Thursday, June 21, 2012
Tuesday, June 19, 2012
Safari ya Drogba China yaiva
![]() |
| Add caption |
SHANGHAI, China
SAFARI ya mshambuliaji wa zamani wa Chelsea ya England, Didier Drogba kwenda kumalizia soka nchini China, imeiva na anatarajia kujiunga na timu ya Shanghai Shenhua wakati wowote wiki hii.
Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ameelezwa kuingia mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya pauni 25 milioni (sawa na Sh60.8 Bilioni).
Kwa sasa Drogba (34) yuko nchini India
Kwa mujibu wa bosi wa klabu hiyo ya China, Zhu Jun, Drogba anatarajia kutangaza uhamisho huo kwenye tovuti yake binafsi.
Mbali na timu hiyo ya China kumtaka drogba, klabu nyingine tajiri ya falme za Kiarabu, Al Wasl FC nayo imeonyesha nia.
safari yake ya China inatarajia kumkutanisha na mshambuliaji mwenzake aliyecheza naye pamoja kwenye kikosi cha Chelsea, Nicolas Anelka.
"Hatua inayofuata kwangu nimefurahi," alisema Drogba wakati wa ziara yake nchini India.
"Muda siyo mrefu nitatangaza uamuzi wangu, lakini kwa sasa ningependa msubiri kwanza," alisema Drogba.
Klabu hiyo ya China imekusudia kufanya mageuzi makubwa kwa kusajili wachezaji wengi wa kigeni pamoja na kocha pia.
Friday, June 15, 2012
Binti aliyehukumiwa kupigwa mawe hadi kufa kwa uzinzi
BLANKETI la uchungu na kukata tamaa limeufumbata uso wa Intisar Abdallah.
Ameketi katika chumba cha jela chenye joto kali, miguu yake ikiwa imefungwa kwa chuma,huku akiendelea kukinyonyesha kichanga chake chenye umri wa miezi mitano.
Intisar, ameathirika kisaikolojia kwa sababu anajua fika kuwa, siku si nyingi ataingizwa kaburini.
Machungu ya Intisar, (20) hayakomei katika hofu ya kifo pekee, bali hata namna na sababu ya kifo hicho.
Intisar, atachimbiwa ardhini na kubakizwa kichwa tu. Kisha atapigwa mawe hadi kufa ikiwa ni adhabu yake baada ya kuzini na kubeba mimba.
Aprili 22 mwaka huu ndiyo siku ambayo Hakimu, Sami Ibrahimu Shabo wa mahakama ya makosa ya jinai ya Ombada iliyoko katika mji mkuu wa Khartoum, Sudan alimhukumu Intisar adhabu kifo.
Kilimchofanya mpaka binti huyu akapewa adhabu hii ni kwa sababu alifanya tendo la ngono nje ya ndoa. Instisar ambaye ni mama wa watoto watatu alionekana mwenye kosa la jinai kwa nchi zenye misingi imara ya dini ya Kiislam.
Hukumu ya Intisar ilitolewa kwa sababu ya kifungu namba 146 cha mwaka 1991 cha makosa ya jinai nchini Sudan.
Awali, Intisar alishtakiwa kwa uzinzi, lakini akaachiwa huru. Baadaye, kaka yake alimpiga kikatili na kumshurutisha akimtaka akiri makosa yake.
Hapana shaka kipigo kile ndicho kilichomfaya Intisar akubali kosa hilo.
Hata hivyo, mwanamume waliyezini naye aliachiwa huru kwa sababu tu, alikana kosa hilo.
Wakati huo, kesi iliendeshwa kwa lugha ya kiarabu,ambayo Intisar haifahamu. Hukumu ikatolewa wakati Intisar akiwa hana wakili wa kumtetea katika hilo.
Mawakili waliruhusiwa kumwona na kumuhoji mara baada ya hukumu kutolewa.
Hukumu ya kuua haikubaliani na sheria za kimataifa, kwani inaenda kinyume na haki za binadamu.
Pamoja na hilo, lakini kibaya zaidi ni kumhukumu kifo mama mwenye mtoto mchanga ni kitendo kinachopingwa na sheria za kimataifa.
Hukumu hiyo ilipingwa vikali na mtandao wa kikundi cha Mapambano cha Wanawake waishio katika Pembe ya Dunia (SIHA network).
Siha kilitoa tamko kali kuhusu kesi hiyo na kusema imejaa upungufu, unyanyasaji na uvunjwaji wa haki kwa kiasi kikubwa.
“Ni ajabu kwamba mwanaume ambaye anatuhumiwa kuzini naye ameachiwa huru. Jambo ambalo linaweka wazi ukatili wa kijinsia na usimamizi mbaya wa migogoro ya kifamilia,” ulisema mtandao huo.
Sudan ya Kaskazini ni miongoni mwa nchi saba duniani zinazotoa adhabu ya kifo kwa kupigwa mawe.
Rais Omar Al Bashir ndiye aliyetambulisha chembechembe za Sharia Law, mwaka 1989 baada ya kuingia madarakani.
Lakini kinachowachanganya wengi ni kuwa, adhabu hizo huwapata zaidi wanawake kuliko wanaume.
Wananchi nchini humo wamekuwa wakifungwa vifungo vya muda mrefu na kupewa adhabu kali kwa makosa kama ya kuuza bidhaa barabarani, kuvaa mavazi yanayokwenda kinyume na taratibu za kidini pamoja uzururaji.
Watu wamewahi kupigwa mawe hadi kufa baada ya kufanya makosa ya uzinzi.
Julai 13, 1997 Changiz Rahimi alihukumiwa kupigwa mawe hadi kufa, huku akilipa faini kwa kuzini.
Julai 14, 1995 wanawake wawili Sada Abdali, 30, na Zeinab Heidary, 38 walihukumiwa kupigwa mawe katika Jiji la Ilam, Gharb.
Lakini pia wapo wanawake waliohukumiwa kupigwa mawe, lakini wakaponea chupuchupu.
Mwaka 2002, Amina Lawal, Nigeria, alihukumiwa kupigwa mawe, lakini aliachiwa huru baada ya kukata rufaa.
Sakineh Mohammadi Ashtian alihukumiwa nchini Iran mwaka 2007, lakini hukumu yake ikapingwa na ipo katika mjadala.
Mwingine ni Safiya Husseini wa Nigeria pia, yeye aliachiwa huru baada ya kukata rufaa.
Ateseka na saratani ya mifupa kwa miaka kumi
WAKATI saratani ya matiti ikiwa tishio kwa wanawake wengi duniani, mwanamke mmoja nchini China anateseka na uvimbe mkubwa usoni mwake uliosababishwa na kuugua saratani ambao amedumu nao kwa miaka 10 sasa.
Li Hongfang (40), ameshindwa kupata matibabu ya kuondoa uvimbe huo unaomsumbua kutokana na kutomudu gharama za matibabu. Ugonjwa huo ambao umeelezwa na madaktari kuwa ni aina ya saratani ya mifupa, ni ugonjwa unaosababisha tishu kukua.
"Mimi si mtu wa kutisha, bali ni mgonjwa tu, lakini watu wengi wamekuwa wakisema kuwa ninatisha na wengine kunikimbia," anasema.
Tatizo lake lilianza mwaka 2001, wakati huo aliona kivimbe kidogo pembeni mwa kichwa chake, lakini anasema hakukitilia maanani kwani kilikuwa hakina maumivu yoyote.
Baada ya afya yake kuanza kubadilika miaka minne baadaye, madaktari walisema kuwa ana jumla ya uvimbe mdogo mdogo saba unaozidi kukua katika uso wake.
Lakini hakuweza kuwa na gharama ya kiasi cha Pauni 60,000 (zaidi ya Sh150 milioni) ili aweze kupatiwa matibabu.
"Najua kwamba watu wengi sasa wananiangalia mimi kama mtu fulani wa kutisha, lakini bado nabaki kuwa mwanamke wa kawaida na mama kwa upande mwingine," anasema.
Kwa mujibu wa madaktari, aina hiyo ya saratani huanza kukua katika fuvu la kichwa na chini ya mgongo. Ingawaje hakuna takwimu sahihi, lakini inaelezwa kuwa ugonjwa huu huathiri mtu mmoja kati ya watu milioni moja nchini Marekani.
![]() |
| Akilia kwa uchungu baada ya kueleza yanayomsibu, kama binadamu wa kawaida ni lazima ujisikie vibaya kwa jinsi watu wengine wanavyomchukulia |
Hongfang ameteseka na ugonjwa huo kwa kipindi chote hicho kutokana na mfumo duni wa matibabu na kuchelewa kupata huduma.
Wakati alipoanza kupatwa na ugonjwa huo, alikuwa akiishi na mumewe na watoto wawili katika kijiji cha Tianchao, katika Kata ya Qianxian huko Magharibi mwa China.
"Hatukuwa na fedha nyingi, lakini tulikuwa na furaha sana na tulipendana pamoja na watoto wetu wawili wa kiume. Ninaweza sema maisha yalikuwa mazuri sana, lakini kadri uvimbe ulivyozidi, aliniacha na kwenda mbali.
"Sikuwahi kufikiria kitu chochote nilipoanza kuuona uvimbe ule katika kichwa changu, nilidhani pengine ni aina tu ya wadudu walikuwa wamening'ata,” anasema.
Anaongeza: "Sikuweza kufanya lolote nilikuwa nakuna tu na kuacha lakini ilianza kukua kwa kasi.”
Nchini China, huduma za afya zinasua sua sana katika miaka ya hivi karibuni, lakini katika miaka ya nyuma kulikuwa na ada maalumu iliyotolewa katika vituo vya afya.
Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo, hawana uwezo wa kupata huduma hiyo.
![]() |
| Akionyesha picha za wanawe |
Hivi sasa China imeanza kujadili mpango wenye lengo la kutoa bima za afya kwa watu wote wanaofikia1.3 bilioni na kuazimia kuwa hadi kufikia mwaka 2020, mpango huo uwe umekamilika.
Thursday, May 17, 2012
Kwa kheri Mafisango
Marehemu akiwa nyumbani kwake enzi za uhai wake
Simanzi, huzuni na vilio viliwatawala wanamichezo nchini baada ya kupata taarifa za kifo cha kiungo wa kimataifa wa Rwanda na Simba, Patrick Mutesa Mafisango (32) aliyefariki dunia jana alfajiri kwa ajali ya gari.
Mafisango anatarajiwa kuagwa leo kwenye Uwanja TCC Sigara Chang'ombe jijini Dar es Salaam kabla ya kesho kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao DR Congo kwa mazishi.
Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema taratibu za kuuaga mwili wa marehemu zitaanza saa nne asubuhi mpaka saa 10 jioni.
Mafisango alipata mauti hayo eneo la Veta Chang'ombe usiku wa kumkia jana saa 8.45 alipokuwa akiendesha gari akitokea Maisha Club akiwa na wenzake wanne na alipofika maeneo ya Veta wakati akijaribu kumkwepa mwendesha baiskeli ya miguu mitatu 'Guta' gari lilimshinda na kugonga mti uliosababisha gari yake kuingia mtaroni na mauti kumkuta hapo hapo.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo mtoto wa dada yake Orly Ilemba (24) aliyekuwamo katika gari hilo alisema jana wakati wanavuka mataa ya Veta, marehemu alikuwa katika mwendo kasi mara mbele akakutana na Guta na katika jitihada za kulikwepa akagonga mti na gari kupinduka na kutumbukia mtaroni na mauti kumkuta hapo hapo.
"Tulitoka salama Maisha Club tunarudi nyumbani marehemu alikuwa akiendesha gari katika mwendo wa kasi, tulipovuka mataa ya Veta wakati akiwa 'spidi' tuliona guta kwa mbele yetu pamoja na pikipiki sasa wakati marehemu anakwepa kwa bahati mbaya aligonga mti na gari ikadumbukia ndani ya mtaro huku nikishuhudia kichwa cha ndugu yangu kikigeukia chini kwenye sehemu ya breki na miguu kuja juu kumbe tayari alishafariki......ndipo tukaanza taratibu za kumkimbiza hospitali," alisema Ilemba.
Aliongeza kuwa,"ndani ya gari hiyo aina ya Gx100 tulikuwa watu jumla ya watano mimi, Gaspar Karemera, Bozy na mwanamke mmoja ambaye yeye hatukumfahamu jina lake mara moja akiwa amekaa mbele na marehemu ambaye mpaka sasa bado yupo hospitali akiendelea na matibabu baada ya kuumia sana maeneo ya kichwani,"alisema Ilemba.
Mashabiki wa soka waliofika Kituo cha Polisi cha Chang'ombe wakiangalia gari la marehemu lililopelekwa kituoni hapo janakifo cha Mafisango
Akithibitisha kifo cha mchezaji huyo, Mkuu wa Trafiki katika mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Prackson Lugazia alisema ajali hiyo ilitokea wakati Mafisango aliyekuwa akiendesha gari aina ya GX 100 akitoka Maisha Club akiwa na familia yake akijaribu kumkwepa mwendesha Guta.
Alisema hali hiyo ilisababisha gari hilo kuacha njia na kuingia mtaroni na kugonga miti mitatu kisha kugeuka na kuangalia lilikokuwa likitoka na baadaye kupinduka.
"Baada ya kupata taarifa za ajali hiyo majira ya saa 10 asubuhi tulifika eneo la tukio haraka iwezekanavyo, lakini hatukukuta mtu yeyote zaidi ya gari lililokuwa limepinduka,"alisema Lugazia.
Alisema,"kufuatia hali hiyo ndipo tulipoanza taratibu za kumtafuta marehemu na tulianzia hospitali ya Amana, tulikwenda hospitali ya Mwananyamala na baadaye Muhimbili ambako tuliukuta mwili wake pamoja mwanamke mmoja ambaye alikuwa na majeraha mbalimbali sehemu za mwili wake," alisema Lugazia.
Akizungumza jana alfajiri jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema,"ni kweli Mafisango hatunaye tena, kwa sasa siwezi kuzungumza chochote huyu ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda, ndiyo nafanya mawasiliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na lile la Rwanda (FERWAFA) kuangalia namna ya kuusafirisha mwili wake."
Mafisango amefariki akiwa amemaliza mkataba wake na Simba na alitarajiwa kusaini mkataba mpya juzi na leo alitarajiwa kwenda Rwanda tayari kujiunga na kikosi cha timu hiyo 'Amavubi' kinachojiandaa kwa ajili ya mechi za mchujo za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2014, zitakazochezwa mwezi ujao.
| Baadhi ya wasanii na wachezaji waliofika Hospitali ya Muhimbili kupata uhakika wa kifo cha Mafisango |
"Ukiniambia amefariki sikuelewi hapa nilipo nimechanganyikiwa, kuna vikao vinaendelea (jana), nitakupigia baadaye,"alisema Micho huku sauti yake ikionekana kuwa na majonzi.
Wakati huohuo; Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea leo (jana) alfajiri kwa ajali ya gari Dar es Salaam.
TFF ilisema msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.
Kifo chake ni pigo kubwa sio tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali Ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto za Mafisango zilikuwa dhahiri uwanjani.
BOBAN
Rafiki mkubwa wa Mafisango kiungo Haruna Moshi 'Boban' alikuwa kwenye majonzi makubwa huku machozi yakimtoka bila kuzungumza lolote.
Wakizungumzia ukaribu wa mchezaji huyo na marehemu baadhi ya wachezaji wa Simba walidai Boban ndiye alikuwa rafiki mkubwa wa Mafisango na walikuwa kila mara wakiongozana pamoja katika starehe na hata wakiwa kambini.
![]() |
| Boban |
"Boban ndio alikuwa mtu wa kwanza kusambaza habari za kifo cha Mafisango kwetu na hata aliposikia taarifa hizo alichofanya alikwenda moja kwa moja Muhimbili kwenye chumba cha maiti na kuomba kuonyeshwa mwili wa marehemu na baada ya hapo hakuzungumza lolote mpaka hapa mnavyomuona,"alisema Juma Jabu.
Mafisango alijiunga na Simba akitokea Azam Fc, mwaka jana alizaliwa Machi 7, mwaka 1987, nchini Rwanda na alikuwa akiichezea timu ya Taifa ya nchi hiyo kabla ya kusimamishwa kwa muda mrefu kutokana na utovu wa nidhamu na amerudishwa kundini na kocha Micho, lakini hata hivyo hajaweza kuitumikia timu hiyo ya Taifa lake.
Mchezaji huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika timu ya Simba msimu huu uliomalizika hivi juzi na kung'aa zaidi katika Ligi hiyo kwa kupachika mabao na kutoa pasi za mwisho, ambapo Mechi ya mwisho ya Mafisango ilikuwa ni kati ya Simba dhidi ya Al Ahly Shandy Jumapili katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penati 9-8, kufuatia sare ya jumla ya mabao 3-3.
Wakati mechi ya kwanza kati ya Simba na Wasudan hao iliyochezwa hapa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Mafisango aliifungia timu yake bao moja kati ya matatu yaliyoiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo huo.
Monday, May 14, 2012
Baada ya kazi kubwa sasa ni kusherehekea kwa kwenda mbeleee!
Baada ya miaka 50 ya Uhuru
Umewahi kuiona hii??!! Hakunaga!
Tamwa yawapa somo wakuu wapya wa Wilaya
Shakila Nyerere
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(Tamwa), kimewataka Wakuu wa Wilaya walioteuliwa kuwa makini katika ufuatiliaji wa Watendaji wa Halmashauri katika shule za kata kuepukanana mimba na kufeli kwa wanafunzi wa kike nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Tamwa, Ananilea Nkya alisema wakuu wote wa Wilaya walioteuliwa wawe ni mifano kwa viongozi wengine walioko madarakani kufuatilia majukumu yanayozikabili jamii.
Alisema kwa takwimu walizozifanya kwa kushirikiana na wanahabari kupata takwimu hizo zilizohusu shule za kata katika mikoa 20 Bara na Visiwani kwa kila Wilaya moja katika Kata mbalimbali kwa shule 7 hadi 10 walibaini kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wanoacha shule au kufeli ni wanafunzi wa kike.
Nkya alisema mazingira ya shule zilikojengwa ni hatari kutokana na kukosekana kwa mahitaji muhimu kwa wanafunzi kama vile Maji, miundombinu mibovu ya barabara ni sababu mojawapo ya kuwapa vishawishi wanafunzi wa kike kuishi wakidanganyika kwa kupitia udhaifu wa maisha waliyonayo.
“Wakati mwingine wanafunzi wa kike hulazimika kuishi kwa Walimu wa kiume na kuwa na mahusiano ya kimapenzi kinyume na maadili na sheria na wengine hujikuta wakiishi kwa vijana walioko mitaani kwa kutaka kujikimu kimaisha na kupata mahitaji ya kujikidhi wanapokuwa shuleni, hiyo yote ni hali za shule za kata kuwa na mapungufumengi,” alisema Nkya.
Nkya aliongeza kwa kusema mazingira ya shule za kata zilizoko mikoani na wilayani kwa upande wa walimu ni matatizo makubwa sana maana inafikiwa wakati mwingine shule yenye kidato cha kwanza hadi cha sita kuwa na walimu watatu ikiwa mwalimu wa somo la sayansi ni mmoja na kwingineko hakuna kabisa mwalimu wa somo hilo la sayansi.
Walimu walioko wanaofundisha somo la sayansi ni mwalimu wa somo la sanaa ndiye anayefundisha sayansi kataka shule hizo.
“Ili taaluma ikue nchini hapa kinachotakiwa ni kuboresha mahitaji muhimu ikiwemo miundombinu kwa walimu na wanafunzi ikiwa ni pamoja na uwajibikaji wa viongozi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kufuatilia watendaji katika idara zao.”
Aliongeza kwa kusema wanafunzi wa kike hufeli na kukatiza masomo kwa kubeba mimba shuleni ni pamoja na kukosekana kwa walimu ambao kwa asilimia 80 wamekuwa wakishindwa kuwasili katika vituo vya kazi wanavyokuwa wamepangiwa wakikumbana na mazingira magumu kwa mara ya kwanza.
Pale ubora unapoonekana
Sunday, May 13, 2012
Magari ya kifahari bado yamtoa udenda Cristiano Ronaldo, ayajaza manane uani kwake
Kuwa mwanasoka ghali duniani kunafanya pesa lisiwe tatizo lako la msingi. Ni kama ilivyo kwa staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo. Tajiri huyu kijana ananunua chochote anachojisikia kwa sasa.
Kwa mujibu wa mkataba wake, Ronaldo, analipwa kiasi cha Euro 12 milioni kwa mwaka na Real Madrid. Hii ni achilia mbali mikataba mbalimbali ya kibiashara ambayo inamwingizia mabilioni ya pesa yanayomfanya awe miongoni mwa wanasoka wanaoingiza pesa nyingi zaidi duniani kwa sasa.
Hata hivyo, ugonjwa wake wa kupenda magari ya kifahari umemfanya Ronaldo ajaze magari mengi ya bei mbaya uani kwake. Amekuwa akiyatumia mara kwenda mazoezini na katika matembezi binafsi.
Yafuatayo ni magari manane ya kifahari ambayo Ronaldo ameyajaza uani na ambayo huwa anayaendesha mara kwa mara.
Bugatti Veyron
Hili ndilo gari kipenzi la Ronaldo. Bugatti Veyron ni ghali zaidi na lina mwendo wa kasi zaidi duniani. Mwendo Kasi wake wa juu huwa unafikia kilomita 407 kwa saa na linaweza kumpita dereva wa formula one anayeendesha kwa kilomita 360. Staa wa Cameroon, Samuel Eto’o ni mchezaji mwingine anayemiliki gari la aina hiyo.
Bugatti huwa linauzwa kwa oda maalumu kutoka kiwandani na mhusika analazimika kulisubiri kwa kipindi fulani wakati likitengenezwa. Linauzwa kiasi cha dola 1.2 milioni na hivyo kulifanya kuwa gari ghali zaidi duniani kwa sasa.
Rolls-Royce Phantom Drophead Coupe
Rolls-Royce ni gari linaloheshimika zaidi Uingereza. Gari hili linamilikiwa na watu matajiri. Kuna watu wachache sana wanaomiliki gari hili Uingereza. Lina thamani ya dola 443,000 za Marekani.
Kinachoshangaza ni kwamba nyuma ya gari hili unaweza kufungua katika sehemu ya mizigo na kupata eneo la kukaa kufanya pikiniki.
Ukifungua kuna meza inajipandisha na kuna sehemu za kuwekea vinywaji mbalimbali.
Porsche Cayenne Diesel
Gari hili limetoka Mei mwaka huu na Ronaldo alilisubiri kwa muda mrefu kulinunua moja kwa moja. Lina injini yenye nguvu na kasi yake ni kilomita 218 kwa saa. Kwa suala la mafuta, gari hili lina uwezo wa kutumia lita 10 kwa mwendo wa kilomita 100. Hili ni moja kati ya magari ya bei rahisi ambayo Ronaldo anayo. Lilimgharimu kiasi cha Euro 49,000.
BMW M6
Duniani kote gari hili linatambulika kuwa ndoto ya kila mtu anayetaka kuendesha ‘Sports Car’. Kwa Ronaldo, hili ndilo gari linalomfaa zaidi kwa sababu yeye ni mwanamichezo wa hali ya juu.
Ingawa bei yake ni dola 100,000, Ronaldo hakuona shida kulinunua na kulitupia uani kwake. Ni moja kati ya magari anayotumia sana.
Porsche 911
Ni moja kati ya magari ya kifahari duniani kote. Lilimgharimu Ronaldo kiasi cha euro 201, 682 kuliweka uani kwake. Ni moja kati ya magari anayoyatumia mara kwa mara pia akienda katika starehe zake.
Bentley Continental GT
Hili ni moja kati ya magari yenye nguvu ambayo kampuni ya Bentley imewahi kuyatengeneza. Gari hili pia lina kasi kubwa huku likitumia mwendo wa kilomita 320 kwa saa. Kutokana na mapenzi yake kwa gari hili, Ronaldo alilazimika kutumia kiasi cha dola 375,000 za Marekani kwa ajili ya kulinunua na kuliweka uani kwake. Ni gari la kifahari ambalo ni ndoto ya wengi.
Ferrari F430
Gari hili la siti za watu wawili tu. Kwa sasa ndiyo dili na Ronaldo bado ana mapenzi nalo ya dhati.
Kuna watu wanasema lishastaafishwa lakini Ronaldo hakutaka kuliuza na mpaka leo amekuwa akilitumia mara nyingi. Alitumia kitita cha dola 188,000 za Marekani kulinunua.
Audi R8
Moja kati ya magari yenye kasi duniani. Gari hili lina uwezo wa kukimbia kwa kilomita 316 kwa saa. Kwa kuliweka uwani kwake kukamilisha idadi ya magari manane ya kifahari aliyonayo, Ronaldo alilazimika kujikamua kiasi cha dola za Marekani 109,000 ili kulinunua.
Tajiri anayeishi na Papa nyumbani kwake

Bill Gates anashika nafasi ya pili katika orodha ya watu matajiri duniani. Hiyo ni kutokana na biashara yake ya kompyuta na vipuli vyake.
Anayeshika namba moja kwa utajiri duniani ni raia wa Mexico, Carlos Slim.
Gates ambaye ni Mmarekani, jina lake ni William Henry "Bill" Gates III. Alizaliwa Oktoba 28, 1955 mjini Washington, Marekani.
Ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Microsoft ambayo aliianzisha na tajiri mwenzake, Paul Allen, mwaka 1975.
Microsoft ni kampuni yenye makao yake makuu huko Redmond, Washington, Marekani na inajishughulisha na utengenezaji na usambazaji wa kompyuta na vipuli vyake duniani.
Pamoja na utajiri wake, Gates pia ni mdau mkubwa wa michezo akijihusisha na soka, gofu na tenisi.
Kupitia mfuko wake wa Bill & Belinda Foundation anashirikiana na klabu ya Barcelona ya Hispania katika kuendesha kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa polio duniani.
Kutokana na shughuli zake mbalimbali, Bill Gates ana utajiri wa Dola 61.3 bilioni (Sh5 trilioni za Kenya). Ni kati ya mabilionea wachache duniani.
Ana nyumba sehemu mbalimbali duniani lakini anaishi katika nyumba ya aina yake iliyoko katika eneo la Medina jijini Washington na liko karibu kabisa na ziwa.
James Cutler ndiye alibuni nyumba hiyo kwa kutumia mfumo wa kompyuta na aliijenga kwa kupasua mlima ulio karibu na Ziwa Washington.

Pia amejenga bwawa la samaki chini ya nyumba na limefunikwa na vioo madhubuti. Miongoni mwa samaki waliomo kwenye bwawa hilo ni pamoja na papa ambao hupita na kuonekana katika sebule ya Gates.

Gates pia ana bwawa la kuogelea kwenye nyumba yake. Bwawa hilo limefungwa vyombo vya muziki na pale mtu anapoogelea basi huburudika na muziki laini pia.
Pia mtu akiingia kwenye chumba chochote cha nyumba hiyo, taa huwaka moja kwa moja bila ya kuwashwa na mtu.
Gates ana magari kadhaa yakiwamo 1988 Porsche 959 Coupe, 1998 Lincoln Continental, 1999 Porsche 911 Convertible, Ford Focus na Limousine Chevrolet Corvette.


Pia tajiri huyo anamiliki ndege nne za kusafiria na pia ana helikopta ya kuzungukia nchini Marekani.
Miongoni mwa ndege anazomiliki Gates ni pamoja na Bombardier BD-700 Global Express ambayo bei yake ni karibu Dola 45.5 milioni.
Gates anamiliki boti yenye jina la Goygpus yenye thamani ya Dola 200 milioni .
Tajiri huyo alimwoa Melinda French, Januari 1, 1994. Ana watoto wawili wa kike, Jennifer Katharine Gates (1996) na Phoebe Adele (2002) na mmoja wa kiume Rory John (1999).
Nani zaidi?
Kweli kaka Kanye ameopoa mtoto wa ukweli, lakini kwangu binafsi ninapata tabu nikiangalia kati ya Kim na Amber nani mkali. Hebu angalia mwenyewe.....
Monday, April 30, 2012
Kanumba alijijua anakufa
MTAALAM wa mambo ya mwanga katika utengenezaji wa filamu Swahiliwood, Steven Shoo ëSammy ShooÃ, amedai kuwa marehemu Steven Kanumba alijua kuhusu kifo chake.
Hilo alilijua siku ambayo alikuwa akirekodi filamu yake ya mwisho ambayo alikuwa akirekodi filamu ya Power In Love kutokana na maneno ambayo awali walijua kama utani.
"Tukiwa tunapiga picha hizo za filamu, siku hiyo alikuwa akituhimiza tumpige picha kwa kutumia simu zetu. Nakumbuka aliniambia 'Sam nipige picha bwana, naweza kufa hapa ukakosa picha yangu ukaanza kuhangaika kuitafuta picha yangu katika Internet wakati mpo na mimi hapa... kila mtu anipige piga bwana', alisisitiza lakini katika hali ya utani," anasema Sam.
Sammy, ambaye amekuwepo na marehemu kwa muda mrefu pia na kufanya kazi na mtayarishaji mwingine Ray, anasema pamoja na kutambua kwamba Kanumba alikuwa mtu mwenye utani, lakini katika kufanya naye kazi hata siku moja hakuwahi kumsisitiza ampige picha ya ukumbusho.
Anasema, mara nyingi wanapokuwa kwenye kazi, Seth ambaye ni mdogo wake Kanumba, hupiga picha kwa ajili ya matumizi ya mtandao wake, kutokana na kusisitizwa na marehemu.
Tuesday, April 24, 2012
Hakimu ambembeleza Lulu mahakamani
Msanii wa filamu, Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akibubujikwa machozi kiasi cha kumfanya Hakimu Ritha Tarimo ambembeleze ili kumnyamazisha.
Lulu anashtakiwa mahakamani hapo kwa kutuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba na alifikishwa jana kwa mara ya pili akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.
Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 3:06 asubuhi akiwa katika basi dogo la Magereza pamoja na mahabusu wengine wanawake ambalo lilikuwa likisindikizwa na magari mengine mawili na alikuwa chini ya ulinzi wa askari sita wa kike wa Magereza na askari mmoja wa kike wa Polisi wakishirikiana na askari wa kiume wa Magereza zaidi ya sita.
Mara baada kuingia katika chumba cha Mahakama, Lulu ambaye alikuwa amevalia dira jekundu alianza kulia kwa uchungu hali ambayo ilimlazimu Hakimu Tarimo pamoja na baadhi ya askari kumnyamazisha.
Ulinzi ulikuwa wa kufa mtu
| Ilikuwa ni kazi kupata picha yake, hata JK halindwi namna hii! |
Kutokana na kujaa kwa watu mahakamani hapo, askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza walilazimika kuufunga mlango wa Mahakama hiyo ili kesi hiyo isikilizwe.
Baada ya kesi hiyo kutajwa, Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda aliiomba Mahakama iamuru watu wote watoke nje kwa sababu walikuwa wamefunga njia ili mtuhumiwa huyo aweze kupitishwa.
Hakimu Tarimo alikubaliana na ombi hilo na kuwaamuru askari kusafisha njia ili waweze kumpitisha msanii huyo kwa kile alichosema kuwa Lulu bado ni mtuhumiwa na anaweza kuumizwa.
“Askari safisheni njia ili mtuhumiwa aweze kupita kwa sababu yeye bado ni mtuhumiwa anaweza kuumizwa,"alisema Hakimu Tarimo.
Baada ya kutolewa kwa amri hiyo, askari walitimiza wajibu wao na muda mfupi njia ilipatikana na msanii huyo kutolewa mahakamani hapo.
Jopo la mawakili
Katika kesi hiyo, Lulu anatetewa na jopo hilo la mawakili akiwemo Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Joaquine De- Melo, Kenedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.
De- Melo pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King.
Fungamtama ambaye ndiye kiongozi wa jopo la mawakili hao wanaomtetea Lulu, anakumbukwa kwa kuitetea kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, katika kesi dhidi ya Tanesco, ambayo alishinda na shirika hilo kuamriwa kuilipa kampuni hiyo zaidi ya Sh94 bilioni kwa kuvunja mkataba.
Kibatala ambaye pia anamtetea kada wa Chadema, Fred Mpendazoe katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Segerea, pia ni Makamu wa Rais wa TLS, wakati Massawe anatoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Mawakili hao walijitokeza jana mbele ya Hakimu Tarimo tayari kumtetea Lulu na baada ya mawakili hao kujitambulisha, Wakili Kaganda alisema upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama iipangie tarehe nyingine.
Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mara ya kwanza Lulu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando akikabiliwa na la shtaka hilo la mauaji.
Wakili Kaganda alimsomea hati ya mashtaka alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu katika maeneo ya Sinza Vatican, Wilaya ya Kinondoni, mtuhumiwa alimuua Kanumba. Kanumba alifariki dunia siku hiyo saa 9:00 usiku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya ugomvi baina yake na Lulu.
Hisia zikampanda
Akaanza kulia
Subscribe to:
Posts (Atom)
































