Mvua kubwa ya upepo iliyonyesha usiku wa kuamkia jana imesababisha mafuriko makubwa, maporomoko ya mawe kwenye Mto Kirurumo uliopo mpakani mwa Wilaya mbili za Karatu na Monduli, mkoani Arusha.
Kutokana na mvua hizo mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya kuzolewa na maji kilomita nne ambako maiti yake iliokotwa.
Mbali na kifo na majeruhi huyo, mvua hizo pia zimewaacha mamia ya wakazi wa maeneo hayo bila makazi kutokana na nyumba kadhaa kusombwa na mafuriko hayo.
Watalii, wagonjwa wakwama
Idadi kubwa ya watalii, ambao jana walitarajia kuendelea na safari kwenda Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na wengine kurejea Arusha walikwama katika barabara hiyo na kubaki wamekaa kwenye magari.
Mmoja wa watalii hayo, Johnson Taylor kutoka Uingereza alisema alikuwa ametarajia kuwahi Arusha jana ili kusafiri kurejea nchini kwao, lakini amekwama.
“nimefika hapa tangu saa 12:00 asubuhi, lakini tumeshindwa kupita kutokana na barabara kuharibika…hii ni tatizo kubwa sasa tunafanya mawasiliano kuona kama tiketi za safari zitabadilishwa”alisema Taylor.
Wananchi waombwa
kuhama mabondeni
Mbunge wa jimbo la Karatu, Mchungaji Israel Natse na mkuu wa wilaya hiyo, Methew Sadoyeka walitoa wito kwa wananchi ambao wanaishi katika maeneo ya mabonde kuhama sasa kwani taarifa za utabiri wa hali ya hewa zimesema kutakuwa na mvua nyingi hadi Desemba.
JWTZ waenda kufungua barabara
Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), kutoka Makao Makuu ya Brigedi ya Mbuni wilayani Monduli, jana walifika eneo la tukio Mto wa Mbu kusaidia kazi ya kufungua barabara ya Karatu-Arusha ili kuruhusu magari kupita.