Tuesday, November 29, 2011

Mvua yaleta maafa Arusha


Mvua kubwa ya upepo iliyonyesha usiku wa kuamkia jana imesababisha mafuriko makubwa, maporomoko ya mawe kwenye Mto Kirurumo uliopo mpakani mwa Wilaya mbili za Karatu na Monduli, mkoani Arusha.

Kutokana na mvua hizo mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya kuzolewa na maji kilomita nne ambako maiti yake iliokotwa.

Mbali na kifo na majeruhi huyo, mvua hizo pia zimewaacha mamia ya wakazi wa maeneo hayo bila makazi kutokana na nyumba kadhaa kusombwa na mafuriko hayo.



Watalii, wagonjwa wakwama

Idadi kubwa ya watalii, ambao jana walitarajia kuendelea na safari kwenda Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na wengine kurejea Arusha walikwama katika barabara hiyo na kubaki wamekaa kwenye magari.

Mmoja wa watalii hayo, Johnson Taylor kutoka Uingereza alisema alikuwa ametarajia kuwahi Arusha jana ili kusafiri kurejea nchini kwao, lakini amekwama.

“nimefika hapa tangu saa 12:00 asubuhi, lakini tumeshindwa kupita kutokana na barabara kuharibika…hii ni tatizo kubwa sasa tunafanya mawasiliano kuona kama tiketi za safari zitabadilishwa”alisema Taylor.



Wananchi waombwa

kuhama mabondeni


Mbunge wa jimbo la Karatu, Mchungaji Israel Natse na mkuu wa wilaya hiyo, Methew Sadoyeka walitoa wito kwa wananchi ambao wanaishi katika maeneo ya mabonde kuhama sasa kwani taarifa za utabiri wa hali ya hewa zimesema kutakuwa na mvua nyingi hadi Desemba.


JWTZ waenda kufungua barabara

Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), kutoka Makao Makuu ya Brigedi ya Mbuni wilayani Monduli, jana walifika eneo la tukio Mto wa Mbu kusaidia kazi ya kufungua barabara ya Karatu-Arusha ili kuruhusu magari kupita.


Rais Bashir amtimua balozi wa Kenya


RAIS Omar al-Bashir wa Sudan amemfukuza Balozi wa Kenya nchini humo, kufuatia Mahakama Kuu ya Kenya kutoa amri ya kukamatwa kwa rais huyo. Pia amemuagiza balozi wake aliyeko mjini Nairobi arejee nyumbani.

Rais Bashir ambaye anatafutwa na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) amempa saa 72 balozi huyo awe ameondoka mjini Khartoum.

Kwa mujibu wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Kenya, Nicholas Ombija, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Usalama wa Ndani lazima watekeleze amri hiyo ya kumkamata iwapo Rais Bashir atakanyaga tena ardhi ya Kenya.



Habari zinasema, japokuwa Kenya ni mwanachama wa mahakama ya ICC, vyombo vyake vya usalama havikuweza kumkamata Rais Bashir wakati alipoitembelea Kenya mwezi Agosti, mwaka jana.

Kutokana na hatua hiyo, baada ya tawi la shirika lisilo la kiserikali, Tume ya Kimataifa ya Wanasheria, iliomba Mahakama Kuu itoe hati ya kumkamata. Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan awali ilijaribu kupuuza uamuzi wa Jaji huyo ikisema uamuzi huo ulikuwa ni maswala ya ndani ya Kenya, ambayo yasingeathiri uhusiano kati ya Sudan na Kenya.


Sunday, November 27, 2011

Congo yachafuka, wawili wauawa


Ikiwa leo wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanatarajia kumchagua rais wao vurugu kubwa zaendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Kampeni hizo ambazo hazikumaliza katika muda uliokusudiwa na tume ya uchaguzi lakini kutokana na vurugu kubwa ambazo mpaka sasa zimesababisha watu wawili kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Juzi, polisi nchini humo ilipiga marufuku kampeni zote za uchaguzi katika mji mkuu Kinshasa baada ya wafuasi wa chama tawala na upinzani kushambuliana na kusababisha mauaji.

Licha ya vurugu hizo kuendelea nchini humo na kusababisha wananchi kuwa na wasiwasi zaidi hasa leo ambapo wanamchagua rais wao atakaoliongoza taifa hilo kwa awamu nyingine pamoja na wabunge.


Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha UDPS katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakiyakimbia mabomu ya machozi yaliyolipuliwa na polisi nchini humo karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa uliopo mjini Kinshasa.

Rais Joseph Kabila na mahasimu wake wakuu wawili Etienne Tshisekedi na Vital Kamerhe juzi walikuwa wamejitayarisha kufanya kampeni za lala salama za uchaguzi huo katika maeneo yanayokaribiana mjini Kinshasa hata hivyo kampeni hizo zilikatishwa na vurugu kubwa zilizoibuka mkutanoni hapo.

Habari zinasema, licha ya leo wananchi wanamchagua kiongozi wao lakini bado kuna wasiwasi kuhusu ugawaji karatasi za kupigia kura, kwa kuwa ndege zimeshindwa kufika baadhi ya maeneo kutokana na hali mbaya ya hewa.


Hivi tunaelekea wapi??!!

Thursday, November 3, 2011

Hapa ni Dar, hii ni shule

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akiangalia mmoja ya darasa lililojengwa mwaka 1978 katika Shule ya Msingi Ushindi iliyopo Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam ambalo halitumiki kufuatia kuchakaa kwake na shule hiyo kushindwa kulikarabati.

Viungo vya binadamu vyampeleka jela miaka 10

Mkazi wa Kijiji cha Wami Dakawa, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Fatma Kachingo, akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kukutwa na fuvu la binadamu eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Morogoro muda mfupi kabla ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela, kufuatia kukiri kosa.


Mwanamke aliyekutwa na viungo vya binadamu, amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela baada ya kukiri kosa hilo huku mume wake akirudishwa mahabusu baada ya kukana shtaka.

Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, walipofikishwa washtakiwa hao ambao ni mume na mke; Fatuma Kachingo (42) na Mogela Victory (38), wakazi wa Kijiji cha Wami Dakawa, Wilaya ya Mvomero.

Hakimu Nuru Nassari alisema kitendo cha mshtakiwa kukiri kosa kinaifanya mahakama kuamini kuwa, alifanya kosa hilo kwa makusudi huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria na kwamba, adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wengine wanaomiliki viungo vya binadamu kwa imani za ushirikina.

Kabla ya kutiwa hatiani, mshtakiwa huyo alijitetea ili mahakama impe adhabu ya huruma kwa madai kuwa, ana familia inayomtegemea wakiwamo wajukuu na umri wake ni mkubwa.

Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali utetezi huo baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Lameck Wabi, kuomba kutoa adhabu kali kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ukataji viungo unaofanywa kwa imani za ushirikina.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja Oktoba 29, mwaka huu saa 2:00 asubuhi, walikutwa na fuvu na ngozi ya binadamu ambavyo vilihifadhiwa chumba kimojawapo kwenye nyumba wanayoishi.

Vitu vingine ni magamba ya konokono ambavyo vinadhaniwa vinatumika katika shughuli za ushirikina.


Htimaye Kabwe afanyiwa operesheni

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akila matunda baada ya kufanyiwa operesheni katika Hospitali ya Apollo nchini India, jana. Zitto amefanyiwa operesheni puani kutona na kusumbuliwa na maradhi ya kipanda uso.

Zitto ni kiongozi wa nne kupelekwa India kwa matibabu katika kipindi kisichozidi miezi mitatu, akitanguliwa na mawaziri wawili na naibu waziri mmoja. Hao ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Aligundulika kuwa na maradhi hayo ya kipanda uso ambayo kitaalamu yanajulikana kama sinusitis tayari yakiwa sugu. Alisema Daktari Bingwa wa magonjwa hayo, Dk Kimaryo wa MNH alimweleza kwa kirefu juu ya tatizo hilo na kumshauri kuwa suluhisho lake upasuaji, huduma ambayo ilikuwa haipatikani katika hospitali hiyo ya Taifa.

Tuesday, November 1, 2011

Unafiki bado unaendelea, kuendelezwa huko Libya

Waziri Mkuu mpya wa Serikali ya Mpito nchini Libya, Abdel Rahim al-Kib (Kushoto) akipongezwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mpito (NTC), Mahmoud Jabril ambaye aliahidi kujiuzulu pale nchi hiyo itakapokuwa imekombolewa kutoka katika utawala wa Muammar Gaddafi.

Mambo ya Watanzania hayoooo! Toka kwa Shivooo!

Miss Vodacom Tanzania 2011, Salha Israel (kushoto) akiwa katika vazi la ufukweni na wenzake katika maonesho ya mavazi hayo, nchini China juzi.

Monday, October 31, 2011

Kizazi kipya cha siku hizi si mchezo

Hii sijawahi kuona tangu nimeanza kujitambua mimi ni nani!

Kiukweli hawa ni mbuzi, tena hapa ni nchini Moroco, hawa mbuzi wanapanda juu ya miti kutafuta majani kama chakula chao

Sunday, October 30, 2011

Sijaelewa vizuri, ama sijui!

Inakuwaje unapiga simu haipokelewi, wewe unaendelea kupiga! Kwa nini ung'ang'anie kupiga simu wakati umekwishapiga mara ya kwanza haijapokelewa, unaendelea kupiga zaidi hata ya mara tano!
Ukiona kimya ujue muhusika yupo mbali na simu, akiichukua simu yake ataona kuwa alipigiwa na atakupigia, tusing'ang'anie kupiga jamani, pengine mwenyewe amelala au yupo busy

Mtoto wa Nguema Mbasogo aanza kufilisiwa


Wakati wa kutawala maisha yote hauna nafasi tena. Upepo wa mabadiliko uliovuma na kuwang'oa vigogo waliotawala kwa miaka mingi Afrika, sasa unaonekana kunaelekea kwa kiongozi mwingine barani Afrika aliyekaa madarakani kwa muda mrefu.

Upepo wa mabadiliko sasa unaelekea nchini Equatoral Guinea ambako mtoto wa rais wa nchi hiyo ambaye anatarajwa kuwa mrithi wa nchi atakapo ondoka madarakani baba yake iwe kustaafu au kifo, ameanza kuandamwa na mataifa mbalimbali wakitaka afilisiwe huku wakimwita ‘mla rushwa.’

Kilichomkuta Gaddafi chaweza kumkuta mtoto huyo, Teodoro Nguema Obiang Mangue kwa sababu nguvu kubwa ya kumuondoa madarakani inatoka nchi za magharibi.

Mangue anatuhumiwa kutumia madaraka yake na ya baba yake kujipatia kipato isivyo halali.

Mangue ni Waziri wa Kilimo na Misitu, anatuhumiwa kuwa na mali nyingi nje ya nchi ambazo zimekubaliana kuzishikilia mali hizo na kuzirudisha kwa wananchi itakapobidi.

Ufaransa yakamata magari yake

Wakati watu 'wakimechisha' viatu na nguo, Mangue anasifika kwa kununua viatu na magari yanayofanana. Akivaa vitu vya bluu, atatoka na Ferrari Enzo ya rangi hiyo.


Ufaranza imekuwa ya kwanza kumchukulia hatua kwa kuyakamata magari yake yote ya kifahari aliyokuwa akiyamili katika ardhi ya nchi hiyo.

Miongoni mwa magari ya kifahari yaliyokamatwa ni pamoja 'Bugatti Veyrons', 'Maserati MC12', 'Porsche Carrera GT', 'Ferrari Enzo', Aston Martin,Rolls Royce Phantom coupé na 'Ferrari 599 GTO'.

Magari yote yaliyokuwa katika ardhi ya nchi hiyo yanashikiliwa ingawa haijajulikana mpaka sasa yatapelekwa nchini Equatorial Guinea au yatauzwa na pesa hizo kurudishwa.

Hata hivyo, nchi hii imeilaumu Serikali ya Marekani kwa kushindwa kulizuia jumba la kifahari la mwanamume huyo lililopo eneo la Malibu ambalo linasifika kwa kuishi mastaa wenye pesa wa nchi hiyo.

Mangue anamiliki jumba linalokadiriwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 35 ambalo alilinunua mwaka 2008 kwa fedha taslimu.


Mbali na jumba hilo, anamiliki ndege binafsi na boti ya kifahari hata hivyo uchunguzi wa awali wa Marekani unasema vitu hivyo amevihamisha kutoka huko na haijulikani amevipeleka nchi gani.

Anapenda umaarufu

Mangue anasifika kwa kuwa karibu na wasanii wakubwa maarufu, moja kati ya watu wake wa karibu ni Mwanamuziki, Janeth Jackson na familia nzima.


Pia anakumbukwa kwa kuinunua ‘glavu’ ya Mwanamuziki Michael Jackson kwa kiasi cha dola za Marekani 3.2milioni, pengine huu ulikuwa mwanzo wa familia ya Jackson kumjua.

Inaelezwa mara kadhaa amekua akiwaalika nchini kwao kaka wa marehemu, Michael Jackson, huku akisisitiza ujio wao ni kibiashara.

Inaelezwa kuwa pia Mangue amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii wa Marekani, Eve. Uhusiano huu ulidumu kwa muda wa miaka miwili.


Anakumbukwa kwa kumfanyia sherehe za kifahari mwanamuziki huyo na kumnunulia zawadi kubwa ikiwemo magari ya kifahari.

Yote kwa yote, Ufaransa imeanza kuchukua hatua, je, ni nchi gani inafuatia katika hili, na je, huu ni mwanzo wa mwisho wa utawala wa baba yake, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo?


Hii ndio Bongo bwana, we acha tu!

Tuwalee, nasi ni watoto wetu

Mlezi wa watoto wa Kituo cha Watoto Yatima na wanaoishi katika Mazingira Magumu cha Samaritan, jijini Arusha, Eli Malemba, akiwanyeshwa uji watoto Ebeneza na Baraka, wanaolelewa katika kituo hicho.

Saturday, October 29, 2011

Watani wa jadi, mmh..Iwe bhojoo!! YANGA HUREEEEEE!!

Mapemaaa.. Tukajua huyu Simba wetu tu!!
Tukamkamata, tukamlegeza kwanza kabla ya kumchinja!


Kaka sisi kama watani zangu Wamakonde, 'hata Chimba tunakulaga chichi'

Thursday, October 27, 2011

Mume wa Kim Kardashian apigwa chini


NI takribani wiki nane zimepita tangu staa wa televisheni, Kim Kardashian afunge ndoa na mcheza kikapu, Kris Humphries lakini ndani ya muda huo matukio mengi yamewakumba wanandoa hao.
Habari zinasema kuwa baada ya Hamphries kufunga ndoa na Kim, walikubaliana kuwa na yeye angekuwa sehemu ya kipindi cha televisheni cha Keeping Up With The Kardashian.
Lakini kampuni inayotengeneza kipindi hicho imekataa kumuingiza mwanamume huyo kama mmoja wa washiriki huku akielezwa kuwa kama atataka kutokea hata lipwa hata senti.
Kampuni inayoandaa kipindi hicho, William Morris Endeavor Entertainment imemkataa Humphries ikisema kuwa haitakuwa na mkataba wowote na mcheza kikapu huyo linapokuja suala la malipo.
Wakati Humpries akipigwa chini kwenye kipindi hicho, habari zimezagaa kuwa wawili hao wako mbioni kutalikiana. Inaelezwa kuwa Kim yuko mbioni kueleza sababu za kuoana na kuachana katika kipindi kifupi.

Miranda Kerr aonyesha sidiria ya almasi


KUNA usemi kuwa almasi ndiye rafiki wa kweli wa mwanamke, lakini kwa Miranda Kerr kwake imekuwa zaidi anapofikia kuvaa sidiria iliyonakshiwa kwa vito vya madini hayo.
Miranda ambaye asili yake ni Australia amenunua sidiria hiyo kwa dola za Marekani 2.5mil. Anatarajia kuionyesha inavyokaa pale anapoivaa katika fasheni shoo itakayofanyika Novemba 29 mwaka huu.
Watengenezaji wa sidiria hiyo, wamemuomba Miranda ashiriki katika onyesho la mavazi maalumu kwaajili ya kuonyesha sidiria hizo ambazo unapoivaa unapaswa kuwa na ulinzi wa kutosha.
Onyesho hilo litarushwa moja kwa moja katika kituo cha televisheni cha CBS.
Sidiria moja imewagharimu watengenezaji masaa mia tano ambayo ni wastani wa siku 20. Vipande 3400 vya almasi vimetumika kunakshi sidiria hiyo.

Cher Lloyd umaarufu haujanizidi


LONDON, Uingereza
CHER Lloyd ambaye ni staa wa shindano la uimbaji nchini Uingereza, X Factor amesema umaarufu alioupata haujabadili maisha yake.
Lloyd amesema tangu aingie kwenye shindano hilo maisha yake yamebadilika kwa kutazamwa tofauti na watu lakini si katika maisha yake binafsi.
Binti huyo mwenye umri wa miaka 18 amesema bado ananunua nguo katika maduka yaleyale aliyokuwa akinunua zamani.
"Watu wakishapata umaarufu huwa wanabadili kila kitu wakati mwingine hata marafiki, lakini mimi bado nanunua nguo katika maduka yaleyale ya watu wa kaiwada na pia marafiki zangu ni walewale," alisema Llyoid.
Mwanamuziki huyo chipukizi anasema jamii inataka kumbadilisha lakini hakubaliani na hali hiyo kwani anataka kuendelea na maisha yake ambayo ni mazuri sana.
"Kuna siku niliingia kwenye duka moja ambalo linasifika kwa kuwauzia nguo mastaa, bei zake zilinishtua sana na niliondoka bila kununua chochote,
Lakini pia kuna siku nilikutana na mashabiki wangu katika maduka ya kawaida wakaniuliza kwanini ninafanya manunuzi katika maduka yale,niliwajibu ndiyo maisha yangu ya kila siku na hayawezi kubadilika," alisema Lloyd.