Thursday, May 17, 2012

Kwa kheri Mafisango


                                      
Marehemu akiwa nyumbani kwake enzi za uhai wake

Waandishi Wetu
Simanzi, huzuni na vilio viliwatawala wanamichezo nchini baada ya kupata taarifa za kifo cha kiungo wa kimataifa wa Rwanda na Simba, Patrick Mutesa Mafisango (32) aliyefariki dunia jana alfajiri kwa ajali ya gari.
Mafisango anatarajiwa kuagwa leo kwenye Uwanja TCC Sigara Chang'ombe jijini Dar es Salaam kabla ya kesho kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao DR Congo kwa mazishi.
Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema taratibu za kuuaga mwili wa marehemu zitaanza saa nne asubuhi mpaka saa 10 jioni.
Mafisango alipata mauti hayo eneo la Veta Chang'ombe usiku wa kumkia jana saa 8.45 alipokuwa akiendesha gari akitokea Maisha Club akiwa na wenzake wanne na alipofika maeneo ya Veta wakati akijaribu kumkwepa mwendesha baiskeli ya miguu mitatu 'Guta' gari lilimshinda na kugonga mti uliosababisha gari yake kuingia mtaroni na mauti kumkuta hapo hapo.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo mtoto wa dada yake Orly Ilemba (24) aliyekuwamo katika gari hilo alisema jana wakati wanavuka mataa ya Veta, marehemu alikuwa katika mwendo kasi mara mbele akakutana na Guta na katika jitihada za kulikwepa akagonga mti na gari kupinduka na kutumbukia mtaroni na mauti kumkuta hapo hapo.
"Tulitoka salama Maisha Club tunarudi nyumbani marehemu alikuwa akiendesha gari katika mwendo wa kasi, tulipovuka mataa ya Veta wakati akiwa 'spidi' tuliona guta kwa mbele yetu pamoja na pikipiki sasa wakati marehemu anakwepa kwa bahati mbaya aligonga mti na gari ikadumbukia ndani ya mtaro huku nikishuhudia kichwa cha ndugu yangu kikigeukia chini kwenye sehemu ya breki na miguu kuja juu kumbe tayari alishafariki......ndipo tukaanza taratibu za kumkimbiza hospitali," alisema Ilemba.
Aliongeza kuwa,"ndani ya gari hiyo aina ya Gx100 tulikuwa watu jumla ya watano mimi, Gaspar Karemera, Bozy na mwanamke mmoja ambaye yeye hatukumfahamu jina lake mara moja akiwa amekaa mbele na marehemu ambaye mpaka sasa bado yupo hospitali akiendelea na matibabu baada ya kuumia sana maeneo ya kichwani,"alisema Ilemba.


Mashabiki wa soka waliofika Kituo cha Polisi cha Chang'ombe wakiangalia gari la marehemu lililopelekwa kituoni hapo janakifo cha Mafisango




Akithibitisha kifo cha mchezaji huyo, Mkuu wa Trafiki katika mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Prackson Lugazia alisema  ajali hiyo ilitokea wakati Mafisango aliyekuwa akiendesha gari aina ya GX 100 akitoka Maisha Club akiwa na familia yake akijaribu kumkwepa mwendesha Guta.
Alisema hali hiyo ilisababisha gari hilo kuacha njia na kuingia mtaroni na kugonga miti mitatu kisha kugeuka na kuangalia lilikokuwa likitoka na baadaye kupinduka.
"Baada ya kupata taarifa za ajali hiyo majira ya saa 10 asubuhi tulifika eneo la tukio haraka iwezekanavyo, lakini hatukukuta mtu yeyote zaidi ya gari lililokuwa limepinduka,"alisema Lugazia.
Alisema,"kufuatia hali hiyo ndipo tulipoanza taratibu za kumtafuta marehemu na tulianzia hospitali ya Amana,  tulikwenda hospitali ya Mwananyamala na baadaye Muhimbili ambako tuliukuta mwili wake pamoja mwanamke mmoja ambaye alikuwa na majeraha mbalimbali sehemu za mwili wake," alisema Lugazia.
Akizungumza jana alfajiri jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema,"ni kweli Mafisango hatunaye tena, kwa sasa siwezi kuzungumza chochote huyu ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda, ndiyo nafanya mawasiliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na lile la Rwanda (FERWAFA) kuangalia namna ya kuusafirisha mwili wake."
Mafisango amefariki akiwa amemaliza mkataba wake na Simba na alitarajiwa kusaini mkataba mpya juzi na leo alitarajiwa kwenda Rwanda tayari kujiunga na kikosi cha timu hiyo 'Amavubi' kinachojiandaa kwa ajili ya mechi za mchujo za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2014, zitakazochezwa mwezi ujao.

Baadhi ya wasanii na wachezaji waliofika Hospitali ya Muhimbili kupata uhakika wa kifo cha Mafisango
Kocha wa timu ya Taifa ya Rwanda, Sredojevich Millutin 'Micho' akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu alisema,"nimeshtuka sana, siamini Mafisango amefariki,  niliongea naye jana (juzi) na nimemtumia tiketi ya ndege kwa ajili ya kujiunga na timu na nilikuwa namsisitiza asichelewe na alinihakikishia Ijumaa (leo) atakuja."
"Ukiniambia amefariki sikuelewi hapa nilipo nimechanganyikiwa, kuna vikao vinaendelea (jana), nitakupigia baadaye,"alisema Micho huku sauti yake ikionekana kuwa na majonzi.
Wakati huohuo; Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea leo (jana) alfajiri kwa ajali ya gari Dar es Salaam.
TFF ilisema msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.
Kifo chake ni pigo kubwa sio tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali Ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto za Mafisango zilikuwa dhahiri uwanjani.

BOBAN
Rafiki mkubwa wa Mafisango kiungo Haruna Moshi 'Boban' alikuwa kwenye majonzi makubwa huku machozi yakimtoka bila kuzungumza lolote.
Wakizungumzia ukaribu wa mchezaji huyo na marehemu baadhi ya wachezaji wa Simba walidai Boban ndiye alikuwa rafiki mkubwa wa Mafisango na walikuwa kila mara wakiongozana pamoja katika starehe na hata wakiwa kambini.

Boban

"Boban ndio alikuwa mtu wa kwanza kusambaza habari za kifo cha Mafisango kwetu na hata aliposikia taarifa hizo alichofanya alikwenda moja kwa moja Muhimbili kwenye chumba cha maiti na kuomba kuonyeshwa mwili wa marehemu na baada ya hapo hakuzungumza lolote mpaka hapa mnavyomuona,"alisema Juma Jabu.
Mafisango alijiunga na Simba akitokea Azam Fc, mwaka jana alizaliwa Machi 7, mwaka 1987, nchini Rwanda na alikuwa akiichezea timu ya Taifa ya nchi hiyo kabla ya kusimamishwa kwa muda mrefu kutokana na utovu wa nidhamu na amerudishwa kundini na kocha Micho, lakini hata hivyo hajaweza kuitumikia timu hiyo ya Taifa lake.
Mchezaji huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika timu ya Simba msimu huu uliomalizika hivi juzi na kung'aa zaidi katika Ligi hiyo kwa kupachika mabao na kutoa pasi za mwisho, ambapo Mechi ya mwisho ya Mafisango ilikuwa ni kati ya Simba dhidi ya Al Ahly Shandy Jumapili katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penati 9-8, kufuatia sare ya jumla ya mabao 3-3.
Wakati mechi ya kwanza kati ya Simba na Wasudan hao iliyochezwa hapa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Mafisango aliifungia timu yake bao moja kati ya matatu yaliyoiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo huo.

Monday, May 14, 2012

Baada ya kazi kubwa sasa ni kusherehekea kwa kwenda mbeleee!

 Wachzaji wa Manchester City wakishangilia baada ya kukabidhiwa Kombe la Ligi Kuu England
Wachzaji wa Manchester City wakipita mtaani jana Jumapili usiku baada ya mechi yao ya fainali iliyopelekea kupata ushindi wa Ligi Kuu England  baada ya kuifunga Queens Park Rangers.



Baada ya miaka 50 ya Uhuru

Wanafunzi wa darasa la sita wa Shule ya Msingi, Selous iliyopo wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma wakiendelea na masomo shuleni hapo. Picha na Mpigapicha Maalum       

Umewahi kuiona hii??!! Hakunaga!

Ndege aina ya Q400 NextGen kutoka Kampuni ya Bombardier ya Canada ikiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa   Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam jana, ikitafuta wateja wa kuikodisha au kuinunua. 

Tamwa yawapa somo wakuu wapya wa Wilaya


Shakila Nyerere
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(Tamwa), kimewataka Wakuu wa Wilaya walioteuliwa kuwa makini katika ufuatiliaji wa Watendaji wa Halmashauri katika shule za kata kuepukanana mimba na kufeli kwa wanafunzi wa kike nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Tamwa, Ananilea Nkya alisema wakuu wote wa Wilaya walioteuliwa wawe ni mifano kwa viongozi wengine walioko madarakani kufuatilia majukumu yanayozikabili jamii.
Alisema kwa takwimu walizozifanya kwa kushirikiana na wanahabari kupata takwimu hizo zilizohusu shule za kata katika mikoa 20 Bara na Visiwani kwa kila Wilaya moja katika Kata mbalimbali kwa shule 7 hadi 10 walibaini kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wanoacha shule au kufeli ni wanafunzi wa kike.
Nkya alisema mazingira ya shule zilikojengwa ni hatari kutokana na kukosekana kwa mahitaji muhimu kwa wanafunzi kama vile Maji, miundombinu mibovu ya barabara  ni sababu mojawapo ya kuwapa vishawishi wanafunzi wa kike kuishi wakidanganyika kwa kupitia udhaifu wa maisha waliyonayo.

Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA), Ananilea Nkya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaamjana, wakati akitoa taarifa ya utafiti wa vyanzo vya ongezeko la wanafuzi kufeli mitihani ya Kitaifa.

“Wakati mwingine wanafunzi wa kike hulazimika kuishi kwa Walimu wa kiume na kuwa na mahusiano ya kimapenzi kinyume na maadili na sheria na wengine hujikuta wakiishi kwa vijana walioko mitaani kwa kutaka kujikimu kimaisha na kupata mahitaji ya kujikidhi wanapokuwa shuleni, hiyo yote ni hali za shule za kata kuwa na mapungufumengi,” alisema Nkya.
Nkya aliongeza kwa kusema mazingira ya shule za kata zilizoko mikoani na wilayani kwa upande wa walimu ni matatizo makubwa sana maana inafikiwa wakati mwingine shule yenye kidato cha kwanza hadi cha sita kuwa na walimu watatu ikiwa mwalimu wa somo la sayansi ni mmoja na kwingineko hakuna kabisa mwalimu wa somo hilo  la sayansi.
Walimu walioko wanaofundisha somo la sayansi ni mwalimu wa somo la sanaa ndiye anayefundisha sayansi kataka shule hizo.
“Ili taaluma ikue nchini hapa kinachotakiwa ni kuboresha mahitaji muhimu ikiwemo miundombinu kwa walimu na wanafunzi ikiwa ni pamoja na uwajibikaji wa viongozi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kufuatilia watendaji katika idara zao.”
Aliongeza kwa kusema wanafunzi wa kike hufeli na kukatiza masomo kwa kubeba mimba shuleni ni pamoja na kukosekana kwa walimu ambao kwa asilimia 80 wamekuwa wakishindwa kuwasili katika vituo vya kazi wanavyokuwa wamepangiwa wakikumbana na mazingira magumu kwa mara ya kwanza. 


Pale ubora unapoonekana


Mkurugenzi wa Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma, akimkabidhi Laptop Zaitun Kaijage (kulia, amabaye ni mmoja kati ya washindi wa tuzo za masomo ya fani ya teknolojia ya mawasiliano katika mamlaka hiyo, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam juzi.

Sunday, May 13, 2012

Magari ya kifahari bado yamtoa udenda Cristiano Ronaldo, ayajaza manane uani kwake


Kuwa mwanasoka ghali duniani kunafanya pesa lisiwe tatizo lako la msingi. Ni kama ilivyo kwa staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo. Tajiri huyu kijana ananunua chochote anachojisikia kwa sasa.

                              

Kwa mujibu wa mkataba wake, Ronaldo, analipwa kiasi cha Euro 12 milioni kwa mwaka na Real Madrid. Hii ni achilia mbali mikataba mbalimbali ya kibiashara ambayo inamwingizia mabilioni ya pesa yanayomfanya awe miongoni mwa wanasoka wanaoingiza pesa nyingi zaidi duniani kwa sasa.
Hata hivyo, ugonjwa wake wa kupenda magari ya kifahari umemfanya Ronaldo ajaze magari mengi ya bei mbaya uani kwake. Amekuwa akiyatumia mara kwenda mazoezini na katika matembezi binafsi.
Yafuatayo ni magari manane ya kifahari ambayo Ronaldo ameyajaza uani na ambayo huwa anayaendesha mara kwa mara.
                              

Bugatti Veyron
Hili ndilo gari kipenzi la Ronaldo. Bugatti Veyron ni ghali zaidi na lina mwendo wa kasi zaidi duniani. Mwendo Kasi wake wa juu huwa unafikia kilomita 407 kwa saa na linaweza kumpita dereva wa formula one anayeendesha kwa kilomita 360. Staa wa Cameroon, Samuel Eto’o ni mchezaji mwingine anayemiliki gari la aina hiyo.
Bugatti huwa linauzwa kwa oda maalumu kutoka kiwandani na mhusika analazimika kulisubiri kwa kipindi fulani wakati likitengenezwa. Linauzwa kiasi cha dola 1.2 milioni na hivyo kulifanya kuwa gari ghali zaidi duniani kwa sasa.
                              

Rolls-Royce Phantom Drophead Coupe
Rolls-Royce ni gari linaloheshimika zaidi Uingereza. Gari hili linamilikiwa na watu matajiri. Kuna watu wachache sana wanaomiliki gari hili Uingereza. Lina thamani ya dola 443,000 za Marekani.
Kinachoshangaza ni kwamba nyuma ya gari hili unaweza kufungua katika sehemu ya mizigo na kupata eneo la kukaa kufanya pikiniki.
Ukifungua kuna meza inajipandisha na kuna sehemu za kuwekea vinywaji mbalimbali.
                                

Porsche Cayenne Diesel
Gari hili limetoka Mei mwaka huu na Ronaldo alilisubiri kwa muda mrefu kulinunua moja kwa moja. Lina injini yenye nguvu na kasi yake ni kilomita 218 kwa saa. Kwa suala la mafuta, gari hili lina uwezo wa kutumia lita 10 kwa mwendo wa kilomita 100. Hili ni moja kati ya magari ya bei rahisi ambayo Ronaldo anayo. Lilimgharimu kiasi cha Euro 49,000.

                               

BMW M6
Duniani kote gari hili linatambulika kuwa ndoto ya kila mtu anayetaka kuendesha ‘Sports Car’. Kwa Ronaldo, hili ndilo gari linalomfaa zaidi kwa sababu yeye ni mwanamichezo wa hali ya juu.
Ingawa bei yake ni dola 100,000, Ronaldo hakuona shida kulinunua na kulitupia uani kwake. Ni moja kati ya magari anayotumia sana.

                                  

Porsche 911
Ni moja kati ya magari ya kifahari duniani kote. Lilimgharimu Ronaldo kiasi cha euro 201, 682 kuliweka uani kwake. Ni moja kati ya magari anayoyatumia mara kwa mara pia akienda katika starehe zake.

                                 

Bentley Continental GT
Hili ni moja kati ya magari yenye nguvu ambayo kampuni ya Bentley imewahi kuyatengeneza. Gari hili pia lina kasi kubwa huku likitumia mwendo wa kilomita 320 kwa saa. Kutokana na mapenzi yake kwa gari hili, Ronaldo alilazimika kutumia kiasi cha dola 375,000 za Marekani kwa ajili ya kulinunua na kuliweka uani kwake. Ni gari la kifahari ambalo ni ndoto ya wengi.

                                   

                                 

Ferrari F430
Gari hili la siti za watu wawili tu. Kwa sasa ndiyo dili na   Ronaldo bado ana mapenzi nalo ya dhati.
Kuna watu wanasema lishastaafishwa lakini Ronaldo hakutaka kuliuza na mpaka leo amekuwa akilitumia mara nyingi. Alitumia kitita cha dola 188,000 za Marekani kulinunua.





Audi R8
Moja kati ya magari yenye kasi duniani. Gari hili lina uwezo wa kukimbia kwa kilomita 316 kwa saa. Kwa kuliweka uwani kwake kukamilisha idadi ya magari manane ya kifahari aliyonayo, Ronaldo alilazimika kujikamua kiasi cha dola za Marekani 109,000 ili kulinunua.

Tajiri anayeishi na Papa nyumbani kwake


                                         

Bill Gates anashika nafasi ya pili katika orodha ya watu matajiri duniani. Hiyo ni kutokana na biashara yake ya kompyuta na vipuli vyake.
Anayeshika namba moja kwa utajiri duniani ni raia wa Mexico, Carlos Slim.
Gates ambaye ni Mmarekani, jina lake ni William Henry "Bill" Gates III. Alizaliwa Oktoba 28, 1955 mjini Washington, Marekani.
Ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Microsoft ambayo aliianzisha na tajiri mwenzake, Paul Allen, mwaka 1975.
Microsoft ni kampuni yenye makao yake makuu huko  Redmond, Washington, Marekani na inajishughulisha na utengenezaji na usambazaji wa kompyuta na vipuli vyake duniani.
Pamoja na utajiri wake, Gates pia ni mdau mkubwa wa michezo akijihusisha na soka, gofu na tenisi.
Kupitia mfuko wake wa Bill & Belinda Foundation anashirikiana na klabu ya Barcelona ya Hispania katika kuendesha kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa polio duniani.
Kutokana na shughuli zake mbalimbali, Bill Gates ana utajiri wa Dola 61.3 bilioni (Sh5 trilioni za Kenya). Ni kati ya mabilionea wachache duniani.
Ana nyumba sehemu mbalimbali duniani lakini anaishi katika nyumba ya aina yake iliyoko katika eneo la Medina jijini Washington na liko karibu kabisa na ziwa.



                                      




Nyumba hiyo yenye vyumba vinane vya kulala,  ina thamani ya Dola 125 milioni (Sh10.2 bilioni za Kenya) na imepakana na Ziwa Washington.
James Cutler ndiye alibuni nyumba hiyo kwa kutumia mfumo wa kompyuta na aliijenga kwa kupasua mlima ulio karibu na Ziwa Washington.

                                    

Pia amejenga bwawa la samaki chini ya nyumba na limefunikwa na vioo madhubuti. Miongoni mwa samaki waliomo kwenye bwawa hilo ni pamoja na papa ambao hupita na kuonekana katika sebule ya Gates.
                                    

Gates pia ana bwawa la kuogelea kwenye nyumba yake. Bwawa hilo limefungwa vyombo vya muziki na pale mtu anapoogelea basi huburudika na muziki laini pia.
Pia mtu akiingia kwenye chumba chochote cha nyumba hiyo, taa huwaka moja kwa moja bila ya kuwashwa na mtu.
Gates ana magari kadhaa yakiwamo 1988 Porsche 959 Coupe,  1998 Lincoln Continental, 1999 Porsche 911 Convertible, Ford Focus na Limousine Chevrolet Corvette.

                                    

                                    

Pia tajiri huyo anamiliki ndege nne za kusafiria na pia ana helikopta ya kuzungukia nchini Marekani.
Miongoni mwa ndege anazomiliki Gates ni pamoja na Bombardier BD-700 Global Express ambayo bei yake ni karibu Dola 45.5 milioni.
Gates anamiliki boti yenye jina la Goygpus yenye thamani ya Dola 200 milioni .




 Tajiri huyo alimwoa Melinda French, Januari 1, 1994. Ana watoto wawili wa kike,  Jennifer Katharine Gates (1996) na Phoebe Adele (2002) na mmoja wa kiume Rory John (1999).

Nani zaidi?

Kweli kaka Kanye ameopoa mtoto wa ukweli, lakini kwangu binafsi ninapata tabu nikiangalia kati ya Kim na Amber nani mkali. Hebu angalia mwenyewe.....