Kobe Bean Bryant ni nyota wa mpira wa kikapu, ambaye anachezea Los Angeles inayoshiriki Ligi ya Marekani (NBA).
Bryant, ambaye amezaliwa Agosti 23, 1978), ndio mfungaji mahiri wa timu hiyo.
Anajiita mwenyewe jina utani la "Black Mamba", akijifananisha na nyoka huyo, ambaye anapatikana barani Afrika.
Nyoka huyo yupo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan, Ethiopia, Eritrea, Somalia, Kenya, Uganda, Tanzania, Msumbiji, Swaziland, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Botswana, Afrika Kusini na Namibia.
Kobe anajifananisha na nyoka huyo kwa kuwa naye ana shabaha kubwa ya kufunga na kasi.
Nyoka aina ya Black Mamba husifika kwa kuteleza kwa kasi na kushambulia bila ya kukosea.
Black Mamba anaaminika kuwa ndio nyoka mwenye kasi zaidi duniani kutokana na uwezo wa kukimbia kilomita 20 kwa saa.
Ukiangalia na rekodi ya Kobe utagundua hajafanya makosa kujilinganisha na nyoka huyo kwani anashikilia rekodi ya kuifungia pointi nyingi zaidi Lakers.
Pia ni mtu wa pili kufunga pointi nyingi zaidi katika mchezo mmoja wa NBA. Amewahi kufunga pointi 81. Wilt Chamberlain ndio anashikilia rekodi kwa kufunga pointi 100 katika mechi moja, aliyoweka mwaka 1962.
Kobe pia ni miongoni mwa watu watatu waliofunga pointi nyingi zaidi katika historia ya NBA.
Ana utajiri wa kiasi cha Dola 200 milioni (Sh. 18 bilioni za Kenya) ukitokana na mshahara wake na matangazo mbalimbali ya biashara.
Mshahara wake wa mwaka katika timu yake ya Lakers ni kiasi cha Dola 24 milioni (Sh. 2.2 bilioni za Kenya)
Ana mkataba wa matangazo na kampuni ya kutengeza vifaa vya michezo ya Nike. Pia ana mikataba na makampuni ya Coca-Cola, McDonald, NBA Infusion Ball, Upper Deck, Ferrero SpA na Russell Corporation.
Bryant pia ana mkataba wa matangazo na Shirika la Ndege la Uturuki.
Pia anafanya matangazo ya magari ya Mercedez Benz nchini China.
Kobe pia anafanya muziki, na hivi karibuni alishirikiana na mwanamuziki wa Taiwan, Jay Chou kutengeneza wimbo wa "The Heaven and Earth Challenge".
Fedha zitakazotokana na wimbo huo zitasambazwa duniani kote kwa ajili ya kutengeneza viwanja vya mpira wa kikapu.
Bryant na mkewe Vanessa wana nyumba ya thamani ya Dola 4 milioni (Sh. 375 milioni za Kenya) huko Newport Beach, Marekani.
Pia alinunua nyumba nyingine ya thamani ya Dola 13.5 milioni (Sh. 1.2 bilioni za Kenya)iliyoko Newport pia, katika Jimbo la California. Nyumba hiyo ipo katika ufukwe wa bahari kwenye eneo hilo.
Nyumba hiyo ina vyumba sita vya kulala, mabafu 11 ya kuogea, bwawa la kuogelea na gereji yenye uwezo wa kuingiza magari matano.
Bryant pia ana nyumba nyingine katika jiji la Los Angeles.
Pia ana magari aina ya Range Rover, Ferrari F430, 360 Modena, 612 Scaglietti, Bentley Continental GT, Azure Mulliner, Cadillac Escalade na 1963 Chevrolet Impala.
Kobe pia anamiliki ndege yake, ambayo hutembea nayo sehemu mbalimbali duniani.
Alianzia mpira wa kikapu katika shule ya Lower Merion kabla ya kusajiliwa na Charlotte Hornets mwaka 1996.
Alikaa kwa muda mfupi kabla ya kuchukuliwa na Los Angeles Lakers, ambako yuko hadi sasa.
Kobe amepata tuzo nyingi za NBA, ikiwamo mchezaji bora mwaka 2003, kuchezea timu ya nyota wa michuano hiyo mara 13 na medali ya dhahabu ya Olimpiki mwaka 2008.
Ni mtoto wa kocha wa zamani wa Los Angeles Sparks, Joe "Jellybean" Bryant na mama yake anaitwa Pamela Cox Bryant.
Yeye na mkewe Vanessa wana watoto wawili wa kike.