Sunday, January 15, 2012

Mbunge Chadema afariki


Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Regia Estelatus Mtema (32), amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha, kupinduka eneo la Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani jana.

Ajali hiyo ilitokea saa 5:30 asubuhi karibu na Sekondari ya Ruvu, wakati mbunge huyo na watu wengine saba, wakisafiri kwa gari aina ya Toyota Landcruiser wakitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.

Akielezea mazingira ya ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, alisema mbunge huyo alifariki baada ya gari hilo alilokuwa akiendesha mwenyewe, kuacha njia na kupinduka.


Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya Mtema kujaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake na ghafla aliona gari lingine likija kasi mbele yake, katika kujaribu kulikwepa, ndipo gari hilo lilipinduka.

"Wakati akiwa hajalipita gari hilo aliliona gari lingine likija mbele kwa kasi , katika kulikwepa wasigongane uso kwa uso, alitoa gari lake barabarani na kusababisha kupinduka,’’ alisema Mangu.

Alisema watu wengine saba waliokuwa kwenye gari hilo walijeruhiwa, wawili kati yao hali zao zilikuwa mbaya, walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, huku wengine watano, wakiwahishwa Hospitali Teule ya Tumbi Kibaha.

Aliwataja majeruhi waliolazwa Tumbi kuwa ni Lawrence Mtokambali (58), Benadetha Mtema (50), Peter Madesa (50) na Rogers Abdallah(18).


Chadema yatoa tamko

Chadema kilisema kuwa Mtema alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho na Waziri Kivuli wa Kazi na alikuwa mchapa kazi hodari katika majukumu mbalimbali yakiwepo ya kijamii na kisiasa.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Chadema jana na kusainiwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho, John Mnyika ilieleza kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibroad Slaa, wajumbe wa Kamati Kuu, Wakurugenzi wa chama hicho makao makuu na wabunge, wameshtushwa na kifo hicho na kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Chadema kimesema taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya kukamilisha majadiliano kati familia ya marehemu, chama na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kufuatia kifo hicho, mkutano wa Chadema uliokuwa umepangwa kufanyika jana Mjini Kibaha umehirishwa hadi itakapotangazwa wakati mwingine.



Elimu yake

Mtema alizaliwa Aprili 21, 1980. Alisoma elimu ya msingi kati ya mwaka 1989 na 1995. Alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani, Dar es Salaam mwaka 1996 hadi 1999 na kuhitimu kidato cha nne.

Aliendelea kidato cha tano 2002 na sita kati ya mwaka 2000 na 2002 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Machame, mkoani Kilimanjaro.

Mwaka 2003 hadi 2006 alisoma Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na kupata Shahada ya Maarifa ya nyumbani na Lishe.

Baada ya kuhitimu shahada yake, marehemu Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na Chadema na kuteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya chama hicho.

Baadaye aliteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya chama hicho, nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum.


JK amtumia rambirambi Mbowe

Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kufuatia kifo cha mbunge huyo.

Katika salamu hizo, Rais ameelezea kusikitishwa kwake na taarifa za kifo cha mbunge huyo na kueleza kwamba, marehemu Mtema amepoteza maisha akiwa kijana na kwamba pigo hilo si kwa Chadema pekee bali kwa taifa zima.

“Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi habari za kifo cha Mheshimiwa Mtema katika ajali ya gari. Siyo kwamba ajali hii imechukua maisha ya kijana bali imelinyang’anya taifa mbunge hodari, na kwa hakika, kifo chake siyo tu ni pigo kwa chama chako bali ni pigo kwa sote na kwa taifa letu kwa jumla.

"Nakutumia wewe binafsi, chama chako na wanachama wake salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo na msiba huu mkubwa," alisema Rais Kikwete kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Aliongeza: “Napenda ujue kuwa niko nanyi katika msiba huu. Napenda vilevile uniwasilishie salamu zangu za rambirambi za dhati kabisa kwa wana-familia, ndugu na jamaa wa marehemu Mheshimiwa Mtema.

Taarifa hiyo imemwomba Mbowe kufikisha salamu za Rais Kikwete kwa familia ya mbunge huyo na kuijulisha kuwa amepokea habari hizo kwa huzuni kubwa.

"Wajulishe kuwa nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, awajalie uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake.





Ajali ya meli, Watu 70 wapotea, nahodha wa meli akamatwa


Wakuu wa forodha nchini Italia wamesema watu 70 wamepotea, baada ya meli ya abiria iliyobeba watu zaidi ya 4000 kwenda mrama katika mwambao katika Visiwa vya Tuscany nchini humo.

Meli hiyo ya abiria iitwayo Costa Concordia iligonga mwamba baharini na kusababisha tundu la mita 70 hadi 100 katika eneo lake la mbele, muda mfupi baada ya kuanza safari yake Ijumaa kutoka bandari ya Civitavecchia karibu na mji wa Roma.


Kikosi cha majanga kikiingia katika meli hiyo kuokoa abiria

Zaidi ya watu 42 wamejeruhiwa, ambao watu watatu hali zao ni mbaya na wengine 70 ambao ni miongoni mwa watu waliokuwa ndani ya meli hiyo hawajulikani walipo.

Meli hiyo ambayo ilikuwa imebeba abiria na wafanyakazi wapatao 4,000 ilipinduka upande mmoja. Hata hivyo, waokoaji nchini humo wanaendelea na juhudi za kutafuta watu waliopotea, baada ya meli hiyo ya abiria kupinduka.

Manrino Giampedron (57), mtumishi wa meli hiyo naye alikuwa miongoni mwa walionusurika, yeye alikuwa wa tatu kuokolewa na inasadikiwa alivunjika mguu wake mmoja

Mkuu wa kazi za uokoaji alisema hawawezi kuthibitisha idadi ya watu waliopotea kutokana na hali ya taharuki iliyopo iliyosababishwa na ajali hiyo. Hata hivyo, wakuu wa forodha nchini humo wanakadiria watu 70 wamepotea.

Habari zinasema kuwa, abiria mmoja alisema kuwa walikua wajitayarisha kwa chakula cha usiku waliposikia kishindo kikubwa kabla ya meli hiyo, kutikisika na kusimama na taa kuzimika.













Kile kibox (black box) kilipatikana, hiki ndicho kitakachotoa uhakika wa kujua ajali hiyo ilisababishwa na nini

Hii ni sehemu ya chini ya meli inavyoonekana ilivyoharibika baada ya kugonga mwamba huo, hapa linaonekana jiwe likiwa bado limeng'ang'ania sehemu hiyo hata baada ya kuitoboa.

Hapa anaonekana raia akishangaa

Uokoaji ulikuwa wa hali ya juu, hapa waokoaji walitumia helkopta pia

Nahodha akamatwa

Wakati huohuo, vyombo vya habari nchini humo jana vimeripoti kuwa nahodha wa meli hiyo, amekamatwa wakati uchunguzi unafanyika juu ya madai ya kuua bila kukusudia na kuitelekeza meli yake.

Nahodha wa meli hiyo, Francesco Schettino akiwa mikononi mwa polisi

Mkuu wa kampuni inayomiliki meli hiyo, Gianni Onorato, alisema ushahidi wa awali unaonyesha kuwa meli iligonga mwamba kisha nahodha kwa haraka akafuata utaratibu wa kuwatoa abiria melini.