Monday, April 30, 2012

Kanumba alijijua anakufa


MTAALAM wa mambo ya mwanga katika utengenezaji wa filamu Swahiliwood, Steven Shoo ëSammy Shooí, amedai kuwa marehemu Steven Kanumba alijua kuhusu kifo chake.
Hilo alilijua siku ambayo alikuwa akirekodi filamu yake ya mwisho ambayo alikuwa akirekodi filamu ya Power In Love kutokana na maneno ambayo awali walijua kama utani.
"Tukiwa tunapiga picha hizo za filamu, siku hiyo alikuwa akituhimiza tumpige picha kwa kutumia simu zetu. Nakumbuka aliniambia 'Sam nipige picha bwana, naweza kufa hapa ukakosa picha yangu ukaanza kuhangaika kuitafuta picha yangu katika Internet wakati mpo na mimi hapa... kila mtu anipige piga bwana', alisisitiza lakini katika hali ya utani," anasema Sam.
Sammy, ambaye amekuwepo na marehemu kwa muda mrefu pia na kufanya kazi na mtayarishaji mwingine Ray, anasema pamoja na kutambua kwamba Kanumba alikuwa mtu mwenye utani, lakini katika kufanya naye kazi hata siku moja hakuwahi kumsisitiza ampige picha ya ukumbusho.
Anasema, mara nyingi wanapokuwa kwenye kazi, Seth ambaye ni mdogo wake Kanumba, hupiga picha kwa ajili ya matumizi ya mtandao wake, kutokana na kusisitizwa na marehemu.


"Yaani simu yangu imejaa picha za 'location' tu nikiwa na marehemu pamoja na watendaji wengi ambao tulikuwa nao katika filamu ya mwisho aliyoigiza, siamini kama kweli bosi wetu kafariki, nahisi kama kasafiri tu kama ambavyo hufanya siku zote," anasema Sammy.

Tuesday, April 24, 2012

Hakimu ambembeleza Lulu mahakamani


Msanii wa filamu, Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akibubujikwa machozi kiasi cha kumfanya Hakimu Ritha Tarimo ambembeleze ili kumnyamazisha.
Lulu anashtakiwa mahakamani hapo kwa kutuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba na alifikishwa jana kwa mara ya pili akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.
Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 3:06 asubuhi akiwa katika basi dogo la Magereza pamoja na mahabusu wengine wanawake ambalo lilikuwa likisindikizwa na magari mengine mawili na alikuwa chini ya ulinzi wa askari sita wa kike wa Magereza na askari mmoja wa kike wa Polisi wakishirikiana na askari wa kiume wa Magereza zaidi ya sita.
Mara baada kuingia katika chumba cha Mahakama, Lulu ambaye alikuwa amevalia dira jekundu alianza kulia kwa uchungu hali ambayo ilimlazimu Hakimu Tarimo pamoja na baadhi ya askari kumnyamazisha.
Ulinzi ulikuwa wa kufa mtu



Ilikuwa ni kazi kupata picha yake, hata JK halindwi namna hii!




Kutokana na kujaa kwa watu mahakamani hapo, askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza walilazimika kuufunga mlango wa Mahakama hiyo ili kesi hiyo isikilizwe.
Baada ya kesi hiyo kutajwa, Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda aliiomba Mahakama iamuru watu wote watoke nje kwa sababu walikuwa wamefunga njia ili mtuhumiwa huyo aweze kupitishwa.
Hakimu Tarimo alikubaliana na ombi hilo na kuwaamuru askari kusafisha njia ili waweze kumpitisha msanii huyo kwa kile alichosema kuwa Lulu bado ni mtuhumiwa na anaweza kuumizwa.
“Askari safisheni njia ili mtuhumiwa aweze kupita kwa sababu yeye bado ni mtuhumiwa anaweza kuumizwa,"alisema Hakimu Tarimo.
Baada ya kutolewa kwa amri hiyo, askari walitimiza wajibu wao na muda mfupi njia ilipatikana na msanii huyo kutolewa mahakamani hapo.







Jopo la mawakili
Katika kesi hiyo, Lulu anatetewa na jopo hilo la mawakili akiwemo Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Joaquine De- Melo, Kenedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe. 
De- Melo  pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King.
Fungamtama ambaye ndiye kiongozi wa jopo la mawakili hao wanaomtetea Lulu, anakumbukwa kwa kuitetea kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, katika kesi dhidi ya Tanesco, ambayo alishinda na shirika hilo kuamriwa kuilipa kampuni hiyo  zaidi ya Sh94 bilioni kwa kuvunja mkataba.
Kibatala ambaye pia anamtetea kada wa Chadema, Fred Mpendazoe katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Segerea, pia ni Makamu wa Rais wa TLS, wakati Massawe anatoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Mawakili hao walijitokeza jana mbele ya Hakimu Tarimo tayari kumtetea Lulu na baada ya mawakili hao kujitambulisha, Wakili Kaganda alisema upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama iipangie tarehe nyingine.
Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mara ya kwanza Lulu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando  akikabiliwa na la shtaka hilo la mauaji. 
Wakili Kaganda alimsomea hati ya mashtaka alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu katika maeneo ya Sinza Vatican, Wilaya ya Kinondoni, mtuhumiwa alimuua  Kanumba. Kanumba alifariki dunia siku hiyo saa 9:00 usiku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya ugomvi baina yake na Lulu.














 Hisia zikampanda
Akaanza kulia

Monday, April 23, 2012

Vingine vinafayika!.... Tunaelekea wapi?!Vifaa zinavyotarajia kutumika katika ujenzi wa daraja la mto Malagarasi mkoani Kigoma vikiwa vimekwama katika shirika la reli ya kati katika stesheni ya mkoa wa Morogoro (TRL) baada ya kudaiwa kushindwa kusafirishwa kwa vifaa hivyo kutokana na shirika hilo kukabiliwa na ukata wa mkoani hapo.

Vifaa zinavyotarajia kutumika katika ujenzi wa daraja la mto Malagarasi mkoani Kigoma vikiwa vimekwama katika shirika la reli ya kati katika stesheni ya mkoa wa Morogoro (TRL) baada ya kudaiwa kushindwa kusafirishwa kwa vifaa hivyo kutokana na shirika hilo kukabiliwa na ukata wa mkoani hapo.

Lulu kupanda kizimbani leo


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo itaitaja kesi ya mauaji ya msanii maarufu wa filamu nchini, Steven Kanumba inayomkabili msanii mwenzake, Elizabeth Kimemeta maarufu kama Lulu (17).
Kwa mara ya kwanza Lulu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando akikabiliwa na shtaka hilo la mauaji. Alisomewa shitaka hilo na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda.
Alipofikishwa mahakamani hapo, polisi walitumia mbinu za kikachero kuwapiga chenga waandishi na kupandishwa kizimbani kisha kusomewa mashtaka katika muda usiozidi dakika 10 na baadaye kupelekwa rumande.


Moja ya mbinu zilizotumika siku hiyo ili ni kutotumia magari yenye ving'ora na ulinzi wa kutisha kama ilivyotarajiwa, badala yake walitumia magari mawili madogo.
Akimsomea hati ya mashtaka, Kaganda alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu maeneo ya Sinza Vatcan, Wilaya ya Kinondoni, Lulu alimuua, Steven Kanumba. Baada ya kumaliza kusoma shtaka hilo, Kaganda alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Lulu hakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo.
Hakimu Mmbando aliamuru Lulu apelekwe rumande katika Gereza la Segerea kwa sababu shtaka linalomkabili ni moja ya yale yasiyo na dhamana.

Sunday, April 22, 2012

Joseph Kony bado anaendelea kusakwa


Mwandishi Wetu, Kampala
KIKOSI maalumu cha majeshi ya Uganda bado kinaendelea kumsaka mbabe wa kivita kiongozi wa kundi la waasi la  lijulikanalo kama “Lords Resistance Army ‘ Joseph Kony.

Askari wa Kikosi Maalumu cha majeshi ya Uganda wakiwa katika operesheni maalum ya kumtafuta kiongozi wa kundi la waasi la la Uganga la Lords Resistance Army (LNRA), Joseph Kony, hivi karibuni. Picha na AFP 
Majeshi hayo yanadaiwa kuendelea kusonga mbele kwa lengo la kumsaka mbabe huyo wa kivita nchini humo aliyepo mafichoni kwa muda mrefu.
Kikosi hicho kimedaiwa kusonga mbele katika msitu mmoja mkubwa uliopo katikati ya Afrika ikiwa ni kile walichodai kumsaka kiongozi huyo.
 Kikosi hicho maalumu chenye watu 59kinachoitwa 77 ndicho kinachoongoza katika mkakati huo wa kimataifa wa kumsaka na hatimaye kumtia mbaroni Joseph Kony na wapiganaji wake waliobakia la kundi la waasi la Lords Resistance Army (LRA).
Inadaiwa kwamba Kony anaendelea kuwa mwenyeji wa misitu hiyo iliyopo katika mipaka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo ni maficho yanayopendwa sana na LRA tangu kikundi hicho kilipokimbia kutoka Nchini Uganda.
“tutahakikisha tunawakamata watu hawa ma kuwarudisha nyumbani, ingawa ni kazi ngumu sana “alisema mmoja kati ya wanajeshi wa kikosi hicho maalumu.
Wanajeshi hao wanaimani kabisa kwamba Kony na kundi lake hilo la kihalifu bado wanaishi msituni kwa muda wote huo, huku wakiendelea kuwateka watoto na kuwatumia katika kundi hilo.
Pia wanadai kwamba chakula wanachokula ni viazi mwitu, pamoja na mifugo ambayo wamesema ni ya wizi huku wakinywa maji ya mito.

Wake wa zuma wahudhuria harusi


Mwandishi Wetu, Afrika Kusini
Hatimaye Rais wa Afrika Kusini  Jacob Zuma ametimiza ahadi yake ya kuongeza mke mwingine.
Wake zake wengine walihudhuria sherehe hiyo ambayo iltawaliwa na nyimbo za kijadi.
Rais huyo alivalia mavazi ya kijadi katika harusi hiyo iliyofana iliyofanyika nchini humo katika Jimbo la Kwazulu-Natal
Zuma mwenye umri wa miaka 70, alivaa ngozi ya chui na kubeba mkuki na ngao, mavazi ya jadi ya Kizulu, kwenye harusi iliyofanywa Jimbo la Kwazulu-Natal.
Kabla ya kuoa mke wake huyo inadaiwa kwamba bibi harusi huyo alikuwa  Bongi Ngema, alikuwa anapata fursa ya kufuatana na Rais Zuma kwenye ziara zake rasmi kwa miaka kadha. 

Kwe Tutafika namna hii?? Hata aibu? Mnaipeleka wapi taaluma hii?!


Haya ndio magazeti yetu... Sishangai lakini, mtu amekung;uta zero yake nzuri halafu anajipiga msasa miezi mitatu, unadhani ataandika nini zaidi!?

Sunday, April 15, 2012

Weweee achia mchuma huooo!

Unajua hata kama una kazi kuubwa...nzuri sanaaa....!!, Wazungu wanasema ukitaka kwenda extra mail inakubidi ufanye kazi ya ziada. Sijaelewa vizuri, ila nafikiri siku hii huyu dada alikwenda kuomba day waka kwenye hili daladala

Kanumba; Nyota iliyozimika ghafla, ataishi kwa muda mrefu


Kaburi la merehemu Steven Kanumba, hapa ni siku nne baada ya kuzikwa kwake

Baadhi ya wananchi ambao hawakuweza kwenda kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu kwa sababu mbalimbali nao waliweza kufanya hivyo hata baada ya mazishi


Mwandishi Wetu

NI msiba ambao umeingia kwenye historia na utaendelea kubaki katika kumbukumbu za wengi na hasa wapenzi wa filamu nchini.

Kifo cha Steven Kanumba ‘The Great’ kimeandika historia kutokana na kugusa watu wengi na wa kada zote, kuanzia Rais Jakaya Kikwete hadi wananchi walalahoi wapenzi wa filamu.

Jina la Kanumba litabaki katika kumbukumbu za watu waliofanikisha kwa kiasi kikubwa kukuza fani ya maigizo na hatimaye filamu hapa nchini, pia jina lake litabaki kukumbukwa na wapenzi wa filamu katika Ukanda wa Afrika Mashariki, hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda ambako alijizolea umaarufu mkubwa.

Makaburi mengi yaliharibiwa na watu kwa kukanyagwa wakati wa mazishi ya marehemu Kanumba




Yote haya




Kanumba anakumbukwa kwa hatua kubwa aliyokuwa amefikia, hatua ambayo hakuna msanii mwingine wa filamu nchini aliyekuwa amefikia, aliweza kijitanua hadi kufanikiwa kufanya kazi na wasanii wakubwa wa Nigeria, nchi inayoongoza kwa kufanya vizuri katika filamu.

Licha ya kuanzisha tasnia hiyo pia amekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha filamu za Tanzania zinakuwa na kiwango cha kimataifa kiasi cha kuinua soko la filamu hizo na kuitanganaza nchi yetu.

Filamu za Dar to Lagos, Devil’s Kingdom, She is my sister, Cross my sin na Hero of the Church, ni kazi zilizofungua milango ya Kanumba nje ya nchi; kazi zote hizo amezifanya kwa ushirikiano na wasanii kutoka Nigeria.

Mpaka anakumbwa na umauti Kanumba ameshacheza takribani filamu 40 ya kwanza ikiwa ni Johari aliyoifanya akiwa bado muigizaji wa kundi la Kaole na filamu ya mwisho inaitwa Ndoa Yangu ambayo bado ilikuwa ikifanyiwa matangazo kabla ya kuingia sokoni.

Kanumba aliweza kujizoelea umaarufu kwa watu wa rika zote kutokana na filamu zake kulenga kukonga nyoyo za wapenzi wa filamu wa makundi yote kwani aliweza kugusa kila nyanja ya maisha.

Mafanikio yake ni mfano wa kuigwa kwa vijana wote kwani amepitia mengi ambayo yangeweza kumkatisha tamaa, historia yake ilianzia nyumbani kwao Shinyanga ambapo Kanumba aliwahi kukaririwa akisema hakupata malezi stahiki kutoka kwa baba yake.

Maisha ya kutopata mapenzi ya baba ndiyo yaliyokuwa chachu kwa Kanumba kwani alipoingia kwenye kundi la Kaole, uwezo wake ulianza kudhihirika.


Hili ni kaburi la Josina Machel, mke wa kwanza wa Rais wa Msumbiji Hayati Samora Machel



Hakuishia hapo, alidhubutu kuingia kwenye fani ya filamu, kwa miaka kadhaa akiwa chini ya kampuni ya utengenezaji filamu ya Game First Quality, lakini hatua kwa hatua na kwa kutumia mafanikio yake, Kanumba aliweza kuwa na kampuni yake binafsi ya utengenezaji filamu ya ‘The Great Film.’

Ni kwa mafanikio na heshima aliyojijengea, Kanumba aliweza kuiwakilisha nchi akiwa Balozi wa Shirika la Kimataifa la Chakula Duniani la Oxfam hapa nchini, Kanumba pia aliweza kutumiwa na kampuni mbalimbali kwa ajili ya matangazo na pia kama balozi wao, hadi anafariki alikuwa pia balozi wa kampuni ya Startimes.

Aidha Kanumba amekuwa mcheza filamu pekee toka Tanzania kupata mualiko wa kutembelea jumba la Big Brother Africa pamoja na kualikwa katika onyesho la utoaji tuzo za filamu nchini Ghana maarufu kama Film of Africa.

Kanumba alizaliwa mwaka 1984 mkoani Shinyanga ambapo ndiko alikojipatia elimu yake ya msingi na sekondari kabla ya kuhamia jijiji Dar es Salaam kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Jitegemee na baadaye kujiingiza moja kwa moja kwenye sanaa.

Aprili 7 mwaka huu alifariki akiwa nyumbani kwake kufuatia kile kinachodaiwa ugomvi kati yake na anayedaiwa kuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael, ‘Lulu’.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa madaktari, Kanumba alifariki baada ya ubongo wake kutikiswa, hivyo kushindwa kupumua na hatimaye kufariki muda mfupi baadaye.

Amefariki akiwa na ndoto nyingi, kubwa ni kuwa mbunge ambapo aliwahi kukaririwa akisema angegombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.

Friday, April 13, 2012

Kanumba alijitabiria kifo filamu yake ya mwisho


Mpiga picha na mhariri wa filamu za Steven Kanumba, Zakayo Magulu amesema kifo cha msanii huyo kinafafana na hadithi ya filamu yake ya mwisho aliyoigiza, inayoitwa Price of Love ambayo bado haijatolewa.

Mugulu alisema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican, Dar es Salaam.

Alisema filamu hiyo ambayo Kanumba aliibadilisha jina na kuiita Power and Love inaeleza jinsi msanii huyo alivyotoa figo na baadaye kufa baada ya kusukumwa na mpenzi wake katika filamu hiyo ambaye alikuwa ni Irene Paul.

Akiielezea filamu hiyo ambayo bado haijatoka licha ya kuwa imeshakamilika, alisema Kanumba aliigiza kama mtu maskini aliyempenda msichana ambaye alikuwa na uhusiano na mwanamume tajiri.

“Katika filamu ile Kanumba alitoa figo yake moja baada ya huyo msichana (mpenzi wake) kuugua na kutakiwa kuwekewa figo nyingine. Alipotoa Figo uliibuka ugomvi baina yake na mpenzi wake ambaye alimsukuma na Kanumba alianguka na kuumia. Baada ya tukio hilo, alikimbizwa hospitali na baada ya muda mfupi alifariki dunia.”


Alisema msanii, Idrisa Makupa maarufu kama Kupa ndiye aliyeona kifo cha Kanumba katika filamu hiyo na pia hata baada ya kifo chake, ndiye mtu wa mwisho kuuona mwili wa Kanumba ukiingizwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuufunika…. “Ni mambo ya ajabu.”

Alisema hata daktari aliyemfanyia operesheni Kanumba katika filamu hiyo ndiye huyo huyo aliyefika nyumbani kwa Kanumba kumpatia huduma baada ya kuanguka.

Alisema tukio la kifo cha Kanumba katika filamu hiyo iliyoandikwa na Ali Yakuti halikuwepo ila liliongezwa na msanii huyo mwenyewe… “Filamu hiyo ilikuwa na matukio (scene) 84 lakini, yalibadilishwa matukio 40 likiwemo la kifo chake.”

Mchaguaji wa maeneo ya kupigia picha za filamu za Kanumba, Rahim Khatib maarufu kama Kiuno alisema katika filamu hiyo ya mwisho ya msanii huyo alipendekeza picha zipigwe katika maeneo yenye giza na mwanga halisi (usio wa taa).



Mtoto wa Kanumba

Katika hatua nyingine imebainika kuwa Kanumba (28), ameacha mtoto mmoja wa kiume.

Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu, mama mzazi wa msanii huyo, Flora Mtegoa alisema: “Kama kuna aliyezaa na mwanangu ajitokeze na familia itamsikiliza.”

Taarifa za Kanumba kuacha mtoto zilikuwa gumzo jana nyumbani kwa marehemu ambako baadhi ya ndugu walioonekana kufurahia na wengine kupinga wakidai kuwa mtoto huyo na marehemu.

“Leteni hilo gazeti…, hao wanaojitokeza waje tu mimi ndiyo nafurahi waache wawalete wajukuu zangu,”alisema Mtegoa baada ya kuelezwa kuwa taarifa hizo ziliwahi pia kuripotiwa na moja ya magazeti nchini (siyo Mwananchi).

Hata hivyo, baada ya mama huyo kutoa kauli hiyo dada yake marehemu Kanumba, Abella Kajumulo alisema mtoto huyo si wa mdogo wake kwa sababu katika uhai wake Kanumba hakuwahi kuieleza familia yake kama ana mtoto wala mke.

“Mbona huyo mwanamke hakujitokeza wakati wa msiba wa Kanumba aje kujitokeza hivi sasa? Niliwahi kumwuliza (Kanumba) juu ya ndoa yake na kama ana mtoto alikataa kabisa akasema hana mtoto wala mke,” alisema Kajumulo.

Wakati ndugu hao wakibishana kuhusu habari hizo, aliibuka kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Patrick Kamwele na kuwaeleza kuwa mtoto huyo ni wa Kanumba na kwamba anamfahamu vizuri msichana huyo.

Kamwele ambaye ni raia wa Kenya aliingia mkataba na kampuni ya Kanumba The Great tangu mwaka 2009 na katika mazungumzo yake na ndugu hao aliwaeleza kuwa atakuwa shahidi iwapo atahitajika kufanya hivyo.

Alisema mara ya kwanza kumwona msichana huyo ilikuwa Septemba 2009, baada ya kufika nyumba kwa Kanumba kwa ajili ya kufanya mazungumzo kabla ya kuingia naye mkataba.

“Baada ya kukaa nyumbani kwa Kanumba kwa muda wa wiki mbili huyo msichana, alianza kuumwa na Kanumba alimpeleka hospitali na alibainika kuwa ni mjamzito,” alisema Kamwele.



Alifafanua kwamba baada ya msichana huyo kusema kuwa mimba hiyo ni ya Kanumba, yeye pamoja na baadhi ya wasanii wa bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia, waliitwa katika kikao na msanii huyo.

“Katika kikao kile tulimhoji msichana huyo na alisema mimba ni ya Kanumba, ila baadaye msichana huyo aliondoka ingawa mimi sijui kama alifukuzwa au aliondoka mwenyewe,” alisema.

Alisema kilichoendelea baada ya hapo hakukijua mpaka alipokuja kuiona habari hiyo katika gazeti jana.

Mmoja wa wasanii wa filamu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema anamfahamu msichana huyo na kwamba alikuwa mfanyakazi wa ndani wa Kanumba.

Msanii huyo alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na Kamwele mbele ya ndugu zake Kanumba, huku akitizama picha ya msichana huyo katika gazeti na alisema: “Namfahamu huyu msichana alikuwa msichana wa kazi wa Kanumba.”

Kamwele aliwataka ndugu wa marehemu Kanumba kulichukulia suala hilo kwa umakini kwa kuwa hawawafahamu watu wote waliokuwa wa karibu wa msanii huyo.

“Mimi nimekaa na marehemu Kanumba kwa muda mrefu na ninawajua waliokuwa watu wake wa karibu akiwemo huyo msichana, nawashauri kulipa uzito suala hili,” alisisitiza Kamwele.


Familia yatoa utaratibu

Katika hatua nyingine, mama wa marehemu Kanumba amewaomba radhi wananchi wote kwa kitendo cha kukatisha ratiba za kuuaga mwili wa msanii huyo juzi katika Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Mutegoa alisema ratiba hiyo ilikatishwa kutokana na watu kuwa wengi na kusababisha kuibuka kwa vurugu… “Sikutegemea kama watu wangekuwa wengi kiasi kile mpaka wengine kufikia hatua ya kupoteza fahamu… nawaomba radhi wote waliofika, pamoja na hayo wingi ule wa watu ulinipa faraja kubwa. Wameonyesha upendo wa hali ya juu.”
Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Sinza Vatican huku taarifa za awali zikieleza kuwa kifo chake kilitokana na ugomvi na aliyekuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.