Mambo matano ya kuiweka juu Chelsea
Mafanikio ya Chelsea yanategemea juhudi za wachezaji mmoja mmoja na timu yote kwa ujumla.
Chelsea ina wachezaji wazuri, lakini si kila mara wachezaji hao wamekuwa wakicheza kwa kiwango kikubwa. Katika soka hicho si kitu cha ajabu, kuna wakati mchezaji anaweza kuwika na kuna wakati anaweza kushuka kiwango na kuacha watu wakiwa midomo wazi.
Vilevile kuna baadhi ya wachezaji huwa ni muhimu katika klabu zao kuliko wengine, hiyo inategemea nafasi ya mchezaji, aina ya uchezaji na kocha anampanga mara ngapi. Chelsea nayo ina wachezaji muhimu na wengine wana umuhimu wa wastani.
Makala hii inawachambua wachezaji watano wa Chelsea ambao ni ngao ya kikosi, ambao wanaweza kuchangia kupatikana kwa ubingwa msimu huu.
5. Petr Cech
Timu zote hung'aa zinapokuwa na beki wa maana. Kama timu ina kipa mzuri, hiyo ni hatua ya kwanza kuelekea katika mafanikio. Chelsea ina bahati kwa kuwa ina kipa makini, Petr Cech. Cech amekuwa mkongwa katika kikosi cha Stamford Bridge. Ameidakia Chelsea mechi zaidi ya 300 na kuna dalili kwamba ataendelea kucheza katika klabu hiyo kwa miaka kadhaa.
Cech mwenye umri wa miaka 29 anadaiwa kuwa ndio kipa mzuri zaidi katika Ligi Kuu England kwa sasa. Mchezaji huyo yupo katika kiwango cha hali ya juu, anaweza kupigana na presha zote za Ligi Kuu England na michuano mingine ya kimataifa. Kama wachezaji wa ndani wakifanya vizuri huku Cech akiboresha kiwango chake mambo yatakuwa mazuri.
4. Winga
Hapa hatajwi mchezaji yeyote kwa kuwa nafasi ya winga ya Chelsea ni nzuri. Lakini winga wa Chelsea wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kusababisha usumbufu kutoka pembeni badala ya katikati kama walivyofanya mara kadhaa msimu uliopita.
Ikumbukwe kuwa hakuna timu inayoweza kutisha sana kama ikitegemea mipira ya kati pekee.
3. John Terry
Umri wa Terry unaweza kuwa umesonga kidogo, lakini nahodha huyo wa Chelsea anabaki kuwa mmoja wa mabeki wa kati wazuri duniani.
Chelsea inajivunia kuwa na beki huyo na amekuwa akiwaokoa katika hatari nyingi.
Mchezaji huyo ni mzuri kwa mipira ya juu na chini, ni wazi kuwa ataisaidia timu yake kufanya vizuri msimu huu.
Kama Terry akiumia au asipokuwepo uwanjani ni rahisi kuona Chelsea ikihangaika kufanya vizuri. Hiyo inaamisha kuwa uongozi wa Chelsea unatakiwa kuomba mchezaji huyo asishuke kiwango katika siku za karibuni la sivyo mambo yatakuwa magumu.
2. Frank Lampard
Watu wamekuwa wakizungumza mambo tofauti juu ya Frank Lampard, wengine wanasema ameanza kuishiwa, wengine wanasema baada ya muda mfupi ataondoka. Lakini bila kujali watu wanasema nini, ukweli ni kuwa Lampard ni mmoja kati ya wachezaji wazuri na hana dalili ya kustaafu karibuni.
Kweli, umri wake umesonga, lakini mchezaji huyo mwenye miaka 33 bado ana kiwango kikubwa. Huenda akapata shida kwenda sambamba na staili ya kocha mpya Andre Villas-Boas, lakini baada ya muda mfupi atasimama.
Tayari Lampard amejinoa vya kutosha katika mechi za kujiandaa na msimu na sasa anatakiwa kuendelea na kasi hiyo.
Lampard ni mchezaji mzuri na klabu yake inamtegemea kufanya mambo makubwa.
1. Didier Drogba/Fernando Torres
Chelsea inahitaji mabao ya kutosha.
Klabu hiyo ina washambuliaji wawili wazuri duniani lakini mmoja wao anatakiwa kuanza mara kwa mara.
Andre Villas-Boas amepanga vizuri maeneo mengine lakini linapokuja suala la washambuliaji anaonekana kuwa na wakati mgumu.
Didier Drogba na Fernando Torres wote ni wachezaji wa daraja la kwanza duniani lakini hakuna mchezaji kati yao, ambaye ameonyesha kiwango kwenye kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Watu wanaweza kusema umri wao umesonga lakini si kweli kwani Torres ana miaka 27. Kinachotokea hapo ni suala la kujiamini.
Drogba ni mchezaji mzuri lakini amekuwa akiwekwa nyuma ya Torres, na hiyo inamuondolea kujiamiani kwa kiasi fulani. Torres, ambaye alitua katika timu Januari bado hajafanya vizuri uwanjani.
Hitimisho
Kocha mpya anatakiwa kutafuta mbinu ya kuwapanga washambuliaji la sivyo hadithi yao itakuwa kama ya kocha wa zamani Carlo Ancelotti. Iwapo kocha akipata seti nzuri, kikosi kitafanya makubwa ziadi.