Thursday, November 3, 2011

Hapa ni Dar, hii ni shule

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akiangalia mmoja ya darasa lililojengwa mwaka 1978 katika Shule ya Msingi Ushindi iliyopo Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam ambalo halitumiki kufuatia kuchakaa kwake na shule hiyo kushindwa kulikarabati.

Viungo vya binadamu vyampeleka jela miaka 10

Mkazi wa Kijiji cha Wami Dakawa, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Fatma Kachingo, akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kukutwa na fuvu la binadamu eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Morogoro muda mfupi kabla ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela, kufuatia kukiri kosa.


Mwanamke aliyekutwa na viungo vya binadamu, amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela baada ya kukiri kosa hilo huku mume wake akirudishwa mahabusu baada ya kukana shtaka.

Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, walipofikishwa washtakiwa hao ambao ni mume na mke; Fatuma Kachingo (42) na Mogela Victory (38), wakazi wa Kijiji cha Wami Dakawa, Wilaya ya Mvomero.

Hakimu Nuru Nassari alisema kitendo cha mshtakiwa kukiri kosa kinaifanya mahakama kuamini kuwa, alifanya kosa hilo kwa makusudi huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria na kwamba, adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wengine wanaomiliki viungo vya binadamu kwa imani za ushirikina.

Kabla ya kutiwa hatiani, mshtakiwa huyo alijitetea ili mahakama impe adhabu ya huruma kwa madai kuwa, ana familia inayomtegemea wakiwamo wajukuu na umri wake ni mkubwa.

Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali utetezi huo baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Lameck Wabi, kuomba kutoa adhabu kali kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ukataji viungo unaofanywa kwa imani za ushirikina.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja Oktoba 29, mwaka huu saa 2:00 asubuhi, walikutwa na fuvu na ngozi ya binadamu ambavyo vilihifadhiwa chumba kimojawapo kwenye nyumba wanayoishi.

Vitu vingine ni magamba ya konokono ambavyo vinadhaniwa vinatumika katika shughuli za ushirikina.


Htimaye Kabwe afanyiwa operesheni

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akila matunda baada ya kufanyiwa operesheni katika Hospitali ya Apollo nchini India, jana. Zitto amefanyiwa operesheni puani kutona na kusumbuliwa na maradhi ya kipanda uso.

Zitto ni kiongozi wa nne kupelekwa India kwa matibabu katika kipindi kisichozidi miezi mitatu, akitanguliwa na mawaziri wawili na naibu waziri mmoja. Hao ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Aligundulika kuwa na maradhi hayo ya kipanda uso ambayo kitaalamu yanajulikana kama sinusitis tayari yakiwa sugu. Alisema Daktari Bingwa wa magonjwa hayo, Dk Kimaryo wa MNH alimweleza kwa kirefu juu ya tatizo hilo na kumshauri kuwa suluhisho lake upasuaji, huduma ambayo ilikuwa haipatikani katika hospitali hiyo ya Taifa.