Sunday, December 4, 2011
Silvio Berlusconi- Amaliza enzi za kashfa kwa kujiuzulu
Gbagbo kutua The Hegue
Aliyekuwa rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo amesafirishwa hadi nchini Uholanzi iliko Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ambayo itaanza kusikiliza kesi yake kesho.
Gbagbo anaingia kwenye historia kwa kuwa mtu wa kwanza aliyekuwa rais kufikishwa mahakamani hapo tangu mahakama hiyo ianzishwe mwaka 2002.
Anatuhumiwa kwa kuwa aliunga mkono uhalifu japo si moja kwa moja wa mauaji, ubakaji, utesaji na vitendo vengine vibaya dhidi ya binadamu. Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka, 66, alipelekwa The Hague mapema wiki iliyopita.
ICC imekuwa ikifanya uchunguzi wa ghasia za miezi minne Ivory Coast, iliyoanza baada ya Gbagbo kukataa kumwachia madaraka Alassane Ouattara katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Waendesha mashtaka wamesema takriban watu 3,000 walifariki dunia kwenye vurugu za pande zote mbili na kulikuwa na mateso mengine ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia.
Kabla ya kupelekwa the Hague, alikuwa kwenye kifungo cha nyumbani huko Korhogo Kaskazini mwa Ivory Coast tangu Aprili mwaka huu, aliondolewa kwa msaada wa majeshi ya Ufaransa na Umoja wa Mataifa yaliyofanya mashambulio ya anga.
Aling'ang'ania madaraka
Gbagbo alishindwa na kiongozi wa upinzani, Allasane Ouattara kwenye uchaguzi wa urais wa Novemba mwaka jana. Alikataa kuachia madaraka, licha ya juhudi za Umoja wa Afriaka (AU) kumtaka afanye hivyo.
Ulikuwa uchaguzi wa kihistoria baada ya yeye na mpinzani wake kila mmoja, kujiapisha kuwa rais na kutangaza baraza la mawaziri, huku mmoja akikaa hotelini na yeye Gbagbo kung'ang'ania Ikulu.
Siku aliyokamatwa, kulia ni mkewe
Viongozi mbalimbali walimsihi aachie madaraka kwa hiari kuepusha vurugu na aibu ya kutolewa madarakani, lakini vyote havikufua dafu mpaka yalipozuka mapigano.
Pengine Gbagbo aliamua kulipiza kisasi kwa kile alichofanyiwa mwaka 2000, na Jenerali Robert Guei aliyejitangaza mshindi ilhali hakushinda.
Hata hivyo Guei alikimbia baada ya kukaliwa kooni na kumuachia madaraka Gbagbo. Lakini yeye hakuachia mpaka lipokuja kutolewa kwa fedheha kubwa katika hoteli moja aliyojichimbia nchini humo.
Hata hivyo wakili wa utetezi wa Gbagbo, anasema mteja wake hajatendewa haki kwa kuwa hakutaarifiwa kuwa angepelekwa The Hegue na badala yake amesafirishwa ‘mzobemzobe’.
Anasema mteja wake amewahi kuwa mtu mwenye madaraka makubwa hivyo anapaswa kupewa taarifa kwa kila hatua inayoendelea katika kesi yake kwa kuwa pia hali yake kiafya si nzuri.
Baba ambaka binti yake miaka 34 mfululizo, amzalisha
Kwa utamaduni wa karibu jamii zote duniani, ni jambo ambalo haliwezi kukubalika, lakini baba mmoja raia wa Ujerumani wiki hii ameshtakiwa kwa kosa la kumbaka binti yake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 34 na kumzalisha watoto watatu wa kiume.
Adolf Bergbaue (69), ambaye alikuwa akiishi na familia yake huko Bavaria, ameshtakiwa kwa makosa zaidi ya 497, likiwepo la ubakaji katika Mahakama ya Nuremberg baada ya kubainika kutenda kosa hilo.
Katika kesi hiyo, imeelezwa kuwa binti huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 46, aliamua kumweleza mke wa daktari kuhusu matatizo ya mmoja wa watoto wake na hapo ndipo siri ilipofichuka.
Bergbaue anadaiwa kutumia viboko kila wakati alipokuwa akihitaji kufanya mapenzi na binti yake huyo. Hata hivyo kwa mujibu wa binti huyo, alianza kubakwa na baba yake kwa mara ya kwanza alipokuwa na umri wa miaka 12. Anaeleza kuwa alikuwa akibakwa mara kadhaa kwa wiki.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Gabriels Gorsolke, mzee huyo alikuwa akiishi na mkewe miaka yote alipokuwa akitenda unyama huo. Watoto wote watatu walizaliwa akiwa na familia yake yote, mkewe, bintiye na mtoto wake mwingine.
Gorsolke alisema Bergbaue alikuwa ameajiriwa wakati binti yake akiwa na umri mdogo, amekuwa hana kazi kwa kipindi kirefu.
Anaeleza kuwa kwa kipindi hicho ndipo aliamua kumfungia nyumbani na kumchunga asitoke wala kuzungumza na watu huku akiendeleza unyama wa ubakaji.
Baba huyo alikuwa akiongozana na bintiye alipohitaji kutoka na kamwe hakutaka awasiliane wala kuwa na mahusiano na mwanaume mwingine.
Gorsolke alisema kuwa mama wa binti huyo alikuwa akifahamu kitendo cha mumewe, lakini hakuweza kushtakiwa kwani mahakama ilieleza kuwa huenda mwanamke huyo alikuwa na mapungufu ya amri katika familia yake.
"Hivi sasa mama wa binti huyo pamoja na mwanaye wanaishi katika mji fulani ambao mahakama haiwezi kuutaja," alisema Gabriels.
Kwa mujibu wa binti huyo, baba yake alikuwa akimbaka katika kitanda anachotumia na mama yake na wakati mwingine katika chumba chake cha kulala na wakati mwingine alimlazimisha kuendesha gari na kwenda sehemu ya mbali , kisha kumbaka ndani ya gari.
"Sijawahi kutenda kitendo hicho," alisema Bergbaue ambaye anadaiwa kumshikia kisu wakati mwingine alipobaini kuwa binti yake hakuhitaji kutenda tendo hilo pamoja naye.
Binti huyo alizalishwa na baba yake watoto watatu ambao wote walikuwa na matatizo ya akili (mtindio wa ubongo) na mmoja wao alifariki akiwa mdogo miaka kadhaa iliyopita. Mtoto wa pili ni mkubwa na anaishi mbali na mama yake.
Mtoto wa tatu alizaliwa mwaka huu na kufariki hivi karibuni. Kifo chake chenye utata ndicho kiliwazindua madaktari na kuamua kufanya uchunguzi wa kina na kugundua sakata hilo.
Madaktari waliamua kufanya uchunguzi wa DNA, ndipo walipogundua kuwa baba wa watoto hao ni baba mzazi wa mama wa watoto hao.
Bergbaue alikamatwa mapema Machi na amekuwa akishikiliwa hadi wiki hii alipoburutwa kortini.
"Hata hivyo alikubali kuwa na mahusiano na binti yake, lakini alisema kuwa hakuwa akimbaka bali walikuwa na makubaliano," alisema Gabriels.
Kumekuwa na matukio kadhaa ya kutisha katika bara la Ulaya kwa miaka kadhaa sasa. Miaka ya karibuni raia wa Australia, Josef Fritzl alimfungia binti yake katika gereza kwa miaka 24.
Fritzl alikuwa akimbaka kila wakati na aliweza kumzalisha watoto kadhaa. Baba huyo alishtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 2009.
Miaka 103 ana watoto 57, wajukuu 200, vitukuu 70
Kwa mara ya kwanza niliposikia habari za mzee Nterege Nyigana Mutari ana umri wa miaka 103, ana watoto 57, wajukuu 200 na vitukuu 70, sikuamini.
Nilijiuliza maswali mengi moja likiwa ni kwa nini mzee huyo asiwemo katika kitabu cha maajabu ya dunia? Hiki ni kitabu ambacho huchapishwa kila mwaka kikiwa na mkusanyiko wa rekodi za dunia kuhusu mafanikio ya binadamu pamoja na maajabu mbalimbali.
Kuishi miaka 103 na kuwa na watoto 57 sio jambo dogo, watoto ambao nao wanakuletea wajukuu 200, na wajukuu nao wanakuletea vitukuu 70.
Kama hiyo haitoshi, anaamua kujenga shule ili wapate elimu bora, tena katika shule hiyo yenye wanafunzi 744, wanafunzi 200 wanatoka katika familia yake, wakiwemo wajukuu na vitukuu. Sasa mzee kama huyu, kwanini asiwemo katika maajabu ya dunia?
Baada ya kufikiria mambo mengi niliamua kumtafuta mzee Nterege ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Nyamaitagi, Kijiji cha Nyamakobiti, kata ya Majimoto Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Nterege na mkewe
Mzee huyu mcheshi ambaye ni wa kabila la Wangoreme anaishi umbali wa kilometa 70 kutoka makao makuu ya wilaya ya Serengeti, mjini Mgumu.
Historia ya Mzee huyo imejaa mengi yakiwemo machungu na raha, lakini kwa upande wake anasema vikwazo katika maisha ni jambo la kawaida.
“Nina miaka 103, wajukuu zaidi ya 200 na vitukuu zaidi ya 70, nilizaa watoto 57 lakini ninachoweza kuieleza jamii ni kwamba watoto wangu nimeamua kuwapa elimu bora kwa kuwa elimu ndiyo ufunguo wa kila kitu hapa duniani,” anasema Nterege.
Maisha yake
Nterege alizaliwa mwaka 1908 lakini akajulikana kwa jina la "Reterenge’’, jina ambalo anasema alipewa na daktari raia wa Ujerumani.
Anasema alizaliwa katika eneo la Kyehonda -Kimeli ambalo kwa sasa ni eneo la kijiji cha Nyamutita na kwamba wakati huo baba yake alikuwa na wake wawili.
“Kwa upande wa mama yangu tulizaliwa wawili tu, mimi na dada yangu ambaye anaitwa Nyakimaiga, mama yetu alikuwa mke wa pili wa baba,” anasema Nterege.
Anasema mwaka 1918 baada ya baba yake kufariki dunia, ndugu wa baba yake walichukua mifugo yote iliyoachwa na baba yake wakiwemo Ng’ombe zaidi ya 100, na kuwanyang’anya nyumba waliyokuwa wakiishi na mama yao.
“Walitufukuza pamoja na mama kwa kuwa alikuwa mke mdogo wa marehemu baba, walisema kuwa mama yetu wa kambo ambaye alikuwa mke mkubwa ndio alikuwa na haki ya kupata kila kitu. Kuanzia hapo tulianza kuishi kwa shida.”
Anasema baada ya tukio hilo alianza maisha ya kujitegemea ambayo yalimfanya ashindwe kwenda shule na kujikita katika kilimo na wakati mwingine kufanya kazi ya kuchunga mifugo ya watu mbalimbali ili kupata fedha za kuweza kujikimu.
“Mwaka 1937 nilioa mke wa kwanza, Wansama Moremi ambaye kwa sasa ni marehemu nilihamia eneo la Nyamakobiti kuanza maisha mapya ya ndoa…, mke wangu nilimtolea maali ya Ng’ombe kumi niliowanunua baada ya kuuza Ulezi niliolima kati ya mwaka 1935 na 1936,” anasema Nterege.
Nyumbani kwake
Wazo la kuwa na familia kubwa
Anasema katika maisha yake mapya baadhi ya mambo yaliyokuwa yanamsumbua, ilikuwa ni jinsi gani angeweza kupata watoto wengi kwa kuwa alizaliwa yeye na dada yake tu.
“Wakati ule kuwa na familia au ukoo mkubwa kilikuwa kitu cha heshima katika mila zetu,” anasema Nterege.
Pia, anasema ukubwa wa familia ulikuwa muhimu ili kuweza kupambana na vitendo vya wizi wa mifugo ambapo mara kwa mara kuliibuka mapigano ya kikabila kati ya kabila lake na Wakulya na Wangoreme.
“Maisha ni mapambano. Nilianza kufanya biashara ya mifugo mwaka 1940 nikishirikiana na Chifu Makongoro wa Waikizu. Nilipata Ng’ombe 800 wa kwangu mwenyewe ila kwa sasa wamebaki 220 baada ya kuwapa watoto wangu kwa ajili ya kuanza maiasha yao ya kujitegemea,”
Kujenga shule
Mzee Nterege ambaye bado ana kumbukumbu ya mambo mengi licha ya kuwa na umri mkubwa anasema kuwa mwaka 1988 baada ya kuona wajukuu zake wakipata usumbufu wa kwenda shule zilizokuwa vijiji vya mbali, aliamua kubuni wazo la kuanzisha shule ya msingi kuondoa usumbufu huo.
Anasema alianza ujenzi wa shule kwa kutumia magari yake kubeba mchanga na kokoto huku akiwahamasisha wakazi wa kijiji hicho kuchangia ujenzi.
“Ilikuwa ngumu kuwashawishi kwa kuwa kipindi hicho watu walikuwa hawapendi kuelezwa habari za kuchangia fedha kwa ajili ya jambo fulani.
Walimu na wanafunzi ambao ni watoto, wajukuu na vikuu vyake
Mkuu wa shule hiyo anasemaje
Akizungumzia historia ya shule hiyo mkuu wa shule hiyo, Machumbe Mairo anasema kuwa huwezi kuzungumzia maendeleo ya shule hiyo bila kumtaja mzee Nterege.
Anasema shule hiyo ina wanafunzi 744 na anafafanua kwamba pamoja na changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwa ni pamoja na uhaba wa walimu.
Pamoja na matatizo hayo alisema inafanya vizuri ambapo wanafunzi wengi hufaulu kuendelea kidato cha kwanza.
Tanzania, Zambia zashindwa kumkamata Bush, atua Ethiopia
Baada ya Tanzania na Zambia kukaidi matakwa ya Amnesty International ya kumkamata aliyekuwa Rais wa Marekani George W Bush, fursa ya mwisho ya kumtia nguvuni kiongozi huyo itajitokeza wakati akiwa nchini Ethiopia.
Kabla ya Bush kuanza safari yake ya siku tano ya kuzitembelea nchi tatu za Afrika iliyoanza Desemba mosi, Amnesty International ilitoa wito kwa Tanzania, Zambia na Ethiopia kumtia mbaroni Bush kutokana na jinai alizotenda akiwa madarakani.
Bush tayari ametua nchini Ethiopia jana katika ziara ya siku mbili ambayo anaikamilisha ziara hiyo leo.
Kwa mujibu wa Amnesty International, sheria za kimataifa zinasema watenda jinai za kivita hawapaswi kuwa huru na kwa hivyo ni wajibu wa nchi atakazotembelea kumtia nguvuni Bush.
Mtawala huyo wa zamani wa Marekani anadai yuko Afrika kuwasaidia wagonjwa wa Ukimwi, Malaria na Saratani katika hali ambayo alihusika katika mauaji ya mamia ya maelfu ya raia wakiwamo wanawake na watoto wasio na hatia Iraq, Afghanistan na maeneo mengine ya dunia.
Mapema mwaka huu Bush alifutilia mbali safari yake huko Uswisi baada ya hofu kuwa angetiwa mbaroni kutokana na jinai alizotenda akiwa rais tokea mwaka 2001 hadi 2009.
Mwezi uliopita Mahakama ya Kimataifa ya Jinai za Kivita ya Kuala Lumpur ilitoa hukumu kuwa Bush na Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza Tony Blair wana hatia ya kuhusika na jinai dhidi ya binadamu katika vita vya Iraq.
Bush nchini Tanzania
Bush ambaye Desemba mosi alikutana na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete walifanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika, viongozi hao walizungumzia jinsi Taasisi ya Bush ya George W Bush Institute for Global Health inavyoweza kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na changamoto kubwa za sekta ya afya na hasa magonjwa ya saratani.
Mchanga ulindwe
Wajumbe wa kundi la Sierra wakizionyesha bendera za baadhi ya nchi duniani pamoja na nembo za makampuni wakati walipokuwa wanaandamana ufukweni mjini Durban, nchini Afrika Kusini kwa kuinamisha vichwa vyao ndani ya shimo la mchanga wakizitaka serikali za mataifa mbalimbali duniani wapaze sauti zao dhidi ya kuulinda mchanga kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.