Lakshmi Mittal: Ana basi la ajabu
Tatiri wa India, Lakshmi Mittal ni kati ya wamiliki wa klabu ya soka ya Queens Park Rangers iliyopanda daraja msimu huu kwenye Ligi Kuu England.
Mwanahisa mkubwa mwingine kwenye klabu hiyo ni Bernie Ecclestone, ambaye ni rafiki mkubwa wa Mittal.
Ecclestone anafahamika kutokana na kumiliki haki za mbio za magari za Formula One.
Mittal, ambaye ni raia wa India, anahesabiwa kama mtu tajiri zaidi barani Asia na Uingereza.
Anashika nafasi ya sita miongoni mwa mabilionea duniani, utajiri wake ukikadiriwa kuwa Dola 31 bilioni (Sh. 2.8 trilioni za Kenya) ukitokana zaidi na mauzo ya bidhaa za chuma.
Mittal ana majumba, magari madogo, ndege, basi, helikopta na boti.
Mittal ana basi lililotengenezwa na kampuni ya kutengeneza mabasi ya Featherlite Luxury.
Basi hilo ni la kipekee likiwa na vitu vya anasa ndani yake na thamani yake ni Dola 2.5 milioni (Sh. 229 milioni za Kenya)

Lina chumba cha kulala, bafu ya kuogea, chumba cha kulia chakula, sebule, jiko na saluni.
Mittal pia ana majumba sehemu mbalimbali duniani ingawa anashikilia rekodi ya kuwa na nyumba ya bei ghali zaidi duniani.
Anaishi katika jumba la thamani ya pauni 250 milioni (Sh. 37 bilioni za Kenya) katika mtaa wa Kensington Palace Gardens, jijini London, Uingereza. Aliinunua kutoka kwa Ecclestone.
Nyumba hiyo ina vyumba 12 vya kulala, bafu, ukumbi mkubwa, bwawa la kuogelea lililotengenezwa kwa madini ya dhahabu na sehemu ya kuegeshea magari 20.
Ukiachia nyumba hiyo anayoishi, pia ana nyumba mbili zaidi katika jiji la London.
Pia ana jumba la thamani ya pauni 15 milioni (Sh. 2.2 bilioni za Kenya) huko Scotland.
Pia nyumba nyingine katika mtaa wa Aurangzeb katika jiji la Delhi, nchini India.
Mittal pia ana nyumba nyingine katika nchi za Indonesia na Trinidad.
Ana magari mengi tu lakini yanayojulikana ni yale ya Ferrari, Range Rover, Mercedes Benz, Jaguar na mengineyo.
Pia ana boti kubwa aliyoipa jina la Amevi na pia ana ndege yake binafsi na helikopta.
Mittal, ambaye amezaliwa Juni 15, 1950, anamiliki kampuni ya ArcelorMittal, ambayo inaongoza duniani kwa kutengeneza vifaa vya bidhaa ya chuma.























