Monday, July 11, 2011

Mheshimiwa Sugu kizimbani Mbeya


Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi na wezanke wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mbeya kwa tuhuma za kuandaa mkutano wa hadhara kinyume cha sheria.

Mbilinyi ni mbunge wa saba wa Chadema kupanda kizimbani akitanguliwa na wabunge wenzake, Freeman Mbowe (Hai), Godbless Lema (Arusha), Joseph Selasini (Rombo), Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Esther Matiko (Viti Maalum), ambao wanashtakiwa kwa tuhuma tofauti katika mahakama mbalimbali nchini.

Mbilinyi maarufu kwa jina la ‘Mr II au Sugu’ alifikishwa mahakamani jana pamoja na wenzake ambao ni Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako na Katibu Mwenezi wa chama hicho wilaya ya Mbeya Mjini, Job Zebedayo Mwanyerere.

Mama Salma azindua uchangiaji madawati

Mke wa Rais Salma Kikwete, akizindua nembo ya Taasisi isiyokuwa ya Kiserikari ya Hassan Maajar Trust, itakayoanzisha kampeni ya kusanya fedha za kukununulia madawati kwa ajili ya shule za msingi na sekondari Kwanza kushoto ni Mjumbe wa Bodi Sharriff Maajar na Mwenyekiti wa Mfuko Balozi Mwanaidi Sinare Maajar.


Mke wa Rais Jakaya Kikwete, mama Salma Kikwete, amezindua kampeni ya kumaliza tatizo la madawati katika shule za umma nchini.

Kiasi cha Sh3 bilioni kinatarajiwa kukusanywa chini ya kampeni ya miaka miwili.

Kampeni hiyo inayoendeshwa na Taasisi ya Hassan Maajar Trust (HMT), ambayo Mwenyekiti wake ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mwanaidi Maajar, ilizinduliwa jana jijini Dar es Salaam.

"Lengo la kampeni hii ni kukusanya Sh3 bilioni katika kipindi cha miaka miwili au mitatu ijayo, fedha zitakazochangwa zitatumika kununulia madawati kwa ajili ya shule za umma za msingi na sekondari, ili kuboresha elimu nchini," alisema Balozi Maajar.


Waziri apokelewa kwa mabango ya malalamiko

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, akimsililiza Diwani wa Kata ya Nairokanoka, wilayani Ngorongoro, Edward Maura (kulia), alipokuwa akitoa maelezo kuhusu hali ya njaa katika kata yake juzi. Kati kati ni Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro, Benard Murunya na wa pili kushoto ni, Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro, Metui ole Shaudo.


Wananchi wa Kijiji cha Nainokanoka ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), juzi walimpokea kwa mabango yenye malalamiko mbalimbali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.

Mabango hayo ni pamoja na yaliyokuwa na ujumbe wa kuishinikiza serikali, iwape ajira ya asilimia 75 katika mamlaka hiyo.

Mengine yalikuwa na ujumbe uliohoji usawa katika elimu, njaa inayowakabili, utegemezi na mbadala wa kuzuiwa kufanya shughuli za kilimo ndani ya hifadhi.

Akizungumza baada ya kuyasoma mabango hayo, Waziri Maige alitoa maelezo kuhusu malalamiko ya wananchi hao.

"Nimesoma mabango yote lakini sehemu kubwa ya malalamiko yenu, tunaweza kuyapatia ufumbuzi hasa kwa kuzingatia kuimarika kwa mahusiano,kati ya wananchi, Baraza la Wafugaji na NCAA,"alisema Maige.

Hii Bongo jamani


Wakazi wa Kijiji cha Nyamilangano Kata ya Kisuke wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wakichota maji katika kisima ambacho kimezungukwa na uchafu ambao unatishia maisha ya wakazi hao. Kisima hicho kimekuwa kikitumia wa wakazi 3,806 pamoja mifugo.

Bila ya aibu!!


Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, akimsililiza Diwani wa Kata ya Nairokanoka, wilayani Ngorongoro, Edward Maura (kulia), alipokuwa akitoa maelezo kuhusu hali ya njaa katika kata yake juzi. Kati kati ni Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro, Benard Murunya na wa pili kushoto ni, Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro, Metui ole Shaudo.

Kweli huyu ni shetani mwekundu!!


Shabiki wa Manchester United aliyejulikana kwa jina moja tu la Michael alitoa mpya.
Alikuwa akiangalia mechi kati ya Manchester United na Liverpool katika uwanja wa Old Trafford.
Karibu na alipokuwa amekaa Michael kulikuwa kuna kiti kitupu.
"Hicho kiti cha nani?" aliuliza mtu aliye karibu na Michael.
"Mke wangu ana kawaida ya kukaa hapa," alijibu Michael.
"Kwanini hayupo hapa?" mtu huyo alizidi kuuliza.
"Amefariki," alijibu Michael.
"Sasa kwanini haukumpa rafiki yako tiketi aje kuangalia mechi?" alihoji tena mtu huyo.
"Rafiki zangu wamekwenda kwenye mazishi ya mke wangu," alisema Michael.

Prince kumsimamia mtoto wa Beckham


Mjukuu wa Malkia wa Uingereza, Prince William na mkewe Princess Kate watasimamia ubatizo wa mtoto wa David Beckham.
Beckham alikutana na watu hao jijini Los Angeles na kuwazawadia jezi ya timu yake ya LA Galaxy.
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba William na Kate kusimamia ubatizo huo.
Beckham, alihudhuria dhifa kwa ajili yao iliyofanyika kwenye ubalozi mdogo wa Uingereza jijini Los Angeles.
Prince William na mkewe pia walimtakia kila la heri Victoria Beckham, ambaye ni mja mzito.
Beckham aliwaambia; "Victoria alitaka kuja lakini kwa sasa amechoka sana."
William alijibu; "Usiwe mpuuzi. Naomba umtumie Victoria salamu zetu."

Balotelli akodiwa mlinzi


Mshambuliaji wa Manchester City, Mario Balotelli ametafutiwa mlinzi na klabu yake.
Mabosi wake katika klabu ya Manchester City wamepanga kuajiri mlinzi na msaidizi maalum kwa ajili ya Balotelli.
Balotelli amekuwa kipenzi cha mashabiki tangu atue katika timu hiyo licha ya tabia zake kutotabirika.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Inter amefanya vituko vingi tangu atue Manchester City.
Alisababisha ugomvi mkubwa wakati wa mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United msimu uliopita.
Pia amewahi kulazimisha kutembelea gereza la wanawake ili kuona jinsi kulivyo.

Mke wa Ashley Cole aonywa


Mke wa beki wa Chelsea, Ashley Cole amerudi Marekani ili kuagana na mpenzi wake, Derek Hough.
Dereck, hata hivyo amemwonya Cheryl Cole kuhusiana na uamuzi wa kumrudia mumewe Ashley.
"Usimrudie huyo jamaa ni mtu muungwana sana."
Dereck, ambaye ni dansa amechukizwa na kitendo cha Cheryl kurudiana na mumewe na kumwonya kuwa anajitakia matatizo.
Amemwonya Cheryl hatakuwa tayari kurudiana naye ikiwa Ashley atamsaliti tena.
Cheryl, 28, alikwenda Los Angeles, Marekani akiwa amefuatana na Kimberley Walsh, ambaye wako naye kwenye bendi ya Girls Aloud.
Walipofika huko ndio walikutana na Dereck na kula naye chakula katika mgawaha wa West Hollywood.

Umbea tu, nani kawaambia mi mjamzito?


Benita Nzeribe amesimama mbele ya mapaparazi akanyoosha kidole tumbo lake akiwauliza; "Mmeona mimba humu?"
Msanii huyo ambaye amekuwa akiandamwa na tetesi kwamba ana ujauzito wa miezi tisa aliibuka kujibu tuhuma hizo na akasisitiza kuwa hana na mama yake amethibitisha.
"Walisema nina mimba ya miezi tisa na nimefanya pia harusi ya siri, sababu ni kwamba nimekuwa sionekani wala sipo sokoni. Ni sawa watu kukusema lakini inauma zaidi wanavyokutafsiri tofauti."

Cossy Orjiakor ajianika Facebook


Cossy Orjiakor ameweka namba zake za nyumbani na ofisini kwenye Facebook lakini ametaja wanaume wawili wa Nigeria ambao wanamsumbua na hawataki.
Msanii huyo ambaye ni kawaida yake kuvaa nguo zinazoonyesha sehemu kubwa ya matiti yake makubwa, ameandika kwenye ukurasa wake kwamba; "Tafadhali wanawake chungeni waume zenu. Kama umeolewa au ni demu wa Oyi Vitus Obunike na Oraniaka Patrick, tafadhali waambie wazee hawa waachane na mimi, waniache. Kama hamuwaridhishi kimapenzi nendeni mkapatiwa mafunzo."
"Tafadhali niacheni niishi maisha yangu na nyie endeleeni na yenu,"alisisitiza msanii huyo ambaye sasa anapiga picha za video za wimbo wake mpya wa 'you want me'

Yvonne Nelson sasa njia panda


Yvonne Nelson ameandika barua akiomba radhi lakini lakini mamlaka ya filamu nchini Ghana imemchunia msanii huyo kwa kutotoa tamko lolote hadi sasa.
Msanii huyo alifungiwa kushiriki katika filamu yoyote na mamlaka hiyo tangu Oktoba mwaka baada ya prodyuza Abdul Mumuni wa Venus Films kuripoti utovu wa nidhamu, ukatili na kukiuka mikataba alivyokuwa akifanya msanii huyo.
Mamlaka hiyo ambayo imejumuisha maprodyuza, wasambazaji, mashirikisho imeripotiwa kuwa huenda ikatoa tamko Alhamisi kwani tayari msanii huyo ameshampigia magoti Abdul na kukiri kosa pamoja na kukubali kufanya nae kazi kwa malipo nafuu ikiwa ni sehemu ya kujikosha.
Prodyuza huyo amemsamehe lakini mamlaka husika bado haijatoa tamko muhimu kuhusu kusamehewa kifungo chake cha mwaka mmoja baada ya kukitumikia miezi tisa sasa.

Mercy Johnson amchunia Mama G

Mercy
Mercy
Mercy
Mama G

Mercy Johnson amewaangukia mastaa karibu wote wa kike na kuwaalika kwenye harusi yake itakayofanyika mwezi Agosti lakini Mama G si mmoja wao.
Habari zinadai kuwa msanii huyo anataka harusi yake iweke rekodi kwa kuhudhuriwa na mastaa wengi zaidi ndani na nje ya Nigeria kabla ya kwenda kwenye fungate katika visiwa vya malta.
Ripoti zinasema kuwa msanii huyo amekuwa akijaribu kupatana mpaka na baadhi ya wasanii ambao alikuwa na tofauti nao huku Genevieve Nnaji akiombwa kuwa msimamizi wa mkuu wa ukumbi na shughuli zote za sherehe hiyo.
Rafiki wa karibu wa Mercy alidokeza kuwa msanii mkongwe Patience Ozokwor 'Mama G' mpaka sasa hajapigiwa simu kupewa mualiko wowote jambo ambalo linaibua mjadala kwamba bado wana bifu.

Wanasoka 10 waislamu safi barani Ulaya

Wakati mwingine ni vigumu kwa mashabiki wa soka kufahamu imani za wachezaji kutokana na majina yao. Na wakati mwingine ni vigumu kwa mashabiki kufahamu imani za wachezaji kutokana na uchache wa watu wa imani fulani katika bara fulani au nchi fulani.

Wachezaji wengi barani Ulaya wana imani ya dini ya Kikristo kutokana na historia za bara hilo zilivyo. Wafuatao ni wachezaji 10 maarufu zaidi ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu. Wengi kati ya hao wanatoka nchini Ufaransa huku wakiwa na asili ya nchi za Afrika Kaskazini. Wengine wanatoka katika nchi za Afrika Magharibi.


Nicolas (Bilal) Anelka

MSHAMBULIAJI huyu wa Chelsea alibadili dini mwaka 2004 alipokwenda Falme za Kiarabu baada ya majadiliano ya muda mrefu na marafiki zake wa utotoni. Aliamua kuchukua jina la Kiislamu la Abdul-Salam Bilal. Anelka alikuwa mchezaji wa Manchester City wakati huo na alifikiria kwenda kucheza katika nchi moja ya falme za kiarabu lakini hata hivyo baadaye aliamua kwenda zake Uturuki kuchezea Fenerbache.


Franck (Bilal) Ribery

Franck Ribery ni mchezaji mwingine wa Kifaransa aliyeamua kubadili dini na kuwa Muislamu. Hii inatokana na mkewe ambaye ni Mfaransa mwenye asili ya Algeria kuwa muislamu anayeifuata dini yake kwa karibu. Ribery hivi karibuni alilipotiwa akisema “Nasali mara tano kwa siku, nafanya hivyo kwa sababu inaniwezesha kujihisi huru na kujisikia vizuri baadaye.”



Kolo (Habib) Toure

MLINZI huyu wa Manchester City alikulia nchini Ivory Coast na aliichezea Asec Mimosas kabla hajatua Arsenal. Toure ni muumini safi wa dini ya Kiislamu kama ilivyo kwa familia yake. Hivi karibuni alikaririwa akisema kwamba angependa kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wote waislamu wa Uingereza.


Frederick (Oumar) Kanoute

Mzaliwa huyu wa Ufaransa mwenye uraia wa Mali ambaye amestaafu kuichezea timu ya taifa ya Mali alianza kushika imani ya Kiislamu kikamilifu tangu akiwa na umri wa miaka 20 (sasa ana miaka 34). Aliwahi kukataa kuvaa jezi ya timu yake Sevilla iliyokuwa inatangaza mtandao wa Kamari, 888.com. badala yake Sevilla walimpa jezi ambayo haikuwa na maandishi hayo kifuani. Kanoute pia alinunua msikiti mmoja jijini Seville uliokuwa na thamani ya pauni 700,000.


Karim Benzema

Karim Benzema alizaliwa Ufaransa kwa wazazi wenye asili ya Algeria. Anasali kwa imani ya Kiislamu. Kwa sasa anachezea Real Madrid baada ya kuhamishwa kwa euro milioni 35 kutoka Olimpiki Lyon. Kwa sasa ana namba ya kudumu katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa.


Samir Nasri

Samir Nasri amekuwa moto katika klabu yake ya Arsenal kiasi kwamba Wafaransa wanamuona kama Zidane mpya. Kwa sasa anahusishwa kuondoka Emirates. Kama ilivyo kwa Zidane na Benzema, Nasri naye amezaliwa na wazazi wa Kialgeria nchini Ufaransa. Amekulia katika mazingira ya Uislamu ndani ya familia yao. Hata hivyo, mpenzi wake, Tatiana Golovan ambaye ni mcheza tenisi wa kike maarufu mwenye asili ya Urusi si Muislamu.


Yaya Toure

Yaya Toure ni mdogo wake Kolo Toure ambaye jina lake linajiochomoza namba tatu katika orodha ya wachezaji hawa. Kama ilivyo kwa kaka yake Kolo, Uislamu wa Yaya unaanzia katika familia yao nchini Ivory Coast. Hivi majuzi alielezwa kukerwa kwake na kitendo cha baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu England, hasa wale wa England kupenda kujirusha katika klabu za usiku bila aibu.


Hatem Ben Arfa

Hatem Ben Arfa ni kipaji kizuri cha soka kutoka Ufaransa. Staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa anayechezea Newcastle amezaliwa na wazazi wenye asili ya Tunisia nchini Ufaransa. Familia yake yote ni Waislamu huku hicho kikiwa kitu kinachomfanya awe muumini safi wa dini ya Kiislamu.


Khalid Boulahrouz

Khalid Boulahrouz ambaye kwa sasa anachezea Stuttgart ana asili ya Morocco huku familia yake ikiwa ni waumini safi wa dini ya Kiislamu. Staa huyu wa zamani wa Chelsea ni Muislamu wa imani ya Sunni na familia yake yote ipo katika mkondo huo. Boulahrouz ana uraia wa Uholanzi kwa sababu amezaliwa nchi hiyo.


Abou Diaby

Abou Diaby, kama ilivyo kwa familia ya akina Toure ana asili ya Ivory Coast. Alizaliwa na kukulia Ufaransa na tayari ameshaichezea Ufaransa katika ngazi zote kuanzia timu za vijana mpaka sasa anachezea timu ya wakubwa huku mwaka jana akiwa miongoni mwa wachezaji wa Ufaransa waliochemsha katika fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini. Diaby anatoka katika familia ya Kiislamu na yeye mwenyewe ni muumini safi wa imani hiyo.


Wananmichezo wa Bongo igeni hii!


Mwanariadha wa Jamaica, alitoa mpya wakati aliposhinda mbio za mita 200 nchini Ufaransa, akiwa amevalia fulana yenye picha yake wiki iliyopita.
Hiki ni kitu ambacho Muhammad Ali angeweza kufanya wakati wa enzi yake akipigana ngumi za kulipwa.
Watu wamechukulia kuwa ni majivuno ya Bolt ya kutaka kuionyesha dunia kuwa yeye ni zaidi.