Friday, June 15, 2012

Binti aliyehukumiwa kupigwa mawe hadi kufa kwa uzinzi


BLANKETI la uchungu na kukata tamaa limeufumbata uso wa Intisar Abdallah.
 Ameketi katika chumba cha jela chenye joto kali, miguu yake ikiwa imefungwa kwa chuma,huku akiendelea kukinyonyesha kichanga chake chenye umri wa miezi mitano.  
Intisar, ameathirika kisaikolojia kwa sababu anajua fika kuwa,  siku si nyingi ataingizwa kaburini.
 Machungu ya Intisar, (20) hayakomei katika hofu ya kifo pekee, bali hata namna na sababu ya kifo hicho. 
Intisar, atachimbiwa ardhini na kubakizwa kichwa tu. Kisha atapigwa mawe hadi kufa ikiwa ni adhabu yake baada ya kuzini na kubeba mimba.
Aprili 22 mwaka huu ndiyo siku ambayo Hakimu, Sami Ibrahimu Shabo wa mahakama ya makosa ya jinai ya Ombada iliyoko katika mji mkuu wa Khartoum, Sudan alimhukumu Intisar adhabu kifo. 
Kilimchofanya mpaka binti huyu akapewa adhabu hii ni kwa sababu alifanya tendo la ngono nje ya ndoa.  Instisar ambaye ni mama wa  watoto watatu alionekana mwenye kosa la jinai kwa nchi zenye misingi imara ya dini ya Kiislam. 
Hukumu ya Intisar ilitolewa kwa sababu ya kifungu namba 146 cha  mwaka 1991 cha makosa ya jinai nchini Sudan. 
 Awali, Intisar alishtakiwa kwa uzinzi, lakini akaachiwa huru. Baadaye, kaka yake alimpiga kikatili na kumshurutisha akimtaka akiri makosa yake. 
Hapana shaka kipigo kile ndicho kilichomfaya Intisar akubali kosa hilo.
 Hata hivyo, mwanamume waliyezini naye aliachiwa huru kwa sababu tu, alikana kosa hilo. 
Wakati huo, kesi iliendeshwa kwa lugha ya kiarabu,ambayo Intisar haifahamu. Hukumu ikatolewa wakati Intisar akiwa hana wakili wa kumtetea katika hilo. 
Mawakili waliruhusiwa kumwona na kumuhoji mara baada ya hukumu kutolewa. 
Hukumu ya kuua haikubaliani na sheria za kimataifa, kwani inaenda kinyume na haki za binadamu.
 Pamoja na hilo, lakini kibaya zaidi ni kumhukumu kifo mama mwenye mtoto mchanga ni kitendo kinachopingwa na sheria za kimataifa. 


Hukumu hiyo ilipingwa vikali na mtandao wa kikundi cha Mapambano cha Wanawake waishio katika Pembe ya Dunia (SIHA network).
 Siha kilitoa tamko kali kuhusu kesi hiyo na kusema imejaa upungufu, unyanyasaji na uvunjwaji wa haki kwa kiasi kikubwa. 
 “Ni ajabu kwamba mwanaume ambaye anatuhumiwa kuzini naye ameachiwa huru. Jambo ambalo linaweka wazi ukatili wa kijinsia na usimamizi mbaya wa migogoro ya kifamilia,” ulisema mtandao huo.
Sudan ya Kaskazini ni miongoni mwa nchi saba duniani zinazotoa adhabu ya kifo kwa kupigwa mawe.
 Rais Omar Al Bashir ndiye aliyetambulisha chembechembe za Sharia Law, mwaka 1989 baada ya kuingia madarakani. 
Lakini kinachowachanganya wengi ni kuwa, adhabu hizo huwapata zaidi  wanawake kuliko wanaume. 
Wananchi nchini humo  wamekuwa wakifungwa vifungo vya muda mrefu na kupewa adhabu kali kwa makosa kama ya kuuza bidhaa barabarani, kuvaa mavazi yanayokwenda kinyume na taratibu za kidini pamoja uzururaji.
Watu wamewahi kupigwa mawe hadi kufa baada ya kufanya makosa ya uzinzi.
Julai 13, 1997 Changiz Rahimi alihukumiwa kupigwa mawe hadi kufa, huku akilipa faini kwa kuzini. 
Julai 14, 1995 wanawake wawili Sada Abdali, 30, na  Zeinab Heidary, 38 walihukumiwa kupigwa mawe katika Jiji la Ilam, Gharb.
 Lakini pia wapo wanawake waliohukumiwa kupigwa mawe, lakini wakaponea chupuchupu.
 Mwaka 2002, Amina Lawal,  Nigeria, alihukumiwa kupigwa mawe, lakini aliachiwa huru baada ya kukata rufaa.
Sakineh Mohammadi Ashtian alihukumiwa nchini Iran mwaka 2007, lakini hukumu yake ikapingwa na ipo katika mjadala.
Mwingine ni Safiya Husseini wa Nigeria pia, yeye aliachiwa huru baada ya kukata rufaa.

Ateseka na saratani ya mifupa kwa miaka kumi


WAKATI saratani ya matiti ikiwa tishio kwa wanawake wengi duniani,  mwanamke mmoja nchini China anateseka na uvimbe mkubwa usoni mwake uliosababishwa na kuugua saratani ambao amedumu nao kwa miaka 10 sasa.

                                 

Li Hongfang (40), ameshindwa kupata matibabu ya kuondoa uvimbe huo unaomsumbua kutokana na kutomudu gharama za matibabu. Ugonjwa huo ambao umeelezwa na madaktari kuwa ni aina ya saratani ya mifupa, ni ugonjwa unaosababisha tishu kukua.
"Mimi si mtu wa kutisha, bali ni mgonjwa tu, lakini watu wengi wamekuwa wakisema kuwa ninatisha na wengine kunikimbia," anasema.
Tatizo lake lilianza mwaka 2001, wakati huo aliona kivimbe kidogo pembeni mwa kichwa chake, lakini anasema hakukitilia maanani kwani kilikuwa hakina maumivu yoyote.

                             

Baada ya afya yake kuanza kubadilika miaka minne baadaye, madaktari walisema kuwa ana jumla ya uvimbe mdogo mdogo saba unaozidi kukua katika uso wake.
Lakini hakuweza kuwa na gharama ya kiasi cha Pauni 60,000 (zaidi ya Sh150 milioni) ili aweze kupatiwa matibabu.
"Najua kwamba watu wengi sasa wananiangalia mimi kama mtu fulani wa kutisha, lakini bado nabaki kuwa mwanamke wa kawaida na mama kwa upande mwingine," anasema.
Kwa mujibu wa madaktari, aina hiyo ya saratani huanza kukua katika fuvu la kichwa na chini ya mgongo. Ingawaje hakuna takwimu sahihi, lakini inaelezwa kuwa ugonjwa huu huathiri mtu mmoja kati ya watu milioni moja nchini Marekani.

Akilia kwa uchungu baada ya kueleza yanayomsibu, kama binadamu wa kawaida ni lazima ujisikie vibaya kwa jinsi watu wengine wanavyomchukulia
                                        
Hongfang ameteseka na ugonjwa huo kwa kipindi chote hicho kutokana na mfumo duni wa matibabu na kuchelewa kupata huduma.
 Wakati alipoanza kupatwa na ugonjwa huo, alikuwa akiishi na mumewe na watoto wawili katika kijiji cha Tianchao, katika Kata ya Qianxian huko Magharibi mwa China.
"Hatukuwa na fedha nyingi, lakini tulikuwa na furaha sana na tulipendana pamoja na watoto wetu wawili wa kiume. Ninaweza sema maisha yalikuwa mazuri sana, lakini kadri uvimbe ulivyozidi, aliniacha na kwenda mbali.
"Sikuwahi kufikiria kitu chochote nilipoanza kuuona uvimbe ule katika kichwa changu, nilidhani pengine ni aina tu ya wadudu walikuwa wamening'ata,” anasema.
Anaongeza: "Sikuweza kufanya lolote nilikuwa nakuna tu na kuacha lakini ilianza kukua kwa kasi.”
Nchini China, huduma za afya zinasua sua sana katika miaka ya hivi karibuni, lakini katika miaka ya nyuma kulikuwa na ada maalumu iliyotolewa katika vituo vya afya.
Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo, hawana uwezo wa kupata huduma hiyo.


Akionyesha picha za wanawe

Hivi sasa China imeanza kujadili mpango wenye lengo la kutoa bima za afya kwa watu wote wanaofikia1.3 bilioni na kuazimia kuwa hadi kufikia mwaka 2020, mpango huo uwe umekamilika.