Tuesday, April 10, 2012
























Huzuni yazidi Dar!

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete akiweka saini kwenye kitabu cha Maombolezo ya Msanii nguli wa Filamu nchini, Marehemu Steven Kanumba aliefariki Dunia siku mbili zilizopita nyumbani kwake Sinza Vatican,Jijini Dar es Salaam.


Mbunge wa Urambo Magharibi, Mheshimiwa Juma Kapuya akiweka saini kwenye kitabu cha Maombolezo ya Msanii nguli wa Filamu nchini, Steven Kanumba



Iman Madega naye alikuwapo, hapa akiweka saini kwenye kitabu cha Maombolezo


Mkongwe wa Muziki nchini,King Kikii akiweka saini kwenye kitabu cha Maombolezo ya Marehemu Steven Kanumba aliefariki nyumbani kwake Sinza Vatican,Jijini Dar es Salaam.


Mke wa Rais,Mama Salma Kikwete akikumbatiana na Mama Mzazi wa Marehemu Steven Kanumba wakati alipofika nyumbani hapo kwa ajili ya kuhani msiba huo,jana jioni


Mke wa Rais,Mama Salma Kikwete akimfariji Mama Mzazi wa Marehemu Steven Kanumba,Nyumbani kwa Marehemu,Sinza Vatican jijini Dar jioni ya leo. Kushoto ni Dada wa Marehemu Steven Kanumba.


Baadaye Mama Salma Kikwete alipata muda na kuzungumza na wasanii waliokuwa wakifanya kazi pamoja na marehemu













Monday, April 9, 2012

Ratiba ya mazishi ya Steven Kanumba


Msanii wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012, atazikwa kesho Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Mazishi ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu, mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.

Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo katika tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye maisha ya milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye shughuli nzima.


Ratiba

Mwili wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga.

Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi, wakijipanga kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.

Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.

Saa 6:00 mchana, ratiba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya Kinondoni, msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea makaburini.

Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya marehemu.

Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili kumuaga kwa heshima.

Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe.


K.N.Y GABRIEL MTITU

MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

Hatima ya Lulu iko mikononi mwa DPP



Hatma ya msanii maarufu wa kike Elizabeth Michael maarufu kama ‘Lulu’ anayeshikiliwa polisi kufuatia kifo cha msanii Steven Kanumba iko mikononi mwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema suala la msanii huyo kusema ana kesi ya kujibu au la, liko mikononi mwa DDP ambaye ndiye atakayepitia jalada baada ya polisi kukamilisha upelelezi wao.

Kamanda Kenyela alisema Lulu kupelekwa mahakamani ni uamuzi wa DPP ambaye atatakiwa kulipitia faili lake na kujiridhisha kama ana kesi ya kujibu au la.

“Kumpeleka mahakamani ni mpaka DPP tutakapomwasilishia jalada la tuliyoyakusanya na ndiye atakayeamua kama kuna kesi ya kujibu au hakuna,”alisema Kamanda Kenyela.

Alisema hadi hivi sasa bado wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa daktari ambao hata hivyo hawatautoa kwa vyombo vya habari kwa kuwa huwa ni siri.

“Bado tunasubiria ripoti ya daktari na upelelezi unaendelea ila ripoti hiyo ni siri, si lazima apelekwe mahakamani kesho (leo) kwa kuwa bado upelelezi unaendelea,”alisema Kenyela.

Kanumba alifariki usiku wa kuamkia Jumamosi nyumbani kwake, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kenyela, zilieleza kuwa kifo cha msanii huyo kilitokana na ugomvi uliotokea kati yake na mpenzi wake ndani ya nyumba yake.


Taarifa za kifo cha Kanumba zilianza kusambaa kuanzia saa 10.00 alfajiri na kuenea kwa kasi ambapo hadi kufikia saa moja asubuhi, mamia ya watu walikuwa wamejazana nyumbani kwa Kanumba kutaka kuthibitisha habari hizo.

Kadri muda ulivyozidi kusogea ndivyo idadi ya watu ilizidi kuongezeka nyumbani kwa msanii huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kutoka na filamu zake kuuzwa na kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa watu waliomiminika kwa haraka nyumbani kwa Kanumba ni wasanii wa fani mbalimbali nchini, wanasiasa na viongozi mbalimbali wa Serikali


Chanzo cha kifo chake

Kwa mujibu wa maelezo ya mdogo wake aitwaye Seth ambaye alikuwapo eneo la tukio, alisema kaka yake alishinda nyumbani na baada ya kula chakula cha jioni, alimwambia wajiandae kutoka.

Hapa mwili wake ukiwekwa vizuri kabla haujaingizwa monchwari ya Muhimbili


Seth alisema kuwa wakati Kanumba akiwa tayari amejiandaa, walisikia mlio wa gari likifunga breki nje ya nyumba.

Alisema gari hilo lilikuwa limemleta mpenzi wa kaka yake msanii wa filamu, Lulu ambaye aliingia ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwa Kanumba.

Baada ya kuingia ndani, muda mfupi alisikia sauti zilizoashiria kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya wapenzi hao.

“Ghafla ulizuka mzozo ndani na dakika chache baadaye, Lulu alitoka na kuja kuniambia kuwa Kanumba amedondoka baada ya kujigonga ukutani na kwamba yupo taabani hajitambui,” alisema Seth.

Alisema alipoingia chumbani, alimkuta kaka yake akiwa katika hali mbaya hivyo akaamua kumpigia simu daktari wake, ambaye alipofika na kuwashauri wampeleke haraka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu.

Seth alisema kabla ya kufika Muhimbili walipitia Kituo cha Polisi cha Oysterbay kupatiwa Fomu ya matibabu (PF3).

Hata hivyo, baada ya polisi kupata maelezo ya awali ya ugomvi huo, walimshikilia Lulu kituoni hapo na kumwacha Seth akimpeleka Kanumba hospitali.

Alisema walipofikia Hospitali ya Muhimbili, madakati waligundua kuwa tayari Kanumba alishaaga dunia.

Awali Kamanda Kenyela akithibitisha kutokea kwa tukio hilo alisema Kanumba alikufariki kutokana na ugomvi uliotokea kati yake na rafiki yake wa kike Lulu.

Sunday, April 8, 2012

Leo jioni hii

Kuonyesha kuwa marehemu alikuwa mtu wa watu geti la nyumba yake limefungwa wandani wandani wa nje wa nje, wengine iliwalazimu kupanda juu ya ukuta ili kupata jua yanayojiri ndani, kweli mdogo wetu alipendwa na watu!



Kwa kifupi njia imefungwa.....watu wa usalama barabarani wametanda hapa

Mwanzo, mwisho wa Steven Kanumba



“Amka Kanumba, mama amekuja. Amka baba. Unameremeta baba, ndoa yako ya mwisho hii… kwaheri mwanangu,” ni maneno ya Mama Mzazi wa Steven Kanumba, Flora Mtegoa mara baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu Sinza, Dar es Salaam akitokea Bukoba.

Maneno hayo yaliyokuwa yakiambatana na kilio alikuwa akiyatoa huku akichanganya lugha za Kisukuma na Kiswahili alieleza jinsi alivyopata taarifa za msiba, adhuhuri ya Aprili 7.

Mara baada ya kuwasili Sinza, Vatican nyumba ya marehemu Kanumba ilizungukwa na umati wa waombolezaji, waliokuwa ndani walitoka kumpokea na hata wale waliokuwa jirani na eneo hilo walisogea wakitaka kumuona.

Kuwasili kwa mama huyo kuliongeza machungu kwa ndugu, jamaa, wasanii na mashabiki ya msanii huyo nguli kiasi cha baadhi yao kupoteza fahamu.

Kikwete aahirisha safari

Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya waombolezaji katika msiba wa msanii huyo akisema alilazimika kusitisha safari yake ya nje ya nchi ili kuungana na wananchi wengine katika maombolezo hayo.

“Nimeguswa na msiba huu, nilikuwa nisafiri lakini nimeamua kuja hapa kuwapa pole ndugu na wasanii wote,” alisema Rais.

Rais Kikwete akisalimiana na mdogo wake Kanumba, Sethi alipowasili nyumbani kwa marehemu Sinza ‘Vatican’ leo

Rais Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu Steven Charles Kanumba

Rais Kikwete akiwafariji wafiwa nyumbani kwa marehemu Steven Charles Kanumba Sinza ‘Vatican’ Dar leo April 8, 2012 alikofika kuwapa pole

Rais Kikwete akiwafariji wafiwa


Kanumba (28), ambaye anatarajiwa kuzikwa kesho katika Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa Polisi inachunguza tukio hilo huku ikimshikilia msanii wa kike, Elizabeth Michael (Lulu).

Ndugu wa marehemu, Seth Bosco ambaye ana sura inayoshabihiana kwa karibu Kanumba alisema kauli ya mwisho kuisikia kutoka katika kinywa cha kaka yake huyo ilikuwa ni ‘nisubiri.’

Alisema jioni ya Aprili 6, mwaka huu, marehemu alimwambia angependa watoke kwenda matembezini pamoja.

“Ilipofika sita za usiku, nilimwambia kuwa mimi nimekwishajiandaa, akasema ‘nisubiri’ na kisha akaingia chumbani mwake,” alisema Seth na kuongeza:

“Kanumba akiwa chumbani kwake, aliingia binti mmoja, ambaye ninamfahamu kuwa ni mtu wake wa karibu. Kwa kuwa namfahamu, sikushangazwa na ujio wake, aliingia chumbani kwa Kanumba.”

Seth alisema baada ya muda, alisikia sauti zilizoonyesha mgogoro wa aina fulani kutoka chumbani humo na alipotaka kuingia, mlango ulikuwa umefungwa kwa funguo.

“Nilisikia Kanumba akimwambia Lulu; ‘Yaani unapigiwa simu na mwanamume wako mbele yangu?’ Baada ya dakika kadhaa za mzozo chumbani, Lulu alitoka akisema kuwa Kanumba ameanguka,” alisema Seth.

Lulu

Alisema ripoti ya awali ya daktari inaonyesha kuwa marehemu hana jeraha lolote katika mwili wake… “Kama alisukumwa ukutani, basi lazima jeraha lingeonekana katika ubongo, lakini ripoti inaonyesha hana jeraha na mimi nilimkuta marehemu akiwa anatokwa na povu mdomoni, macho yamemtoka, huku akikoroma, cha ajabu hakutokwa damu… bado tunasubiri uchunguzi zaidi wa polisi.”

Akizungumzia msiba huo dada wa marehemu, Kabela Kajumulo alisema: “Ninachoweza kusema ni kuwa, tumepata pengo lisiloweza kuzibika.”

Wasanii wamwelezea

Wasanii wa filamu na muziki waliokuwa katika msiba huo walimwelezea marehemu Kanumba kwamba alikuwa ni mtu wa watu.

Akimzungumzia marehemu Kanumba, mmoja wa wasanii hao, Blandina Chagula (Johari), alisema alikuwa zaidi ya rafiki kwake akisema hawakujuana katika maigizo tu, bali walicheza pamoja tangu utotoni.

“Nimesoma na Kanumba Mwanza, Shule ya Msingi Bugoyi, lakini si hivyo tu, bali mama yake Kanumba na mama yangu ni marafiki wa karibu. Tulikutana tena hapa jijini, lakini yeye akisoma Shule ya Jitegemee mimi, shule nyingine, ndipo tulipojiunga katika maigizo katika Kikundi cha Kaole.”

Johari alisema amepata pigo kwa kuondokewa na Kanumba kwani alikuwa ni zaidi ya kaka na zaidi ya rafiki akisema alikuwa mshauri na alimuonya pale alipokosea.

Alitaja mambo matatu ambayo angependa wasanii wengine wamuige Kanumba. Aliyataja kuwa ni uchapakazi, kujihifadhi na ustaarabu…“Hana mfano wake, alikuwa ni mstaarabu, mwenye upendo na anayejiheshimu,” alisema Chagula.

Ruth Suka (Mainda) ambaye aliwahi kufanya kazi na marehemu Kanumba pia alimwelezea kuwa alikuwa miongoni mwa watu wachapakazi na wanaojiheshimu.

Alisema Kanumba alikuwa kijana mstaarabu na kabla hajawa maarufu, alikuwa akiogopa mno kuwa karibu na wanawake… “Ni mtu aliyejisitiri mno na mambo yake, lakini mazingira yake ya usanii yalimfanya aanze kuchangamka na kujichanganya na watu wa rika zote. Kwa kifupi ni mtu wa kanisa.”

Msanii mwingine ambaye pia alisoma na marehemu Jitegemee, Emmanuel Myamba alisema alikuwa na uhusiano wa karibu na kwamba alifahamu mambo mengi na kujifunza mwengi kupitia kwa marehemu.

Ujumbe wa mwisho

Aprili, 6 mwaka huu Kanumba alitoa ujumbe ulioonekana kutabiri kifo chake, akiyanukuu maneno ya Mwanafalsafa, Albert Pine na ujumbe huu aliuandika baada ya kutoka kwenye uzinduzi wa jengo la THM lililopo Msasani jijini Dar es Salaam na hapo juu ni picha alizopiga akiwa pamoja na Khadija Mwanamboka katika uzinduzi huo yaliyosema:

"What we do for ourselves dies with us. What we do for others and the world remains and is immortal."

“Tunachofanya kwa ajili yetu tunakufa nacho. Lakini tunachofanya kwa wengine na kwa ulimwengu, kinadumu na ni cha milele.”