
Kwa utamaduni wa karibu jamii zote duniani, ni jambo ambalo haliwezi kukubalika, lakini baba mmoja raia wa Ujerumani wiki hii ameshtakiwa kwa kosa la kumbaka binti yake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 34 na kumzalisha watoto watatu wa kiume.
Adolf Bergbaue (69), ambaye alikuwa akiishi na familia yake huko Bavaria, ameshtakiwa kwa makosa zaidi ya 497, likiwepo la ubakaji katika Mahakama ya Nuremberg baada ya kubainika kutenda kosa hilo.
Katika kesi hiyo, imeelezwa kuwa binti huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 46, aliamua kumweleza mke wa daktari kuhusu matatizo ya mmoja wa watoto wake na hapo ndipo siri ilipofichuka.
Bergbaue anadaiwa kutumia viboko kila wakati alipokuwa akihitaji kufanya mapenzi na binti yake huyo. Hata hivyo kwa mujibu wa binti huyo, alianza kubakwa na baba yake kwa mara ya kwanza alipokuwa na umri wa miaka 12. Anaeleza kuwa alikuwa akibakwa mara kadhaa kwa wiki.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Gabriels Gorsolke, mzee huyo alikuwa akiishi na mkewe miaka yote alipokuwa akitenda unyama huo. Watoto wote watatu walizaliwa akiwa na familia yake yote, mkewe, bintiye na mtoto wake mwingine.
Gorsolke alisema Bergbaue alikuwa ameajiriwa wakati binti yake akiwa na umri mdogo, amekuwa hana kazi kwa kipindi kirefu.
Anaeleza kuwa kwa kipindi hicho ndipo aliamua kumfungia nyumbani na kumchunga asitoke wala kuzungumza na watu huku akiendeleza unyama wa ubakaji.
Baba huyo alikuwa akiongozana na bintiye alipohitaji kutoka na kamwe hakutaka awasiliane wala kuwa na mahusiano na mwanaume mwingine.

Gorsolke alisema kuwa mama wa binti huyo alikuwa akifahamu kitendo cha mumewe, lakini hakuweza kushtakiwa kwani mahakama ilieleza kuwa huenda mwanamke huyo alikuwa na mapungufu ya amri katika familia yake.
"Hivi sasa mama wa binti huyo pamoja na mwanaye wanaishi katika mji fulani ambao mahakama haiwezi kuutaja," alisema Gabriels.
Kwa mujibu wa binti huyo, baba yake alikuwa akimbaka katika kitanda anachotumia na mama yake na wakati mwingine katika chumba chake cha kulala na wakati mwingine alimlazimisha kuendesha gari na kwenda sehemu ya mbali , kisha kumbaka ndani ya gari.
"Sijawahi kutenda kitendo hicho," alisema Bergbaue ambaye anadaiwa kumshikia kisu wakati mwingine alipobaini kuwa binti yake hakuhitaji kutenda tendo hilo pamoja naye.
Binti huyo alizalishwa na baba yake watoto watatu ambao wote walikuwa na matatizo ya akili (mtindio wa ubongo) na mmoja wao alifariki akiwa mdogo miaka kadhaa iliyopita. Mtoto wa pili ni mkubwa na anaishi mbali na mama yake.

Mtoto wa tatu alizaliwa mwaka huu na kufariki hivi karibuni. Kifo chake chenye utata ndicho kiliwazindua madaktari na kuamua kufanya uchunguzi wa kina na kugundua sakata hilo.
Madaktari waliamua kufanya uchunguzi wa DNA, ndipo walipogundua kuwa baba wa watoto hao ni baba mzazi wa mama wa watoto hao.
Bergbaue alikamatwa mapema Machi na amekuwa akishikiliwa hadi wiki hii alipoburutwa kortini.
"Hata hivyo alikubali kuwa na mahusiano na binti yake, lakini alisema kuwa hakuwa akimbaka bali walikuwa na makubaliano," alisema Gabriels.
Kumekuwa na matukio kadhaa ya kutisha katika bara la Ulaya kwa miaka kadhaa sasa. Miaka ya karibuni raia wa Australia, Josef Fritzl alimfungia binti yake katika gereza kwa miaka 24.
Fritzl alikuwa akimbaka kila wakati na aliweza kumzalisha watoto kadhaa. Baba huyo alishtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 2009.


























