Sunday, April 15, 2012
Weweee achia mchuma huooo!
Kanumba; Nyota iliyozimika ghafla, ataishi kwa muda mrefu
Mwandishi Wetu
NI msiba ambao umeingia kwenye historia na utaendelea kubaki katika kumbukumbu za wengi na hasa wapenzi wa filamu nchini.
Kifo cha Steven Kanumba ‘The Great’ kimeandika historia kutokana na kugusa watu wengi na wa kada zote, kuanzia Rais Jakaya Kikwete hadi wananchi walalahoi wapenzi wa filamu.
Jina la Kanumba litabaki katika kumbukumbu za watu waliofanikisha kwa kiasi kikubwa kukuza fani ya maigizo na hatimaye filamu hapa nchini, pia jina lake litabaki kukumbukwa na wapenzi wa filamu katika Ukanda wa Afrika Mashariki, hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda ambako alijizolea umaarufu mkubwa.
Makaburi mengi yaliharibiwa na watu kwa kukanyagwa wakati wa mazishi ya marehemu Kanumba
Kanumba anakumbukwa kwa hatua kubwa aliyokuwa amefikia, hatua ambayo hakuna msanii mwingine wa filamu nchini aliyekuwa amefikia, aliweza kijitanua hadi kufanikiwa kufanya kazi na wasanii wakubwa wa Nigeria, nchi inayoongoza kwa kufanya vizuri katika filamu.
Licha ya kuanzisha tasnia hiyo pia amekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha filamu za Tanzania zinakuwa na kiwango cha kimataifa kiasi cha kuinua soko la filamu hizo na kuitanganaza nchi yetu.
Filamu za Dar to Lagos, Devil’s Kingdom, She is my sister, Cross my sin na Hero of the Church, ni kazi zilizofungua milango ya Kanumba nje ya nchi; kazi zote hizo amezifanya kwa ushirikiano na wasanii kutoka Nigeria.
Mpaka anakumbwa na umauti Kanumba ameshacheza takribani filamu 40 ya kwanza ikiwa ni Johari aliyoifanya akiwa bado muigizaji wa kundi la Kaole na filamu ya mwisho inaitwa Ndoa Yangu ambayo bado ilikuwa ikifanyiwa matangazo kabla ya kuingia sokoni.
Kanumba aliweza kujizoelea umaarufu kwa watu wa rika zote kutokana na filamu zake kulenga kukonga nyoyo za wapenzi wa filamu wa makundi yote kwani aliweza kugusa kila nyanja ya maisha.
Mafanikio yake ni mfano wa kuigwa kwa vijana wote kwani amepitia mengi ambayo yangeweza kumkatisha tamaa, historia yake ilianzia nyumbani kwao Shinyanga ambapo Kanumba aliwahi kukaririwa akisema hakupata malezi stahiki kutoka kwa baba yake.
Maisha ya kutopata mapenzi ya baba ndiyo yaliyokuwa chachu kwa Kanumba kwani alipoingia kwenye kundi la Kaole, uwezo wake ulianza kudhihirika.
Hakuishia hapo, alidhubutu kuingia kwenye fani ya filamu, kwa miaka kadhaa akiwa chini ya kampuni ya utengenezaji filamu ya Game First Quality, lakini hatua kwa hatua na kwa kutumia mafanikio yake, Kanumba aliweza kuwa na kampuni yake binafsi ya utengenezaji filamu ya ‘The Great Film.’
Ni kwa mafanikio na heshima aliyojijengea, Kanumba aliweza kuiwakilisha nchi akiwa Balozi wa Shirika la Kimataifa la Chakula Duniani la Oxfam hapa nchini, Kanumba pia aliweza kutumiwa na kampuni mbalimbali kwa ajili ya matangazo na pia kama balozi wao, hadi anafariki alikuwa pia balozi wa kampuni ya Startimes.
Aidha Kanumba amekuwa mcheza filamu pekee toka Tanzania kupata mualiko wa kutembelea jumba la Big Brother Africa pamoja na kualikwa katika onyesho la utoaji tuzo za filamu nchini Ghana maarufu kama Film of Africa.
Kanumba alizaliwa mwaka 1984 mkoani Shinyanga ambapo ndiko alikojipatia elimu yake ya msingi na sekondari kabla ya kuhamia jijiji Dar es Salaam kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Jitegemee na baadaye kujiingiza moja kwa moja kwenye sanaa.
Aprili 7 mwaka huu alifariki akiwa nyumbani kwake kufuatia kile kinachodaiwa ugomvi kati yake na anayedaiwa kuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael, ‘Lulu’.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa madaktari, Kanumba alifariki baada ya ubongo wake kutikiswa, hivyo kushindwa kupumua na hatimaye kufariki muda mfupi baadaye.
Amefariki akiwa na ndoto nyingi, kubwa ni kuwa mbunge ambapo aliwahi kukaririwa akisema angegombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.