salama na katika hali nzuri mjini humo.

Al-islam ambaye alionekana kuwa mchangamfu na mwenye shauku kuu aliongeza waasi wameingia kwenye ''mtego'' mjini Tripoli na kwamba wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi walikuwa ''wamevunja uti wa mgogo wa waasi hao''.


"Niko hapa kuuondoa uwongo uliotangazwa" alisema Saif Al-Islam mbele ya kikundi cha waandishi wa habari mjini Tripoli katika kitongoji cha Bab al- Azizyah ambapo ni makao ya baba yake.

“Mji mkuu Tripoli ungali uko chini ya udhibiti wa utawala wa baba yangu na kwamba Magharibi ilitumia teknolojia yake kuvuruga mifumo ya mawasiliano na kutuma jumbe kwa wananchi kwamba utawala wa Gaddafi umeanguka,” alisema Al- Islam.


Mtoto wa kiume wa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, Seif Al Islam akiwa na wafuasi wake pamoja na waandishi wa habari, akionyesha alama ya ushindi ya V baada ya kuibuka katika hoteli moja mjini Tripoli jana asubuhi. Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), Luis Moreno-Ocampo, na waasi wa Libya walisema juzi kuwa mtoto huyo wa Gaddafi wamemkamata.