Waliondoka barani afrika kwenda Ulaya kutafuta utajiri wa pesa. Sasa wanashindana kuvuna fedha katika klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya. Wafuatao ni wanasoka watano wa Afrika wanaoongoza kwa utajiri katika soka la Ulaya.
Samuel Etoo (Dola 40 milioni)
KABLA hajapata mkataba mnono akiwa na klabu ya Anzhi Makhchkahala ya Russia, Etoío ndiye baba wa fedha miongoni mwa wachezaji wa Afrika wakiwa huko ng'ambo.
Etoío anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 40 milioni. Kwa mwaka anaingiza kiasi cha Pauni 7 milioni. Hii ilikuwa wakati akiichezea Inter Milan kabla hajasaini mkataba mpya nchini Russia ambao unamlipa mara tatu ya kiasi hicho.
Kwa mwaka jana tu, Etoío aliingiza kiasi cha Dola 15 milioni kutokana na mikataba yake ya kibiashara na Puma na Ford pamoja na mshahara wake akiwa na Inter Milan. Kwa sasa ndiye mwanasoka anayelipwa zaidi duniani akipokea kiasi cha Pauni 365,000 kwa wiki akiwa amewaacha mbali mastaa kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Carlos Tevez, Kun Aguero na wengineo.
Aliwahi kuwanunulia wachezaji, makocha na maofisa wa timu ya taifa ya Cameroon kila mmoja saa yenye thamani ya Pauni 26,000 baada ya timu hiyo kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka jana. Etoío pia huwa hachukui pesa zozote za posho anaporudi kuichezea timu ya taifa huku akijikatia mwenyewe tiketi za ndege tofauti na wachezaji wengine.
Didier Drogba (Dola 30.7 milioni)
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Times, Drogba ana utajiri unaokadiriwa kufikia kiasi cha Pauni 19 milioni ambazo ni sawa na Dola 30 milioni akishika nafasi ya pili nyuma ya Etoío kwa wanasoka wa Kiafrika wanaotesa Ulaya.
Kwa mshahara wa mwaka, Drogba anaingiza kiasi cha Pauni 5.5 milioni huku akiwa na mkataba unaompatia kiasi cha Pauni 105,000 kwa wiki Stamford Bridge. Drogba ana mkataba mnono na kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsi, lakini pia ana mikataba na kampuni za Nike na Orange France.
Kudhihirisha utajiri wake, mwishoni mwa mwaka 2009, Drogba alitoa kiasi cha Pauni 3 milioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali katika jiji la Abidjan nchini Ivory Coast.
Michael Essien (Dola 22 milioni)
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Times, kiungo huyu wa kimataifa wa Ghana anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 22 milioni ambazo ni sawa na Pauni 14 milioni.
Misimu miwili iliyopita, Chelsea ilimuongezea mshahara wake mpaka kufikia Pauni 80,000 kwa wiki na hilo liliongeza akaunti yake kwa kiasi kikubwa kwa mujibu wa takwimu zilizofanyika Mei mwaka huu.
Dosari kubwa katika utajiri wa Essien ni kitendo kilichoripotiwa miaka ya karibuni kuwa alikuwa amemtelekeza baba yake mzazi nchini Ghana bila ya kumjali kwa kile kinachoitwa tofauti za kifamilia. Hata hivyo kwa sasa wana maelewano mazuri na amemjengea nyumba ya kuishi.
Yaya Toure (Dola 11 milioni)
Mashine hii ya Manchester City inakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 11 milioni ambazo kwa pesa za Kiingereza ni sawa na Pauni 7 milioni. Yaya ni mmoja kati ya wachezaji wanaolipwa fedha nyingi duniani huku mkataba wake na Man City ukimpatia kiasi cha pauni 200,000 kwa wiki.
Mapato yake kwa mwaka yanakadiriwa kufikia Pauni 8.8 milioni lakini ataingiza Pauni 4 milioni na zaidi baada ya kukatwa kodi na serikali ya Uingereza. Hata hivyo, hapa amejumlishiwa na kiasi cha fedha alizokuwa anapata akiwa na Barcelona ya Hispania.
Baada ya kuipatia Manchester City nafasi ya kucheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Toure alipata kiasi cha Pauni 800,000 kama bonasi kwa mujibu wa mkataba wake na matajiri hao wa Man City.
Pamoja na utajiri wake, Yaya hapendi maisha ya anasa na hivi karibuni aliripotiwa akiwalaumu wanasoka wengi maarufu, hasa wa Ligi Kuu England kwa kuendekeza zaidi anasa mpaka asubuhi.
Kolo Toure (Dola 11 milioni)
Kaka wa Yaya Toure ambaye kitita chake kinatoka sare na cha mdogo wake kwa sababu ghafla Yaya anavuna pesa nyingi kwa wakati mfupi wakati Kolo amevuna kwa muda mrefu tangu akiwa Arsenal.
Kolo anapokea kiasi cha Pauni 120,000 kwa wiki akiwa na Man City huku mdogo wake akipokea Pauni 200,000 kwa wiki. Kwa mwaka Kolo anaingiza kiasi cha Pauni 5.7 milioni huku akijivunia pia mkataba wake na kampuni ya Adidas.
Kolo amejikuta katika wakati mgumu baada ya kufungiwa na FA ya England kwa kufeli vipimo vya kutumia dawa za kuongeza nguvu, lakini amerudi tena uwanjani Septemba baada ya kumaliza adhabu yake ya miezi sita.