Monday, April 30, 2012

Kanumba alijijua anakufa


MTAALAM wa mambo ya mwanga katika utengenezaji wa filamu Swahiliwood, Steven Shoo ëSammy Shooí, amedai kuwa marehemu Steven Kanumba alijua kuhusu kifo chake.
Hilo alilijua siku ambayo alikuwa akirekodi filamu yake ya mwisho ambayo alikuwa akirekodi filamu ya Power In Love kutokana na maneno ambayo awali walijua kama utani.
"Tukiwa tunapiga picha hizo za filamu, siku hiyo alikuwa akituhimiza tumpige picha kwa kutumia simu zetu. Nakumbuka aliniambia 'Sam nipige picha bwana, naweza kufa hapa ukakosa picha yangu ukaanza kuhangaika kuitafuta picha yangu katika Internet wakati mpo na mimi hapa... kila mtu anipige piga bwana', alisisitiza lakini katika hali ya utani," anasema Sam.
Sammy, ambaye amekuwepo na marehemu kwa muda mrefu pia na kufanya kazi na mtayarishaji mwingine Ray, anasema pamoja na kutambua kwamba Kanumba alikuwa mtu mwenye utani, lakini katika kufanya naye kazi hata siku moja hakuwahi kumsisitiza ampige picha ya ukumbusho.
Anasema, mara nyingi wanapokuwa kwenye kazi, Seth ambaye ni mdogo wake Kanumba, hupiga picha kwa ajili ya matumizi ya mtandao wake, kutokana na kusisitizwa na marehemu.


"Yaani simu yangu imejaa picha za 'location' tu nikiwa na marehemu pamoja na watendaji wengi ambao tulikuwa nao katika filamu ya mwisho aliyoigiza, siamini kama kweli bosi wetu kafariki, nahisi kama kasafiri tu kama ambavyo hufanya siku zote," anasema Sammy.