Thursday, January 5, 2012

Urefu unamnyima gari bomba



Peter Crouch ni mshambuliaji wa Stoke City na kikosi cha England.
Akiwa na urefu wa futi 6 na inchi 7 anaaminika kuwa mchezaji mrefu zaidi kwenye Ligi Kuu England.
Crouch, ambaye alizaliwa Januari 30, 1981, alianzia soka yake katika timu ya watoto wa Tottenham Hotspur.
Hakupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu ile na mwaka 2000 aliondoka na kujiunga na timu nyingine za Ligi Kuu.

Alichezea timu za Portsmouth, Aston Villa, Southampton na Liverpool kabla ya kurejea Tottenham mwaka 2009.
Ana utajiri wa kiasi cha pauni 15 milioni (Sh. 36.4 bilioni) na jumba la thamani la pauni 5 milioni (Sh 12.1 bilioni) katika eneo la Cheshire jijini Manchester.
Alinunua jumba hilo kutoka kwa nyota wa Kriketi wa England, Andrew ìFreddieî Flintoff.
Nyumba huyo ina bwawa kali la kuogelea, vyumba sita vya kulala na gym.
Crouch amekiri kuwa anapenda sana magari lakini amekuwa na wakati mgumu wa kupata gari la saizi yake.
Alidai kuwa hali hiyo inachangiwa na urefu wake wa futi 6 na inchi 7.
Alisema kutokana na hali hiyo, anakosa uhondo wa kuendesha magari makali na kufanya awe na magari ya kawaida tu.
Pamoja na changamoto hiyo, anamiliki magari aina ya Hyundai Santa Fe SUV, Aston Martin, Range Rover na Bentley.



Crouch alizaliwa katika eneo la Macclesfield, Cheshire lakini familia yake ilihamia Singapore alipokuwa na umri wa mwaka mmoja.
Walikaa huko kwa miaka mitatu na kurejea katika eneo la Ealing, London.
Akiwa na umri wa miaka 10, alipata nafasi ya kuwa muokota mipira katika uwanja wa Stamford Bridge.
Kutokana na urefu wake, Crouch ana majina mengi ya utani kama Crouchy, RoboCrouch, Crouchinho na Mr. Roboto.


Katika enzi yake akichezea Liverpool, mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakimuimba "Crouch ni mrefu, anavaa jezi nyekundu na miguu yake haitoshi kitandani."
Jina la 'Mr Roboto' alipachikwa na mashabiki baada ya kuifungia England kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Hungary, Mei 30, 2006.
Alicheza dansi kwa staili ya Robot na akarudia tena kwenye mechi dhidi ya Jamaica, Juni 3, 2006.
Hata hivyo, alisitisha staili hiyo na kusema angeicheza kama England ingetwaa Kombe la Dunia mwaka 2006.
Crouch ana mke anayeitwa Abigail Clancy na wana mtoto anayeitwa Sofia.

Kimenuka CUF, Hamad, wenzake watimuliwa


Hatimaye Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake watatu wamefukuzwa uanachama wa CUF kuanzia jana. Hatua hiyo ilichukuliwa na zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho katika kikao chake kilichofanyika hapa.

Uamuzi huo umekata mzizi wa fitina wa hatma ya Hamad na washirika wake hao kisiasa ndani ya chama hicho, baada ya kuibuka mvutano wa muda mrefu kati yake na uongozi wa juu.

Mvutano huo uliochomoza zaidi baada ya Hamad kutangaza kuwania nafasi ya Katibu Mkuu inayoshikiliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa na Hamad ambaye ameiita kuwa ni ya kihuni kwani imekiuka amri ya Mahakama iliyotangaza kusitishwa kwa kikao kilichochukua uamuzi huo.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alithibitisha kuvuliwa uanachama kwa Hamad na kuwataja wengine walioondolewa pia kuwa ni Mjumbe wa Baraza Kuu (Tanga), Doyo Hassan Doyo, Mjumbe wa Baraza Kuu (Pemba), Shoka Khamis Juma, Mjumbe wa Baraza Kuu Unguja, Juma Saanane na Mjumbe wa Baraza Kuu (Mbeya), Yassin Mrotwa.

“Kwa mujibu wa katiba ya chama, wasioridhika na uamuzi huo wanaweza kukata rufaa kwenye mkutano mkuu wa taifa,” alisema.


Wanandoa waadhimisha miaka 75 ya ndoa


Kama kuna yeyote anayefahamu siri ya kudumu kwa ndoa, basi ni Robert and Susan Erskine.

Walizama katika penzi mara tu walipoonana. Wakati huo Susana akiwa na umri wa miaka 20 na mume wake Robert akiwa na umri wa miaka 21.

Penzi hilo lilichanua na kudumu mpaka leo hii katika sikukuu ya kusherehekea mwaka mpya wa 2012 wameadhimisha miaka 75 ya ndoa yao.

Robert, 100 na Susan 99 walifanya sherehe hiyo iliyojumuisha vizazi vyao vitatu. Yaani watoto, wajukuu na vitukuu vyao.

Wapenzi hawa, walifunga ndoa baada ya miaka mitano ya uchumba, mwaka 1937 na tangu vita vya ya pili dunia, hawakuwahi kutengana kwa zaidi ya siku moja.

Susan anasema walifunga ndoa yao siku ya mwaka mpya kwa sababu hapo zamani, ukikosa kuhudhuria kazi- hulipwi, na sisi tulitaka kila mtu ahudhurie ndoa yetu. Ndiyo maana tukafunga ndoa yetu siku ya mapumziko.

“Nampenda Robert sana sasa hivi kama ambayo nilimpenda siku ya kwanza nilipomuona kwa macho yangu. tulipokutana, tu tulijua kuwa tunapendana. Bado tunapigana busu na kushikana mikono,” anasema Susan.


Walikutana wapi?

Walikutana kijijini kwao Bo’ ness in Stirlingshire, katika kwaya ya kanisani.

Susan anasema mama yangu alimkubali Robert kwa sababu alimuona kuwa ni kijana mzuri ambaye hatumii pombe wala kuvuta sigara.

“Na mpaka leo hagusi hata tone la pombe,” anasema Susan.

Baada ya Robert kurudi kutoka katika vita kuu ya pili ya dunia, walihamia Edingburgh ambako alipata kazi nyingine na Susan.

Wanandoa hawa walirudi nchini Bo’ness miaka 25, baadaye na ndipo waliposherehekea maadhimisho yao ya ndoa, pamoja na watoto wao.

Susan na Robert wana watoto watatu, William, 68, Margaret, 64 na Bobby 54. Wana wajukuu sita na vitukuu sita.

Susan anazungumzia namna ambavyo ndoa nyingi katika ulimwengu wa sasa zinavyovunjika na kusema, mapenzi mengi siku hizi si ya kweli.

Anaongeza na kusema unapoingia katika ndoa unatakiwa ujipange.

“Uwe kama mwanamke halisi, usijifanye mwanaume, kwa mfano mimi nafanya kazi zote za ndani, wakati Robert anafanya kazi ndogondogo kama kutupa taka na kupanda maua,” anasema Susan.

Anaendelea na kusema kuwa pamoja na kupendana sana, lakini wana tabia tofauti. Wakati Susan ni mzingumzaji na anayependa kucheka, Robert ni mkimya.


“Napenda utani, yeye ni mkimya, anapenda kuniambia kuwa, ninaongea sana kwa hiyo hapati nafasi ya kuongeza neno,” anasema Susan.

Anasema ili ndoa zidumu ni vyema kila mmoja akatambua udhaifu wa mwenzake na ahakikishe anaulewa na kuukabili.

Wakati Susan na Robert wanasherehekea miaka 75 ya ndoa, zipo ndoa ambazo zimedumu kwa saa chache tu. Na watu hao ni mwanamuziki Britney Spear na Jason Alexander ambao ndoa yao ilidumu kwa saa 55 tu.